Thursday, February 23, 2012

DAWASCO umekiuka mikataba; hatua za haraka zinahitajika kuboresha upatikanaji wa maji DSM

Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) imekiuka mikataba miwili muhimu inayoongoza kazi zake na kusababisha matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ikiwemo maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.

Imenibidi nitoe taarifa hii kwa umma kwa nilitumia taratibu za kawaida za kiofisi tarehe 14 Februari 2012 kuiandikia barua DAWASCO kuchukua hatua kuhusu tatizo la kutozingatiwa kwa ratiba ya mgawo wa maji katika Jiji la Dar es salaam hali ambayo imesababisha kero ya maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo.

Hata hivyo DAWASCO haikujibu barua husika kueleza hatua ambazo imechukua, hivyo natoa mwito wa wazi wa siku tatu kwa DAWASCO kufanya ukaguzi wa mtandao wa maji na kurekebisha kasoro zilizopo na kutoa taarifa kwa umma kuhusu matitizo ya maji yanayoendelea katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo.

Kazi ya mbunge kwa mujibu wa katiba ni kuwawakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia serikali hivyo nakusudia kuchukua hatua zaidi za kibunge dhidi ya DAWASCO iwapo haitazingatia masharti ya mikataba husika na kushughulikia matatizo ya maji yanayoendelea hivi sasa katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo.

Ikumbukwe kuwa DAWASCO ni shirika la umma lililoundwa kwa tangazo la Serikali nambari 139 la tarehe 20 Mei 2005 kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992.


Tarehe 1 Julai 2005 DAWASCO ilipewa mkataba wa ukodishaji (lease agreement) na DAWASA ambao unaitaka DAWASCO kuendesha miundombinu ya maji na kuhakikisha matengenezo ya mtandao wa maji katika jiji la Dar es salaam.

Aidha, katika kutekeleza mkataba huo DAWASCO inapaswa kuzingatia mkataba wa huduma kwa wateja (Client Service Charter) ambao unaitaka DAWASCO kushughulikia kwa muda maalum malalamiko ya wateja na kutoa taarifa kwa umma kila panapokuwa na matatizo ya maji.

Kwa mujibu wa mkataba wa huduma kwa wateja DAWASCO inapaswa kushughulia malalamiko ya wateja na kuyajibu ndani ya siku tano na iwapo matatizo yaliyopo yanahitaji hatua za kiufundi; DAWASCO inatakiwa kushughulikia matatizo hayo ndani ya siku 30.

Kuanzia mwishoni mwa mwezi Disemba 2011 mara baada ya maafa ya mafuriko katika Mkoa wa Dar es salaam mpaka leo tarehe 22 Februari 2012 nimepokea malalamiko mbalimbali toka kwa wananchi kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo sio nzuri kama ilivyokuwa baada ya hatua ambazo tulichukua kwa nyakati mbalimbali kuanzia Januari 2011 mpaka Septemba 2011.

Itakumbukwa kwamba tarehe 5 mwezi Septemba 2011 nilifanya maandamano ya kwenda DAWASCO nikiwa na wawakilishi wa wananchi wa kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo ambapo tulifanya mkutano na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO.

Kufuatia mkutano huo DAWASCO ilichukua hatua mbalimbali ambazo ziliboresha mgawo wa maji katika maeneo kadhaa ya Jimbo la Ubungo kabla ya ratiba ya mgawo kuvurugika kufuatia mafuriko yaliyokumba mkoa wa Dar es salaam.

Hata hivyo, baada ya mafuriko hayo DAWASCO haikuchukua hatua zinazostahili kwa wakati na kuachia kurejea tena kwa mtandao haramu wa biashara ya maji wenye kuhujumu wananchi hususan wa kipato cha chini katika Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.

Hivyo, bodi ya wakurugenzi ya DAWASCO chini ya uenyekiti wa Mhandisi Suleiman Said Suleiman na Mtendaji Mkuu wa kampuni Jackson Midala wanapaswa kurekebisha kwa haraka mfumo mzima wa ufuatiliaji wa DAWASCO kuwezesha ukaguzi wa ufanisi wa mtandao mzima wa maji.

Katika kipindi hiki cha matatizo makubwa ya maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo DAWASCO iache kuwatumia wafanyakazi wanaohusika na ukaguzi kufanya kazi tofauti za kusoma mita na kugawa Ankara badala yake wafanyakazi tajwa wafanye ufuatiliaji wa dharura wa ufanisi wa mtandao mzima wa maji katika maeneo mbalimbali.

Baadhi ya maeneo ambayo yanapaswa kutembelewa ni kata za Makuburi, Kimara, Saranga, Mbezi Luis, Msigani, Kwembe, Goba, Kibamba, Sinza, Makurumla, Mabibo, Manzese, Ubungo na Mburahati.

Kwa upande mwingine, kwa kuwa mkataba wa huduma kwa wateja unatoa haki kwa wateja wa DAWASCO lakini pia unaeleza wajibu; natoa mwito kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam kutimiza wajibu wa kuwaelekeza wakaguzi husika mitaa yenye matatizo katika mtandao wa maji ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Mkataba huo unawataka wateja wa DAWASCO kutoa taarifa kuhusu uharibifu wa miundombinu, wizi wa maji na kuhusu matatizo ya maji hivyo wananchi watoe taarifa husika na kufuatilia wakaguzi kufika maeneo yao kwa kupiga nambari ya bure 0225500240 au 0762979627 za DAWASCO makao makuu.

Pia, wananchi wanaweza kuwasilisha kero za maji kwa ofisi ya DAWASCO zilizo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam na kupitia nambari zifuatazo: Temeke +255 775016184, Ilala +255 775048556, Magomeni +255 775016179, Boko/Tegeta +255 775048553, Tabata +255 775016181, Kawe +255 775016185, Kinondoni +255 775016180 na Kimara +255 775048554.

Wananchi watumie pia nafasi hii kuwasilisha kwa DAWASCO maelezo na vielelezo kuhusu maeneo ambayo hakuna miundombinu ya maji kabisa au miundombinu iliyopo haijawahi kutoa maji kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kutaka hatua za ziada.

Matatizo ya maji katika maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo yamedumu kwa miaka mingi, wananchi wametupa wajibu wa kuwawakilisha kuisimamia serikali na mamlaka zake kupunguza kero husika kwa haraka hivyo wananchi watarajie vitendo zaidi vya kushinikiza uwajibikaji kwenye sekta ya maji katika kipindi cha karibuni.

Imetolewa tarehe 22 Februari 2011 na:

John Mnyika (Mb)2 comments:

Anonymous said...

go go go jembe,komaaa kitaeleweka tu

Anonymous said...

nitakua nje ya madakwahio am sor 4that,hivi kazi ya makamu wa rais ni kukata utepe na kufunua vipazia vya jiwe la msingi?kila siku ukitizama habari utamkuta huyu mzee anatembea huko anazindua miradi na mingine ya ajabu ajabu wala haina hadhi ya kuzinduliwa,mi naomba akae ofisini amshauri mwenzie nini kifanyike maana nchi inawashinda wasitafute visinizio kjifanya wa misionari
chela wa dom