Saturday, December 26, 2009

Miaka 48 ya Uhuru: Tusake mabadiliko ya kweli tupate uhuru wa kweli-3

Katika makala zangu zilizotangulia nilieleza kwamba kumbukumbu ya miaka ni wakati wa kutafakari taifa letu lilipotoka, lilipo na tunapotaka liende. Katika makala hizo niliitathmini hali ya kiuchumi na kijamii miaka 48 baada ya uhuru na kuhimitimisha kwamba; uhuru wa kiuchumi na kijamii katika taifa letu utapatikana kupitia mabadiliko ya kweli, yenye kuhimili misukosuko ya ukoloni mamboleo; na kujenga taifa lenye kutumia vizuri rasilimali katika kutoa fursa kwa raia wake huku likilinda utadamuni za haki za kijamii (social justice). Katika makala hii nigeukie tathmini ya kisiasa nikiamini kwamba takafakari kuhusu uhuru haipaswi kufanyika tarehe 9 Disemba pekee bali ni mchakato unaopaswa kuendelezwa na mtanzania yoyote mwenye kuamini kwamba uhuru wa kweli, si uhuru wa bendera bali ni uhuru dhidi ya umasikini, ujinga, maradhi na ufisadi. Uhuru wa kweli, ni uhuru wenye kuleta maendeleo kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Mwaka 1961, tulipata uhuru wa kisiasa wa kujitawala na kufanya maamuzi ya kisiasa kwa kushusha bendera ya mkoloni na kupandisha ya Tanganyika. Hii ilikuwa pia ishara ya kubadili watawala kutoka wakoloni kwenda kwa viongozi wazawa kupitia chama cha TANU. Lakini je, ni kweli tuna uhuru wa kweli wa kisiasa ama tuna uhuru wa bendera?

Baada ya Uhuru, viongozi wa kwanza wakiongozwa na Mwalimu Nyerere walianza mikakati ya kujenga taifa (National Building) kwa kuchukua maamuzi magumu ya kujaribu kuleta uhuru na umoja. Kuanzia katika maamuzi kama ya ‘uhuru na umoja’, ‘uhuru na kazi’ na hata baadaye ‘uhuru na maendeleo’; huku kauli mbiu kama ‘siasa ni kilimo’ zikitumika kusukuma ajenda husika.

Baadhi ya maamuzi magumu ya kisiasa ni pamoja na: Muungano katika ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964; kufutwa kwa Mfumo wa Vyama vingi mwaka 1965; kutangazwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967 kulikofuatiwa na utaifishaji (nationalization) wa njia kuu za kiuchumi- kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea; kufutwa kwa dhana ya serikali za mitaa mwaka 1972 na kuanzishwa kwa madaraka mikoani nk. Kwa ujumla kati ya kipindi cha mwaka 1961 mpaka 1985 taifa lilioongozwa kufanya maamuzi mengi ya kisiasa yenye taathira kubwa ya kiuchumi na kisiasa ambayo inaonekana hadi leo. Si lengo la makala haya kuchambua kila uamuzi na faida na hasara zake; katika kipindi husika ambacho Urais wa taifa letu uliongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa ujumla maamuzi mengi yaliyofanyika wakati huo yaliwezesha kujengwa kwa taifa lenye umoja; hata hivyo maamuzi hayo hayo yamedumaza utamaduni wa ushindani katika taifa letu iwe ni kwenye sekta za kiuchumi na hata siasa yenyewe. Mathalani, uamuzi wa kufanya chama kishike hatamu, ulifanya moja kwa moja taasisi ambazo zinapawa kuwa huru kugeuzwa kuwa mihimili ya chama kinachotawala; kuanzia vyama vya wafanyakazi, asasi za kiraia na hata jeshi ambalo baada ya maasi(mutiny) ya mwaka 1964, jeshi mpya la wazalendo(JWTZ) liliundwa na askari kutoka umoja wa vijana wa TANU(TYL). Uhuru wa fikra uliminywa kiitikadi, kisheria na kimatendo kwa kutumia kivuli cha kutaka kujenga umoja wa kitaifa. Wakati huo huo, katika kipindi husika kuliendelezwa kwa kiasi kikubwa sheria na mfumo wa utawala tuliorithi kutoka kwa mkoloni.

Awamu ya Pili ya Utawala Tanzania kati ya mwaka 1985 mpaka mwaka 1995 chini ya Rais wa wakati huo- Ali Hassan Mwinyi; nao ulikuwa na maamuzi yake ambayo ni muhimu kukumbukwa kihistoria. Kwa kiasi kikubwa maamuzi hayo ya kisiasa yakifanyika kwa shinikizo kutoka nje, ambapo maamuzi ya kiuchumi ndiyo kwa kiwango kikubwa yaliyokuwa yakiamua hatma ya mwelekeo wa kisiasa. Kwa masharti ya Benki ya Dunia (WB) na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa(IMF), Tanzania ikafanya ‘geuka nyuma’ ya kisiasa, kwa maelezo ya kufuata sera za ubinafsishaji na soko huria. Kumbe mambo yote yalikuwa ni barakoa (mask) ya kutupeleka kwenye utamaduni wa ubinafsi na soko holela. Kati ya matukio ya kukumbukwa wakati huo ni pamoja na: Maamuzi ya Zanzibar ya mwaka 1991 ambayo yalifuta misingi muhimu ya Azimio la Arusha, hususani iliyohusu maadili ya uongozi na nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Hata hivyo, mageuzi yote hayakuendena na kuandikwa kwa katiba mpya, na matokeo yake ni sheria na hata utamaduni wa kisiasa kuendeleza misingi ya chama tawala kuwa chama dola; mithili ya nchi kuendelea kuwa katika mfumo wa chama kimoja. Ripoti za Tume ya Nyalali na Tume ya Kisanga zinaweza kutupa picha ya ziada ya hali ya kisiasa katika kipindi husika na maamuzi ambayo yalipaswa kufanyika.

Awamu ya tatu ya utawala chini ya urais wa Benjamin Mkapa kati ya mwaka 1995 mpaka mwaka 2005 ulitaasisisha misingi ya soko holela na ubinafsi na hivyo kuliondoa taifa katika misingi ya uwajibikaji na kulitumbikiza katika utamaduni wa ufisadi. Ukiweka katika mizani, mafanikio ya Mkapa katika kuweka misingi ya kiuchumi iliyojikita zaidi katika utandawazi, uwekezaji wa kigeni na unyonyaji wa kodi toka kwa wananchi masikini hayawezi kulingana na hasara ya ufisadi na uuzaji wa rasilimali ambao ulifanyika katika awamu yake ya utawala. Ni katika kipindi hicho hicho ambacho maamuzi ya siasa zetu katika uchaguzi, yameanza kuwekwa katika nguvu zilizo nje ya nguvu ya umma wa watanzania. Uhuru wa kisiasa unazidi kuterereka kwa uhuru wa kiuchumi kupotea na taratibu tumeingia katika ukoloni mamboleo huku watawala wa ndani wakiwa ni makuwadi tu wa siasa za nje zinazotuongoza.

Awamu ya nne imeingia mwaka 2005 chini ya Rais Jakaya Kikwete na kuahidi kuendeleza yale yaliyoachwa na awamu ya tatu kwa ari, nguvu na kasi mpya. Kauli tata baada ya safari za mara kwa mara za nje ya nchi na hali tete ya migogoro katika sekta ya ardhi hususani kati ya wawekezaji kutoka nje na wazawa ni mambo ambayo yanahitaji tafakari ya kina tupate mwelekeo mbadala wa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Miaka 48 baada ya uhuru; tumeweka reheni uhuru wetu wa kisiasa; CCM imeshindwa kutoa uongozi wa kisiasa na kufanya taifa kudumbukia katika siasa chafu na uongozi mbovu. Ombwe hili la uongozi, lenye ishara zote za kushindwa kufanya maamuzi bora katika masuala ya msingi yanayolikabili taifa; limesababisha misingi ya haki na utawala wa sheria inazidi kupuuzwa.

Toka CHADEMA na viongozi wake kwa kushirikiana na vyama vingine tutoe orodha ya mafisadi (list of shame) mnamo Septemba 15, 2007; mafisadi wameendelea kuachwa wakitamba na kuliteteresha taifa. Mtiririko wa matukio unaonyesha kwamba CCM imetekwa na mafisadi, mivutano ndani ya NEC yao na mpasuko wa dhahiri katika kikao cha Wabunge wao na wazee wa chama chao cha hivi karibuni Dodoma; ni ishara za hali hiyo. Lakini watanzania wakumbuke kwamba kutekwa huku na mafisadi, chanzo chake ni viongozi wengi walioko madarakani kuingizwa kwa nguvu ya fedha za ufisadi. Pamoja na Spika wa Bunge kuapa kwamba suala la utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Richmond kumalizika kikao cha Novemba; kikao kimemalizika bila suala hilo kumalizika. Ufisadi wa EPA nawe umefanyiwa usanii wa hali ya juu wa kisiasa, kwa bahati mbaya ukiongozwa na mkuu wa nchi. Hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa bungeni ya kutamka msamaha kwa waliorejesha fedha za wizi; ni sehemu ya hali hiyo. Mhimili wa Bunge, umeshindwa kumwajibisha Rais katika hili kwani hata hotuba hiyo ya Rais pamoja na ahadi za Spika kuwa ingejadiliwa bungeni mpaka leo haijawahi kutolewa. Nachukua fursa hii kutoa mwito kwa ikulu kuiweka wazi Hotuba hiyo ya Rais Kikwete ijadiliwe na umma; kwani muda mrefu sana umepita toka tuelezwe kwamba hotuba hiyo imerudishwa ikulu ‘kukarabatiwa’. Kushindwa huku kuwa na kumbukumbu za Bunge zilizohadharani (Hansard) za suala nyeti kama hili la Hotuba ya Rais Bungeni kuhusu hali ya taifa (state of the nation address) na aibu kwa Spika aliyetangaza kuendesha bunge kwa viwango na kasi.

CCM hii hii leo inabuka kuwaghilibu watanzania kuwa imeanza kutafuta vyanzo visafi vya fedha za kampeni zake. Wakati wetu ni huu; tusidanganyike. Wachukue hatua kwanza kuhusu kampuni ya Kagoda na mengineyo ambayo fedha zake zilitumika kwa wagombea wa chama hicho kwenye kampeni za mwaka 2005. Watanzania wakumbuke kwamba utapeli kama huu wa kisiasa ulifanyika katika uchaguzi uliopita ambapo viongozi hawa hawa wa CCM walizunguka kupokea michango ya wafanyabiashara; kumbe wafanyabiashara hao ndio wale wale wa EPA. CCM iwaeleze watanzania ina mkakati gani wa kuchota fedha chafu katika uchaguzi wa 2010 ambao utakwenda sambamba na mfumo wa kuzisafisha kupitia kinachoitwa michango toka kwa wapenzi na wanachama wake?

Uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa uliofanyika mwaka huu ulikuwa ni aibu kwa taifa na ishara ya wazi ya CCM kuhubiri demokrasia huku ikipanga kila mbinu za kupora ridhaa ya umma miaka 48 baada ya uhuru. Kutokana na serikali yenyewe ya CCM kujisimamia yenyewe uchaguzi; Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikiuka kanuni alizozitunga mwenyewe kwa kutoa tangazo kwenye vyombo vya habari Julai 25, 2009 kuwa uandikishaji wa wapiga kura ungefanyika kwa siku 21 kama kanuni zilivyohitaji katika mwezi Septemba. Lakini cha kushangaza, akatoa tangazo lingine baadaye chini ya siku tisini ambazo kanuni zimeelekeza la kutaka uandikishaji ufanyike mwezi Oktoba; na hivyo kufanya usikamilike chini ya siku 21 kabla ya uchaguzi kama kanuni zilivyohitaji. Akaenda mbele zaidi kutenga kanuni zenye kutoa mwanya kwa watendaji wa kiserikali kusimamia chaguzi hizo na hivyo kutoa mwanya wa uvurugaji wa uchaguzi. Uchaguzi wenye wapiga kura wachache waliolazimishwa kuandika wenyewe majina ya wagombea na vyama vyao. Kwa vyovyote vile, uchaguzi huu hauwezi kuwa kipimo kamili cha mwelekeo wa kisiasa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambao utasimamiwa na chombo tofauti kwa sheria na taratibu tofauti. CCM ikatengeneza mazingira ya kutumia uchaguzi huu kukatisha tama matumaini ya mabadiliko. Waziri Mkuu mwenyewe akawa mstari wa mbele kulipotosha bunge kwa kutangaza matokeo, kabla hata Wizara ya TAMISEMI haijamilisha kupokea matokeo toka maeneo mbalimbali ya nchi. Hivyo, idara ya kumbukumbu za Bunge(hansard) inapaswa itoe hotuba ile hadharani kama ilivyo; taifa liweze kujadili kama kweli matokeo yale ni kamili ama zilikuwa ni propaganda tu za kufanya umma uamini kwamba CCM ilishida kwa kiwango kilichotajwa. Hata hivyo, pamoja na hujuma zote vipo vyama vilivyopanda kisiasa ukilinganisha matokeo ya mwaka 2004 na haya ya 2009; CHADEMA ikiwa kinara katika kundi hilo.

Kama kuna tishio la umoja na amani ya nchi basi ni uchaguzi katika nchi ambayo watawala hawataki kuachia madaraka. CCM inajivuna kwamba inafanya chaguzi za amani huku doa pekee likitajwa kuwa ni chaguzi za Zanzibar. Lakini ukweli ni kuwa hali ya CCM kutumia nguvu za dola, na makada wake kutumia vikundi vya kiharamia kumwaga damu ni utamaduni wao kila wanapozidiwa, kwenye pande zote mbili za Muungano. Viongozi wa CCM ni vinara wa vurugu kwenye chaguzi za marudio kama ilivyothibitika Kiteto, Tarime, Busanda na Biharamulo. CCM ya sasa na viongozi wake ni tishio kwa amani na usalama wa taifa letu hususani katika kipindi cha chaguzi. Kizazi kipya kijikumbushe ujumbe wa Malcom X, ‘ballot or bullet’; tuwabane CCM na mawakala wao kwa nguvu ya umma, tuwaeleze wazi kwamba amani ni tunda la haki. Uzoefu duniani unaonyesha kuwa risasi haziwezi kushindana na umma wenye kutaka kuleta mabadiliko kidemokrasia kupitia sanduku la kura.

Katika kutafuta uhuru wa kweli wa kisiasa tuendelee kudai mabadiliko ya katiba ili tuweze kubadili sheria na mazingira ya kisiasa pamoja na CCM imehodhi mamlaka ya umma na kukataa kuandikwa kwa katiba mpya nchini. Watanzania wasitarajie CCM kwa uwingi wake bungeni ikubali kuandikwa kwa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. CCM wanajua kuwa kuandikwa kwa katiba mpya kutaweka misingi ya uwajibikaji, ikiwemo kushughulikiwa kikamilifu kwa mafisadi. CCM inahofu pia kuwa kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi kutakiondoa chama hicho madarakani. Tutumie mbinu mbadala kusukuma mabadiliko yanayokusudiwa kwa kuunganisha Nguvu ya Umma. Kama ilivyowezekana wagombea wa upizani kushinda katika baadhi ya wajimbo ndivyo ambavyo inapaswa kuwa katika chaguzi zinazofuata. Katiba mpya itaandikwa baada ya kufanya mabadiliko ya kuondoa hodhi ya chama kimoja bungeni na kuchagua uongozi mbadala.

Ili kupata uhuru wa kweli kwa kisiasa tunahitaji mabadiliko ya mfumo wa kiutawala. Haiwezekani tukaendelea kuwa na mfumo wa utawala tuliorithi kwa mkoloni wa kuwapa madaraka makubwa viongozi wa kuteuliwa kama wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa; hodhi ya utawala ikiwa kwa serikali kuu badala ya kuongozwa kwa nguvu ya umma kupitia viongozi waliochaguliwa na umma kidemokrasia. Kwa pamoja tunapaswa kufanya maamuzi ya kulitoa taifa letu katika kufilisika kimaadili na kiitikadi na kukubaliana tunu za kitaifa zenye kuwezesha misingi ya uwajibikaji. Uhuru wa kweli wa kisiasa utakuja kwa kubadili uongozi na kuweka madarakani uongozi wenye dira, maadili na msimamo wa kufanya ukombozi wa taifa kisiasa na hatimaye kuleta tija kiuchumi na manufaa ya kijamii. Hivyo, tuuchukulie uchaguzi wa viongozi kama harakati za kutafuta uhuru wa kweli; tukiacha uchaguzi wetu kutawaliwa na nguvu za ziada nje ya ridhaa ya umma iwe ni kwa fedha haramu au shinikizo la ndani na nje tunaitumbukiza nchi yetu katika ukoloni mamboleo. Uhuru wa kweli ni pamoja na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi huru na haki na uhuru wa kushiriki katika maamuzi ya kisiasa kwa ujumla. Tukiacha viongozi wa kisiasa wakatutawala kwa mwelekeo wao, bila maridhiano ya pamoja; tutakuwa tumepata uhuru tu wakuondoa wakoloni toka nchi za kigeni na kuingiza ‘wakoloni’ wa ndani. Ni muhimu siasa zetu zitatuwezesha kunufaika na rasilimali zetu: iwe ni vipaji vyetu, kodi zetu au maliasili za nchi yetu. Tunahitaji mjadala wa kitaifa kufikia azma hiyo.

No comments: