Saturday, December 5, 2009

Kashfa Kampuni ya Reli: Serikali ya Tanzania, India ziwaombe radhi watanzania

TAARIFA KWA UMMA

KASHFA KAMPUNI YA RELI: WATANZANIA NDIO WAKUOMBWA RADHI

Taarifa inatolewa kwa umma kupitia kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA kufuatia kauli kwamba Ubalozi wa India nchini umeitaka Serikali ya Tanzania kuomba radhi kutokana na kitendo cha wafanyakazi wa Kampuni ya Reli (TRL) kubeba msalaba na kuimba nyimbo za msiba wakati wakiwa kwenye mgomo uliolenga kushinikiza menejimenti ya kampuni hiyo inayoongozwa kwa kiasi kikubwa na raia wa India kutimiza madai yao.

Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA haipendi kuamini kwamba kauli hiyo imetolewa na ubalozi husika kwani ina dalili za kuzusha malumbano ya kidiplomasia baina ya serikali ya Tanzania na India.

Aidha ikiwa kauli hiyo iliyonukuliwa na vyombo mbalimbali vya Habari hususani gazeti la Majira Na. 5813 la tarehe 5 Disemba 2009 ni msimamo rasmi wa nchi ya India, tunaupongeza ubalozi huo kwa kuweka hisia zao hadharani juu ya yaliyojiri katika mgomo wa wafanyakazi wa TRL na hivyo kuibua mjadala wa umma kuhusu masuala muhimu yahusuyo mustakabali wa Kampuni hiyo inayohudumia watanzania na raia wa nchi mbalimbali.

Ubalozi wa nchi hiyo kwa kutoa kauli kama hiyo utakuwa umezingatia misingi ya diplomasia inayosimamia ukweli bila kuendekeza unafiki wa kimataifa. Hata hivyo ubalozi wa nchi hiyo ulipaswa kuzingatia pia kanuni nyingine ya msingi(golden rule) kwenye utamaduni wa kidiplomasia ya nchi kuepuka kutenda ama kusema yale ambayo isingependa kutendewa au kusemwa.

Katika muktadha huo; kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inatoa tamko la kutaka Serikali ya India na hata ya Tanzania kuwaomba radhi wafanyakazi na watanzania kwa ujumla kutokana na yaliyotokea na yanayoendelea kutokea katika kampuni ya TRL.

Serikali zote mbili zinawajibika kubeba mzigo wa lawama, ndio maana kurugenzi ya mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA haikushangazwa sana kuona wafanyakazi wakiwa wamebeba msalaba ambao pengine ni ishara ya mzigo huo kwa menejimenti ya TRL inayotoka India na kwa serikali ya Tanzania inatawaliwa na CCM.

Aidha hatukushangwa na wafanyakazi kuimba nyimbo za msiba wakati wa mgomo wao kwani Kampuni hiyo kwa aina ya mabehema/vichwa vyenye ubovu, kwa huduma mbovu na kwa menejimenti bomu ni wazi kwamba hali ya mambo ni kama katika mazingira ya kifo na kwamba kashfa ya TRL ni msiba wa watanzania. Hata mkataba wenyewe wa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya RITES ya India; ni mkataba marehemu kutokana na maudhui yake.

Hivyo kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inazitaka serikali zote mbili; Tanzania na India, kuwaomba radhi wafanyakazi na watanzania kwa kuwaingiza katika kadhia hii yenye kuleta vilio vya aina mbalimbali kila kukicha.

Ubalozi wa India ndio unaopaswa kuwaomba radhi wafanyakazi kwa kuwa menejimenti mbovu ya TRL yenye raia toka nchini India ndiyo inayochangia katika kuwaingiza wafanyakazi kwenye migomo ya mara kwa mara kutokana na uhai kuwa mashakani kutokana na maslahi na mishahara duni. Aidha ubalozi wa India unapaswa pia kuomba radhi kwa watanzania kutokana na Kampuni yake ya RITES kuingia katika ubia wenye kuua taratibu mfumo mzima wa reli Tanzania kuanzia kampuni yenyewe, huduma zake za usafiri na hata miundo mbinu yake na kufanya hali ya mazingira ya usafiri huo hapa nchini kuwa hatari kwa usalama wa raia.

Katika medani ya diplomasia inafahamika kwamba kazi za Balozi mbalimbali ni pamoja na kuwa mawakala wa masuala ya mahusiano ya kiuchumi na kibiashara; hivyo Ubalozi wa India nchini hauwezi kukwepa lawama kutokana na Kampuni ya RITES toka nchi hiyo kushindwa kuendana na mahitaji ya watanzania na viwango vya kimataifa vya usafirishaji wa reli.

Izingatiwe kuwa nchini India kampuni ya RITES si moja ya kampuni zinazoheshimika katika masuala ya usafiri wa reli; inashangaza kwa ubalozi wa nchi hiyo kuitetea kampuni ambayo ndani ya nchi yao wenyewe haiwezi kupata mikataba ya miradi ya umma nyeti kama walivyoipata hapa Tanzania.

Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inaamini kwamba Ubalozi wa India nchini ulifahamu kabla udhaifu wa Kampuni ya TRL na menejimenti toka nchi yao; lakini haukuishauri wala kuitahadharisha Serikali ya Tanzania kama ambavyo taratibu za diplomasia nyenye dhamira njema; ikiwemo ya kiuchumi inavyohitaji.

Uamuzi wa kunyamaza kimya na hata wa kutoa kauli kama hii yenye kulinda maslahi ya raia wa India pekee bila kuzingatia hali ya wafanyakazi wa Tanzania ni dalili za kwamba Ubalozi wa India ulinyamaza kwa makusudi kuiacha serikali ya Tanzania iingie katika mkataba mbovu na kuletewa huduma/miundo mbinu kanyaboya kwa maslahi yao ya kiuchumi suala ambalo linafanya ubalozi huo uwajibike kuomba radhi kwa watanzania.

Aidha Serikali ya Tanzania inayoongozwa na CCM ndio inayowajibika zaidi kuomba radhi si kwa raia wa India bali kwa wafanyakazi na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kutokana na kusababisha matatizo makubwa yanayotokea katika Kampuni hiyo.

Serikali inayoongozwa na CCM ndiyo iliyopeleka bungeni muswada wa kurekebisha sheria iliyoua TRC, na kuweka vipengele vilivyoruhusu mianya ya kuingia mikataba mibovu ambayo imesababisha msiba kwa sekta ya reli nchini. Matokeo yake ni kwaba hali ya usafiri wa reli inazidi kuwa mbaya usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia hii unazidi kupungua mwaka hadi mwaka; mathalani kutoka tani 1,169,000 mwaka 2005 mpaka tani 429,000 mwaka 2008. Serikali imeingiza fedha za walipa kodi katika uwekezaji wa kibadhirifu na kudhoofisha miundombinu iliyojengwa kwa jasho la umma.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitoa fedha za umma bila kufuata taratibu(misappropriation) kwa ajili ya kulipa wafanyakazi wa Kampuni hiyo; na ikaendelea kuwalipa kwa maelezo kwamba kampuni husika haina fedha. Lakini Serikali hiyo hiyo ikaeleza kauli tofauti inayoonyesha kwamba kampuni ya TRL ilishapatiwa mkopo.

Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inawataka Waziri Mkuu ama Waziri wa Miundo Mbinu kuwaeleza ukweli wote wa Tanzania wa kinachoendelea kutokana na fedha za umma zilizotolewa kwenda kampuni hiyo na mikopo ama fedha zingine ambazo kampuni hiyo ilipokea.

Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi (CHADEMA) ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama aliwasilisha maelezo binafsi kuhusu matatizo ya reli nchini chini ya TRL lakini serikali haikutoa majibu kamili na amekuwa akizungushwazungushwa kuhusu kusudio lake la kuwasilisha hoja binafsi juu ya kashfa ya TRL.

Katika mazingira haya ya utata na hali tete katika kampuni wakati umefika sasa wa Rais Jakaya Kikwete kuelekeza watendaji wake kuweka wazi kwa umma ama kupitia wawakilishi wao Mkataba wa TRL na taarifa yenye kuchambua hali ya mambo katika kampuni hiyo na mazingira ya kuingiwa kwa mkataba ikiwemo kuwataja hadharani wamiliki halisi wa kampuni ya RITES na washirika waliohusika katika kushinikiza Tanzania kuingia katika mazingira haya yanayotishia uhai wa sekta ya reli, wafanyakazi wake, watanzania wanaotumia usafiri huo, uchumi wa nchi na na hali ya maisha ya wadau wote waotegemea njia hiyo kiuchumi ndani ya Tanzania na nje ya mipaka yetu hususani katika eneo la maziwa makuu.

Imetolewa tarehe 5 Disemba mwaka 2009 na:John Mnyika
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje
0754694553

No comments: