Tuesday, March 5, 2013

TUTAFANYA MAANDAMANO KWENDA WIZARA YA MAJI TAREHE 16 MACHI 2013; NIMESHAWASILISHA NOTISI, TUENDELEE NA MAANDALIZI

Tarehe 16 Machi 2013 nitaongoza maandamano ya amani ya wananchi kwenda kwa Waziri wa Maji kusimamia uwajibikaji kuwezesha hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.

Wote mlioshiriki mkutano wa tarehe 10 Februari 2013 (Kwa wale ambao hamkushiriki mnaweza kutazama video hii: http://www.youtube.com/watch?feature=player_embedded&v=O0txSoHqfGY ) , mtakumbuka tulimpa wiki mbili Waziri kujitokeza kwa wananchi kujibu hoja alizokwepa kujibu bungeni.

Tutakusanyika kata ya Manzese eneo la Bakhresa (jirani na daraja) saa 5 asubuhi na tutapita barabara ya Morogoro kuelekea kata ya Ubungo zilipo ofisi za Wizara ya Maji kufuatilia majibu ya ukweli na ukamilifu kuhusu hatua tisa za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka nilizopendekeza kwa niaba ya wananchi bungeni kupitia hoja binafsi na masuala mengine ambayo wananchi watataka yatolewe majibu siku hiyo.

Kila mmoja anaweza kuendelea na maandalizi ya kushiriki kwa kuwa tayari tarehe 4 Machi 2013 nimewasilisha notisi kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni na Maafisa wa Polisi Wasimamizi wa Maeneo kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 43 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi Sura ya 322 (The Police Force and Auxiliary Service Act, Chapter 322).

Itakumbukwa kwamba baada ya kutoa wiki mbili Waziri alijitokeza mara tatu ndani ya wiki hizo; mbili kati ya hizo ikiwa ni kupitia mikutano ya CCM na mara moja ikiwa ni kwenye mkutano kati yake na wafanyakazi wa DAWASA na DAWASCO.

Katika mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika Temeke mwisho tarehe 16 Februari 2013, Waziri hakutoa majibu badala yake alirudia tena maelezo yale yale potofu aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.

Kwenye mkutano wa hadhara wa Goba tarehe 17 Februari 2013 ambapo aliahidi maji kutoka tarehe 20 Februari, 2013 ambayo hayakutoka. Tarehe 23 Februari 2013 nilifanya mkutano Goba na kutangaza namba zake za simu wananchi wamhoji ahadi hiyo na kutaka Manispaa, DAWASA na DAWASCO waweke kambi Goba mpaka maji yatoke.

Shinikizo hilo limesaidia baadhi ya maeneo ya Goba maji yameanza kutoka hata hivyo maeneo mengi bado hali ambayo inahitaji hatua za haraka nilizopendekeza bungeni kuhusu kata hiyo ziweze kutekelezwa.

Kupitia mkutano wake na DAWASA na DAWASCO tarehe 21 Februari 2013 (tofauti na maelezo yake bungeni) alikiri kwamba kuna upotevu wa maji ikiwemo kwa wizi, kuna biashara haramu yenye kuhusisha hujuma ya miundombinu, bei ya juu ya maji na kutozingatiwa kwa ratiba ya mgawo wa maji katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo, zaidi ya wiki moja imepita Waziri wa Maji na Wizara kwa ujumla haionyeshi kwa matendo kuisimamia kwa karibu EWURA, DAWASA, DAWASCO na Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za haraka ambazo nilizieleza kwenye hoja binafsi.

Hivyo, wote mlioahidi kupitia mkutano wa tarehe 10 Februari 2013 kushiriki maandamano na wote ambapo mnaguswa na matatizo ya maji katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar Es salaam tukusanyike Manzese tarehe 16 Machi 2013 saa 5 asubuhi tuandamane kwenda Wizara ya Maji kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara za 8, 18, 20 na 21.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi, 

John Mnyika (Mb)
05/03/2013

5 comments:

Swahili Trainers and Translators CO LTD said...

Wewe tractor siyo jembe tena kata mizizi ya fitina

Anonymous said...

Mheshimiwa hivi ndivyo tutakavyo!

Anonymous said...

Mh. Mnyika, suala hili ni nyeti sana , Wana Malamba Mawili/Msingwa tupo kwenye adha kubwa sana ya maji, tunaomba jitihada zako zizae matunda, nasi tupo pamoja kwa kweli.

Anonymous said...

safi bro matatizo ya wananchi hayatatuliwi kwa kukaa ofisini au kwa kauli za majukwaani lazima vitendo vionekane safi kwa kuonyesha mfano tuko nyuma yako mpaka kieleweke.

Unknown said...

Tembele blog ya www.bungelawote.blogspot.com uweze kujadili mada mbalimbali na pia utapata downloads ya Windows 8(32bit & 64 bit) na zaidi unaweza kutuma SMS na kupiga simu bure ukiwa hapo, temebelea sasa, www.bungelawote.blogspot.com