Friday, March 1, 2013

RUFAA DHIDI YA UENDESHAJI WA BUNGE USIOKUWA WA HAKI NA UKIUKAJI WA KANUNI WA NAIBU SPIKA JOB NDUGAI KATIKA KUONDOA HOJA BINAFSI YA MAJI

Tarehe 28 Februari 2013 nimewasilisha rasmi rufaa kwa mujibu wa Kanuni ya 5 (4) dhidi ya uendeshaji wa Bunge usiokuwa wa haki wa Naibu Spika Job Ndugai kwa kukiuka kanuni ya 58 (5) kwa kulihoji bunge kinyume na kanuni kufanya uamuzi badili wa kuondoa hoja binafsi kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka katika Jiji la Dar es salaam.

Nimefanya hivyo baada ya kupata kumbukumbu rasmi ya Bunge (Hansard) za kikao cha tano cha tarehe 4 Februari 2013 cha mkutano wa kumi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika Mkutano huo Naibu Spika Job Ndugai alisema na kufanya maamuzi kwamba: “Sasa ninahoji wanaoafiki kwamba hoja hii iondolewe waseme ndiyo…..hoja imeondolewa. Walioafiki Wameshinda”; wakati mtoa hoja sikuwa nimeomba idhini yoyote ya hoja yangu kuondolewa.

Maamuzi hayo ni kinyume na Kanuni ya 58 Fasili 5 ambayo inaelekeza kwamba “Endapo hoja imefikishwa Bungeni, mtoa hoja anaweza tu kuiondoa hoja yake kwa kusimama mahali pake na kusema ‘Ninaomba ruhusa kuondoa hoja’ na papo hapo Spika ataliuliza Bunge kama linaafiki hoja hiyo kuondolewa na inapotokea Wabunge walio wengi watakubali, Spika atasema ‘hoja hiyo inaondolewa kwa idhini ya Bunge’ na hoja hiyo itakuwa imeondolewa na Bunge litaendelea na shughuli inayofuata”.

Ushahidi wa Kumbukumbu Rasmi za Bunge (Hansard) za kikao tajwa unathibitisha ukiukwaji huo wa kanuni kama ifuatavyo:

“……..WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa hoja iliyo mbele ya Bunge lako Tukufu ni kuitaka Serikali kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka Jijini Dar es Salaam, ambalo tayari linatekelezwa na mpango maalumu uliotengewa fedha nyingi na Serikali, hivyo naomba kutoa hoja kwamba hoja hii iondolewe. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja……

………..MBUNGE FULANI: Waziri amesema uongo,

amedanganya!

NAIBU SPIKA: Sasa ninahoji wanaoafiki kwamba hoja hii

iondolewe waseme ndiyo.

WABUNGE FULANI: Sasa utaihoji vipi wakati tuna

majadiliano?

WABUNGE FULANI: Ndiyooooooooo!

NAIBU SPIKA: Wanaokataa waseme siyo.

WABUNGE FULANI: Siyooo!

NAIBU SPIKA: Hoja imeondolewa. Walioafiki

wameshinda.

(Hoja ilitolewa iamuliwe)

(Hoja iliamuliwa na Kuafikiwa)

(Hoja Binafsi ya Mheshimiwa John Mnyika

iliondolewa na Bunge)


MHE. TUNDU M. LISSU: Aaaaaa! Aaaaaaaaaaah! Aibu!

NAIBU SPIKA: Hoja imeondolewa na Bunge

linaahirishwa hadi kesho saa tatu kamili asubuhi…….”

Hivyo, pamoja na kuwa Kanuni ya 8 inataka Spika kuendesha shughuli za Bunge na kutoa maamuzi kwa haki, uadilifu na bila chuki wala upendeleo wowote kwa kuongozwa na Katiba ya Nchi na Kanuni za Bunge, Naibu Spika wa Bunge alifanya maamuzi yenye kukiuka kanuni ya 58 Fasili ya 5 kwa kuruhusu hoja yangu kuondolewa kwa hoja iliyowasilishwa na Waziri wa Maji.

Kufuatia rufaa hii Spika atataarifiwa kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) na kuitisha kikao cha kamati ya kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5) ya kanuni za Kudumu za Bunge na kulijulisha bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)

7 comments:

nicholaus marco said...

got your back john!!!!!

Unknown said...

Hawa CCM wanadhani Tanzania ni mali yao wanaiongoza kama watakavyo. kiama yao itafika tu

Anonymous said...

Yale yale ya udhaifu ....

Anonymous said...


NAMMISS SANA MZEE WA SPEED AND STANDARDS. WALAU HUYU ALIKUWA ANAJUA ANACHOKIFANYA... HAWA WAKINA BI KIDUDE NA BWANA WAKE WANAUWEZO MDOGO SANA WA KUSIMAMIA KITI HICHO..

Anonymous said...

Washachoka hao

Unknown said...

Shida ya ndugai sijui anajipendekeza kwa nani. Badala ya kukisaidia chama chake anawasaidia wapinzani kupata umaarufu zaidi. Nadhani kwa kufanya kazi yake vizuri angekisaidia zaidi chama chake. Chama sio team ya mpira, ni uhai wa watu.

Unknown said...

Tembele blog ya

www.bungelawote.blogspot.com uweze kujadili mada mbalimbali na pia utapata downloads ya Windows 8(32bit & 64 bit) na zaidi unaweza kutuma SMS na kupiga simu bure ukiwa hapo, temebelea sasa, www.bungelawote.blogspot.com