Thursday, December 3, 2009

Tuhuma kuhusu Silaha: Akheri nife nikiwa nimesimama kuliko kuishi nikiwa nimepiga magoti

Leo Tarehe 3 Disemba 2009 nasema: Akheri kufa nikiwa nimesimama kuliko kuishi nikiwa nimepiga magoti. Hii ni kauli ya mwanafalsafa na mwanamapinduzi, maarufu kama Che Guevara. Kauli hii ni muhimu kutakariwa na watanzania leo, tunapoendelea kujadili ripoti ya Kikundi cha wataalamu kilichoundwa na UN katika muktadha wa Orodha ya Mafisadi (list of shame) iliyotolewa na CHADEMA. Ripoti ya muda kikundi cha wataalamu wa UN inaitaja Tanzania ama baadhi ya watanzania kuhusika kwa namna moja au nyingine kuwezesha biashara haramu ya silaha kwenda maeneo ya vita DRC na ujangili wa madini toka maeneo hayo; madini ambayo yametapakaa damu ya mauji wa raia wasio na hatia katika maeneo yenye vita vya wenyewe kwa wenyewe (Blood Minerals). Matukio ndani ya ripoti hii yametokea hivi karibuni, katika kipindi cha utawala wa Rais wa awamu ya nne, kupitia serikali ya chama cha Mapinduzi; Jakaya Mrisho Kikwete.

Wakati wa upande mwingine, Orodha ya Mafisadi inataja ushiriki wa serikali na viongozi wake katika makampuni tata kama Meremeta, Tangold, Deep Green Finnance na mengineyo ambayo yamekuwa yakihusishwa na biashara ya utoroshaji wa dhahabu toka maeneo yenye vita. Ukitazama filamu ya Darwins Nighmare, unaweza kupata picha ya uhusiano baina ya biashara hii na nyinginezo na biashara haramu ya silaha. Taarifa zote mbili: ya Kundi ya Wataalamu wa UN na Orodha ya Mafisadi, tumeziweka kwenye mtandao wa www.chadema.or.tz ili watanzania bila kujali itikadi wazijadili taarifa hizi kwa mustabali mwema wa Taifa letu.


Mkutano wangu na wanahabari, nikiwa ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa wa CHADEMA kumjibu Waziri wa Serikali ya CCM anayeongoza wizara ya sekta yangu, na uamuzi wa kutangaza kwamba suala hili lijadiliwe na umma wa watanzania na wawililishi wa wananchi; hakika kwa pamoja vimeanza kutimiza lengo. Wapo waliopinga, wapo waliounga. Wapo waliotukana, wapo waliosifu. Wapo waliotangaza kuniunga mkono; wapo walionitishia kwamba jambo hili ni hatari. Tuendelee na mjadala; ili tutoke na msimamo wa pamoja kama watanzania badala ya msimamo wa serikali ya CCM ambao unajaribu kufunika kombe mwanaharamu apite bila kujali kwamba mficha maradhi kifo kitamuumbua.

Hivyo, naandika kauli hii kwa tahadhari kubwa ya kizalendo kwa kuwa najua suala hili linagusa kwa namna au nyingine vyombo vyeti na masuala tete yanayoelekezwa kwa nchi yetu yanayogusa jeshi, polisi, usalama wa taifa, chama tawala, serikali yake, na viongozi wake. Mambo ninayoandika pia yanagusa genge la mafisadi na watumiaji vibaya wa madaraka; wengine wakiwa ni wafanyabiashara, wengine wakiwa ni viongozi, wengine wakiwa ni wahalifu waliokubuhu na waasi wenye kufanya mauaji. Haya ni mambo hatari yanayotishia maisha si tu ya mtu mmoja mmoja bali hata amani katika nchi yetu kwa ujumla. Ndio maana nimeikumbuka kauli hii ya Che Guevara; Akheri Nife nikiwa nimesimama kuliko kuishi nimepiga magoti.


Sasa nijibu hoja za waliotaharuki ama kukurupuka tena na kujibu tamko langu nililolitoa kwa niaba ya CHADEMA ili mjadala uendelee kwa manufaa ya taifa letu na dunia kwa ujumla. Pia, nitazigusia hoja za walioniunga mkono mpaka kieleweke.

Waziri Membe amerudia tena tabia yake ile ile ya kutoa kauli bila kufikiria; bila kujadiliana. Yeye ameamua kusema kwamba CHADEMA iache siasa zenye kuichafua Tanzania; itangulize uzalendo. Sasa nani anaichafua Tanzania; kati ya waliofanya ufisadi na/ama kutumia madaraka vibaya na kuitumbukiza Tanzania katika kashfa kama hizi za usafirishaji wa silaha na utoroshaji wa madini kutoka maeneo yenye vita vya wenyewe kwa wenyewe au mtu anayetaka mjadala kuhusu suala hili ili utoke msimamo wa pamoja wa wazalendo wote wenye kukerwa na mambo hayo ili kulirudisha taifa kwenye mkondo unaostahili wenye kulinda heshima ya Tanzania kitaifa na kimataifa? Membe angetaka kutanguliza maslahi ya pamoja ya Tanzania asingekurupuka kutoa kauli ya serikali ya CCM bila kushirikisha umma wa watanzania ama wawakilishi wa wananchi. Membe hana haki ya kusema kwa niaba ya watanzania katika masuala tata bila kupata maoni yetu au ya kambi yetu bungeni. Ndio maana narudia kusema; kila anachokisema ni msimamo wake na serikali ya chama chake; hakiwakilishi msimamo wa watanzania wote, mimi nikiwa mmoja wao. Kama alitaka watanzania tusivuane nguo hadharani; yeye kwa kuwa ndiye yuko kwenye serikali; kabla ya kutoa kauli, walau angeomba ushauri toka kwa wenzake tulio katika upinzani tuliopo kwenye sekta yake, mwanadiplomasia kama yeye anapaswa kujua umuhimu wa maridhiano baina ya viongozi kabla ya kutoka hadharani katika masuala tete ya kitaifa. Ujumbe wangu kwa Membe, mtu mzima akivuliwa nguo; huchutama, watanzania tumevuliwa nguo, tuchutame; yeye amejivua nguo kwa kauli yake, achutame. Narudia tena kutoa msimamo wangu binafsi kuwa niko tayari kwa majadiliano kama watanzania kuhusu suala hili ili tutoke na msimamo wa pamoja kama taifa. Lakini majadiliano yatakuwa na maana kama tu Membe akiacha propaganda nyeusi dhidi ya CHADEMA, ama sivyo nitashindwa kutofautisha kati yake na Waziri wa nchi moja ya Mashariki ya Kati; ambapo majeshi yalikuwa yakikaribia kuingia mji mkuu na ikulu; yeye alikuwa busy kueneza propaganda kuwa ‘sasa adui ndio anakaribia mstari wa kifo’. Matokeo yake yeye na Rais wake waliishia kukamatwa na kufa vifo vya aibu.

Membe ametaka tupeleke ushahidi kwake au tunyamaze; staili ile ile iliyotumiwa na Wazee kama wakina Kingunge mara baada ya Mzee mwenzake Dr Wilbroad Slaa kuanika hadharani Orodha ya Mafisadi(List of Shame). Mzee huyu wa CCM, wakati huo akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais kwenye wizara iliyodumu kwa muda mchache iliyojishughulisha na mahusiano ya kisiasa na kijamii; huku ikiweka kipaumbele katika kazi ya kuwasafisha mafisadi. Kuhoji uzalendo wa wanaotaka watanzania waliotajwa kwenye ripoti ya Kikundi cha Wataalamu kilichoundwa na UN ni sawa na kuwatetea mafisadi ama waliotumia vibaya madaraka yao waliotuhumiwa kwenye ripoti husika. Waziri Membe kwa uzoefu wake wa ukachero naamini anafahamu kabisa kwamba tuhuma za Tanzania kujihusisha na vita vya DRC zilianza toka wakati taifa hili linaasisiwa. Tofauti ya watawala wa sasa ni kwamba uongozi wa Nyerere ulikuwa unasema wazi kuwa unasaidia waasi, na UN inajua. Lakini wakati ule walioitwa waasi ni wazalendo waliokuwa wakipambana dhidi ya watawala wa kidikteta ambao walikuwa ni makuwadi wa ubeberu na ukoloni mamboeleo katika Afrika. Sera ya wakati huo ya mambo ya nje ya Afrika ilikuwa ni kuleta ukombozi Afrika nzima (hata ikiwa ni kwa kuunga mkono vita vya msituni) na kueneza umajumuhi wa kiafrika (Pan Africanism). Ndio maana wanamapinduzi kama wakina Che, na wengine walikwenda DRC kupambana, na serikali ya Tanzania ya wakati huo ilikuwa mstari wa mbele kwenye ukombozi kusini mwa Afrika.

Serikali ya sasa ipo tofauti; kwanza haina msimamo; pili, sera yake ya mambo ya nje haieleweki; tatu, masuala ya sasa ya usafirishaji wa silaha ama utoroshaji wa madini toka maeneo yenye vita ambao yanasemwa kuwa yanafanywa na serikali ama watanzania yanahusu zaidi miradi binafsi ya watu ambayo wanaindesha kwa ama kuzitumia taasisi za kiserikali au kuruhusu mianya kwa kutowajibika kusimamia utawala wa sheria ikiwemo kuheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa (UN) ambayo nchi yetu imetia saini.

Waziri Membe anapaswa kutoa kauli ya kuunga mkono rai yangu niliyoitoa kwenye mkutano wangu na waandishi wa habari Disemba Mosi, 2009: Kwamba wazalendo wote, waliokerwa na Tanzania ‘kuchafuliwa’ na ripoti hiyo ya Kikundi cha Wataalamu wa UN, wanapaswa kuwashinikiza watanzania wote wanaoishi Dar es salaam, Kigoma na kote duniani ambao wametajwa kwenye taarifa hiyo kwa majina yao; wajitokeze kutoa kauli za kusafisha majina yao, tukiridhika na hoja zao, katika utetezi wao; basi na sisi tutajiunga katika kundi la kuwatetea na kuwasafisha. Viongozi na taasisi za serikali zilizotajwa kwa namna moja au nyingine katika taarifa hiyo iwe kwa majina au kwa matukio zijitokeze kuelezea kutajwa kwao; tukiridhika na maelezo yao na vielezo vyao, tutajiunga katika kazi ya kizalendo ya kuwatetea na kuwasafisha. Na hii isiwe kwa taarifa ya UN pekee; iwe pia Orodha ya Mafisadi, katika vipengele vinavyohusiana na Kampuni za Meremeta, Tangold, Deep Green nk. Membe kama mseminari anajua kuwa vitabu vyote vitakatifu na vitukufu vinatamka kwamba haki huponya taifa; kwa hiyo ni ukweli pekee ndio utakaotufanya watanzania kuwa huru dhidi ya kadhia hii.

Nimesoma kauli ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyonukuliwa katika vyombo vya habari vya habari; kwamba ripoti ile ‘sio rasmi’ na kwamba ‘wako tayari kuishirikisha Tanzania katika kuifanyia mapitio ripoti husika’. Na kwamba ripoti hiyo isihusishwe moja kwa moja na Sekretariati ya Umoja wa Mataifa, na Mashirika yake; sina tatizo na kauli hizi. Hivyo, watanzania, wanahabari na wachambuzi; wanapaswa kuendelea kuinukuu na kuirejee ripoti hiyo kuwa ni ripoti rasmi kabisa na ya mwisho ya Kundi la Wataalamu iliyoundwa na UN; ripoti hii inaweza kubadilika tu, ikiwa aliyepewa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Vikwazo (Sanctions Committee) atajadiliana na wajumbe wake na kutoa ripoti mbadala. Ama ataipandisha juu zaidi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa(UN Security Council) ambalo ndio chombo chenye mamlaka ya kutoa maazimio kuhusu masuala hayo. Nilitarajia ripoti kama hii ya ukomavu wa kidiplomasia toka kwa umoja wa mataifa. Kauli hii ya kisiasa yenye kuendana na nadharia ya ‘ukila na kipofu usimshike mkono’ inasadifu maudhui ya Mkataba wa Kuundwa kwa umoja wa Mataifa(UN Charter), Tamko kuhusu Haki za Binadamu(UDHR)- kama vile UN imeamua kumpa mtuhumiwa Benard Membe na serikali yake haki ya kusikilizwa. Kauli hii inaendana pia na Mkataba wa Vienna; ambao Benard Membe aliutumia kulipotosha Bunge kwa kutoa karipio kali kwa mabalozi wa nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa kutokuingilia ‘mambo ya ndani’ ya Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Kauli ambayo iliicha uchi serikali ya Tanzania kuhusu dhamira yake ya kutaka wabaki wenyewe; sijui wanataka kuiba tena kura uchaguzi ujao!.

UN ikiwemo ofisi ya Umoja wa Mataifa hapa Tanzania chini ya mpango wao wa kufanya kazi kwa pamoja kama familia(One UN Programme) inapaswa kuzitafsiri kwa pamoja kauli hizi za serikali ya CCM. UN inabidi itambue kwamba serikali ya CCM ya leo sio ile ya Mwalimu Nyerere ya ukweli na uadilifu. Hivyo UN, inapotafakari matukio ya sasa irejee na matukio ya nyuma, kwani ni UN hii hii imekuwa ikiisifia kupindukia serikali ya CCM kwa demokrasia; imekuwa ikutuma waangalizi wa uchaguzi(Elections Observers) wake na kutangaza chaguzi kuwa huru na haki. Matokeo yake CCM ya kina Membe, imekuwa ikibaki yenyewe; waangalizi wa UN huja mwishoni, na huja maeneo machache; sehemu kubwa ya nchi CCM inabaki yenyewe ikisimamia uchaguzi wenyewe kupitia Tume isiyo huru ya uchaguzi ambayo Makamishna wake wanateuliwa na serikali hiyo hiyo inayoshiriki uchaguzi. Lakini mbaya zaidi; tume hiyo haina watendaji wake huru katika ngazi za kata na majimbo, inatumia watendaji wa serikali walioteuliwa moja kwa moja na serikali yenyewe kama watendaji wa kata na wakurugenzi wa halmashauri. Tume haizingatii kuwa watendaji hawa wamekuwa wakipewa maelekezo na Mawaziri hao hao wa serikali kabla ya uchaguzi kwamba atayeachia eneo lake liende upinzani atakuwa amepoteza ajira yake aliyoteuliwa. Matokeo yake ni CCM kushinda kwa kishindo na hivyo kuwa na hodhi (monopoly) ya chama kimoja bungeni; na hivyo kupunguza uwezo wa kambi ya upinzani kuiwajibisha serikali kikamilifu. Hivyo, wakati tunatafakari ripoti ya Kikundi cha Wataalamu kilichoundwa UN; ni wasaa pia wa UN Tanzania kupitia UNDP kuongeza kasi ya kuisimamia serikali kutekeleza marekebisho ya kisheria na kitaasisi ya kuwezesha uchaguzi wa 2010 kuwa huru na haki. Hii ni kupitia programu yake ya kusimika demokrasia(deepening democracy program) na kusimamia vizuri mfuko wa uchaguzi wa mwaka 2010(UN Basket Fund for Elections).

Kwa upande mwingine, naiomba Ofisi ya Umoja wa Mataifa hapa nchini (UN Tanzania) itoe tamko tena kufafanua yafuatayo kwa kuwa kauli ya UN inaweza kutafsiriwa vibaya na Serikali ama wasioitakia mema Tanzania kufunika mjadala kuhusu ripoti ya Kundi la Wataalamu lililoundwa na UN yenyewe kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa maazimio rasmi kabisa ya UN hio hio ambayo Tanzania ni moja ya nchi wanachama.

UN ijibu maswali na kufafanua masuala yafuatayo: Mosi; Je, Kikundi cha Wataalamu kilichoundwa na UN haikuwasilisha ripoti ya mwisho kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Vikwazo iliyoundwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa azimio namba 1533 la mwaka 2004 ambalo serikali ya Tanzania inalitambua? Pili; kundi kazi hilo halikupewa jukumu na Umoja wa Mataifa kufuatilia kama nchi wanachama zimetimiza aya ya 5 ya azimio namba 1807 la mwaka 2008 la Baraza la Usalama ambalo limezitaka nchi wanachama za UN ikiwemo Tanzania kuitaarifu kabla(inadvance) kuhusu kusafirishwa kwa silaha na mambo yanayohusiana nayo kwa ajili DRC au msaada wa, ushauri au mafunzo yanayohusiana na operesheni za kijeshi? Je, ni kwa kiasi gani Tanzania imetekeleza azimio hilo kwa kulingisha kati ya taarifa za serikali na tafiti huru zinazofanyika ikiwemo hii ya Kundi la Wataalamu lililoundwa na Umoja wa Mataifa wenyewe.

Je, Umoja wa Mataifa haukulipa Kundi hilo la Wataalamu jukumu la kutoa taarifa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanyika ambao ni kinyume na aya ndogo 4(d)(e) na (f) ya Azimio namba 1857 la mwaka 2008 la Baraza la Usalama? Je, ni kwa kiasi gani Tanzania au watanzania wametajwa kushiriki katika vitendo hivyo kwa kurejea taarifa ambazo Tanzania imekuwa ikizitoa ukilinganisha na ripoti ya Kundi la Wataalamu lililoundwa na UN ambalo limeeleza kwamba kuna vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu vimefanyika ambavyo ni kinyume na sheria ya kimataifa ya ubinadamu(International Humanitarian Law).

UN imesema kwamba iko tayari kuishirisha serikali ili kuisuka upya ripoti husika. Sina tatizo na kauli hii ya UN pia. Imetolewa kidiplomasia. Kauli hii haifuti ukweli kuwa ripoti ya mwisho ya Kundi la Wataalamu wa UN imeshatolewa na imeshasambaa; namna ya kuepuka tuhuma zilizotolewa na ripoti ya awali ambayo serikali imeamua kuziita za kizushi zenye nia mbaya ya kuichafua Tanzania. Tafsiri ya kauli hii ya serikali ya Tanzania ni kuwa UN iliunda timu ya wataalamu wa uzushi, wenye nia mbaya ya kuichafua Tanzania: haya ni matusi kwa UN na tuhuma nzito kwa wataalamu hao kwa ubinafsi wao na taasisi wanazoziwakilisha katika kazi hiyo. Haitarajiwi kwamba Kundi la Wataalamu na hata UN yenyewe kwamba wataicha kauli hiyo kupita bila kutolewa kauli. Lazima wote waungane kuweka wazi; tatizo linaweza lisiwe kufilisika kitaalamu kwa UN; kundi lake la wataalamu na taasisi zao; tatizo ni kufilisika kimaadili kwa Membe na serikali yao ya CCM ambao wako tayari kuweka pembeni taaluma zao na wataalamu wao. Na kutoa kauli za kihuni ambazo hazistahili kutolewa katika medani ya diplomasia; tena kuhusu UN, chombo kinachounganisha mataifa yoye duniani ambacho kila kinapotoa taarifa za kuisifia serikali hiyo hiyo ya CCM Membe na wenzake wamekuwa wakiisifu kwa utalaamu wake na wataalamu wake wanaofanya tafiti hizo. Kama Waziri Membe anaamini kwamba UN na timu inazounda zinaweza kuwa ‘unproffessional’ kama alivyoeleza; basi atamke kutilia mashaka ripoti zote ambazo wamekuwa wakizitumia kujisifia, na kutubeza wakosoaji wa taarifa hizo. Halafu anatulazimisha tutangaze kwamba kauli yake hiyo ni ya kulinda ‘maslahi ya taifa’; Membe afafanue ni maslahi gani hayo ya taifa anayoyalinda kwa kauli hiyo ya kihuni? Membe anatakiwa kutuomba radhi watanzania, na kuiomba radhi UN kwa kusema maneno ya kihuni kwa kutumia cheo cha serikali cha uwaziri wake wa mambo ya nje na mahusiano ya kimataifa kwa kuwa mishahara na masurufu anayopata kumwezesha kutoa kauli hizo vyote vinavyotokana na kodi za watanzania wote iwe wanaCHADEMA au hata wasiokuwa na vyama.

Waziri Membe na serikali yao chini ya CCM, wana dalili zote za kulewa madaraka; madaraka hulevya, madaraka zaidi hulevya zaidi. Ndio maana viongozi wa serikali ikiwemo mawaziri wa wizara nyeti kama utawala bora inayosimamia idara ya usalama wa taifa na hata mawaziri wa wizara nyingine muhimu katika nchi yetu, wanamazoea ya kuropoka na kutoa kauli za kebehi na kupuuza hata mambo tete na tata ya kitaifa. Lakini katika hili, nawaomba sana watoe kauli za kujibu hoja kwa hoja kuhusiana na mambo yaliyoibuliwa katika ripoti ya Kundi la Wataalamu wa UN ambayo imetaja masuala yanayogusa wizara zao ama sekta zao; na wajibu tuhuma zenye maelezo na vielelezo kwa kutoa maelezo na vielelezo.

Ndio maana nawakumbusha tena kauli tuliyowaeleza watanzania mwaka 2010; kwamba mabadiliko ya kweli katika taifa letu; hawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile; chenye uoza ule ule wakiendeleza yale yale; kwa ari, nguvu na kasi mpya(Anguka); kwa falsafa ya chukua chako mapema, ya chama cha mafisadi(ccm); Tanzania yenye neema, haiwezekani.

Kosa kubwa la Waziri Membe katika sakata hili ni kulibeba zigo hili kashfa ya Taifa mwenyewe; tuhuma za ripoti hii ya Kundi la wataalamu lililoundwa na UN zitamuelemea. Wakati umefika sasa wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwashinikiza Mawaziri wengine ambao sekta zao zimeguswa kutoa kauli za kujibu ama kufafanua hoja zilizoibuliwa ndani ya taarifa hiyo, ambayo Membe alishafanya kosa la kuitumbukiza serikali kwenye malumbano mapema kwa kuliibua suala hili na kuituhumu UN kabla hata Tanzania kufafanua ama kujieleza kwenye Kamati ya Vikwazo.

Mawaziri wote hawa watatu, wameshavuka umri wa ujana kwa mujibu wa sera ya Tanzania ambao umekomea miaka 35; lakini kwa kuwa chama cha zamani CCM na serikali yake inaendelea kuwatambulisha kuwa ni mawaziri vijana, niseme kwamba nawaomba mawaziri hawa watoe matamko ya kina kumjibu kijana ‘mwenzao’ toka chama cha kizazi kipya, CHADEMA. Nawaomba wasinitazame kwa umri wangu, bali wazitafakari hoja zangu ambazo nazitoa kwa nafasi yangu ya kichama; Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya kimataifa, lakini pia kama raia wa Tanzania ambaye Membe ambaye serikali imetoa kauli kwa niaba yake isiyokubalika.

Mawaziri wawili wanaopaswa kutoa kauli zao za kina kuhusu Ripoti hii ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Hussein Mwinyi na Waziri wa Usalama wa Raia; Lawrence Masha.

Hawa wasipojibu hoja; itathibisha kauli yangu niliyoitoa wakati nikifungua Mkutano wa Baraza la Vijana wa CHADEMA Kanda Maalum ya Dar es salaam tarehe 29 Novemba 2009 kwamba kauli ya Rais Kikwete ya kusema kwamba akichaguliwa tena atateua mawaziri wengi zaidi vijana ni kauli inayostahili kutozingatiwa na vijana makini. Nilieleza wazi msimamo wangu kwamba mwaka 2005; Kikwete aliwatapeli vijana kwa kutoa ahadi za ajira kwa vijana na kuwapa fursa vijana kwa kiwango ambacho hajakitimiza mpaka sasa hivyo hakuna sababu ya kumpa nafasi ya pili. Kadhalika niileza kwamba hata vijana wachache aliowateua wengi wao wakiwa ni vijana wa vigogo ndani ya chama hicho hicho kama Tanzania ni nchi ya kifalme ambayo uongozi ni wa kurithi hawana mchango wowote wa maana kwa vijana wenzao na hata kwa taifa. Nikahitimisha kwa kusema wazi, kwa aina hii ya vijana wa CCM; ni afadhali kuwa na Wazee kama Dr Slaa wenye kutoa uongozi bora na kutetea maslahi ya Taifa kuliko vijana hao. Hivyo, nikawataka watanzania kufanya mabadiliko kamili ya utawala ili kuweka madarakani chama cha kizazi kipya, chenye sera mbadala na uongozi bora wa vijana makini wa sasa na vijana mahiri wa zamani(wazee) wenye kukubali mabadiliko.

Pamoja na kuwa Waziri Mwinyi yeye alishatoa kauli fupi ya kukanusha tu kwa ujumla bila kujibu hoja kwa hoja. Pamoja na kuwa natambua kwamba ni muhimu kwa Jeshi letu, kutunza siri za mikakati yetu ya kijeshi. Bado Waziri Mwinyi anawajibu kutoa kauli za ufafanuzi. Waziri Mwinyi ajibu: Je, kwa kuwa Balozi wa Tanzania Burundi ambaye alikuwa ni mmoja wa majenerali wa jeshi, namba yake ya simu imetajwa kutumika kuwasiliana na waasi; JWTZ haina sera ya kuendelea kuwatumia maafisa wake waandamizi wa jeshi wanaoitwa wastaafu, wanaotumwa kwenye nchi zenye vita kama ilivyo DRC kuweza kufanya kwa barokoa ya ubalozi majukumu yanayoyofanana na uambata wa kijeshi? (Millitary attacheship). Kama hivyo ndivyo, anaweza kutuambia ni mawasiliano gani ya kijeshi yalikuwa yakifanyika baina ya namba ya simu ya balozi wetu na makamanda wa vikundi vya waasi DRC hususani FDLR na maswahiba wao ndani FARDC? Kwa kuwa mabalozi wetu kuwasiliana na vikundi vya waasi katika nchi ambazo serikali yetu inatambua serikali zake za kiraia ni jambo lisilokubalika na halina uhusiano wowote na ‘siri kuu za jeshi’ wala ‘maslahi ya taifa’; kwanini nini serikali isituleze mawasiliano yaliyokuwa yakiendelea kama inavyotuhimiwa kwenye ripoti ya kundi la Wataalamu lililoundwa na UN? Kwa kuwa silaha za kivita ni kubwa, sio ndogo kama sindano kiasi kwamba zinaweza kupita bila kuonekana; Waziri waulinzi anazielezeaje tuhuma ya silaha kupitishwa Tanzania ambazo zimeelezwa na Kundi la Wataalamu wa UN kwa maelezo na vielelezo? Anaweza kulieleza taifa silaha hizo zimekwenda nchi gani na kwa makubaliano gani ya kijeshi? Mwisho, kwa kuwa Kamati ya Vikwazo ya UN kuhusu DRC iliundwa toka mwaka 2004; pamoja na kuwa ripoti ya Kundi la Wataalamu wa UN imegusia zaidi miaka ya 2007 mpaka 2009; Waziri anazizungumziaje taarifa zilizozagaa katika mitandao mbalimbali zinazohusisha Meremeta, Tangold; Deep Green na makampuni mengine yaliyosajiliwa kwa majina ya vigogo wa serikali ya awamu ya tatu ambayo yanatajwa kuhusika na biashara haramu za silaha na utoroshaji wa madini toka maeneo yenye vita; kampuni ambazo mojawapo serikali imesema kwamba inahusika na JWTZ? Izingatiwe kuwa CHADEMA ilishaweka msingi wa taarifa hizo kwenye orodha ya mafisadi iliyotolewa 15 Septemba 2009.

Waziri Masha naye avunje ukimya kwa kuwa mjadala huu unaonyesha kwamba usalama wa raia Tanzania upo mashakani?
Jana tarehe 2 Disemba 2009 Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa Tanzania haihusiki kwa namna yoyote ile katika kashfa ya kuwapatia silaha waasi wa serikali za mataifa mengine kama ilivyotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Mratibu wa Udhibiti wa Silaha hapa nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Dominick Hayuma, amesema kuwa taarifa za Kundi la Wataalamu lililoteuliwa na UN hazina ukweli wowote.
Amesema kuwa Tanzania ina uhusiano mkubwa na serikali za nchi jirani na ndiyo maana majeshi ya polisi katika ukanda wa nchi za Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika na zile za kusini mwa Afrika (SADC) zinashirikiana katika masuala ya operesheni kwa lengo la kudhibiti kwa pamoja vitendo vya kihalifu.
Amesema kuwa kuna baadhi ya mashirika ya ndani na nje ya nchi wanakusanya taarifa za uongo kwa lengo la kujipatia fedha ama kuleta uchochezi baina ya nchi moja na nyingine.




Nichukue fursa hii kuwatahadharisha wataalamu wetu wa polisi kutokuingizwa kutoa kauli za kisiasa katika mambo yanayostahili maelezo na vielelezo. Ni vizuri zikatolewa kauli za kisera kuhusu masuala hayo; ushahidi wa kuingia ama kutoka kwa silaha za kijeshi katika nchi yetu niliushuhidia mwenyewe Biharamulo wakati wa uchaguzi wa marudio; katika tukio ambalo nitalizungumzia siku za usoni. Niwaombe polisi ambao tunawalipa kwa kodi zetu, wakae mbali na mijadala ya kisera na ya kisiasa ili kutenganisha kati ya jeshi na propaganda za wanasiasa. Tabia hii ya kutumwa na viongozi wa CCM ndio ambayo inafanya Polisi wetu kushiriki katika kuiba kura na kuhujumu wapinzani wakati wa uchaguzi. Polisi wetu wajue kwamba mishahara midogo wanayolipwa na maslahi duni wanayoyapata ni matokeo ya uongozi mbovu wa serikali hiyo hiyo ya CCM inayofanya waweke pembeni maadili ya taaluma zao; na kuitetea na hata kuipigania nyakati za uchaguzi. Hivyo, polisi ikae mbali na mapambano ya kisiasa baina ya vyama, ikiwemo mapambano ya hoja kwa ajili ya kupata msimamo wa pamoja wa watanzania. Polisi ibaki na jukumu la kusimamia sheria na kuhakikisha kwamba utawala wa sheria unazingatiwa badala ya kukanusha tu bila maelezo na vielelezo ripoti ya Kundi la wataalamu wa UN ambayo imewataja kwa majina watanzania wanatuhumiwa kuvunja sheria lakini polisi haijawakamata mpaka sasa.

Waziri Masha akitoa tamko natarajia atatangaza kutoa maelekezo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwachunguza watu wote na taasisi zote za Tanzania zilizotuhumiwa kwenye ripoti hiyo likiwemo jeshi la polisi lenyewe. Waziri Masha ajibu maswali na kufafanunua masuala yafuatayo: Je, taarifa ya kwamba polisi waliizunguka meli inayotuhumiwa katika ripoti hiyo ya Kundi la Wataalamu wa UN anaizungumziaje? Je, polisi hao walikuwa wa nchi gani? Kama ni watanzania walikwenda kufanya nini kwa maelekezo ya nani? Aidha ripoti ya Kundi la Wataalamu, inataja kwamba yapo maduka ya masonara yaliyokuwa yananunua madini yaliyotoshwa kutoka DRC? Na kwamba kwa maelezo ya mmojawapo wa wamiliki wa maduka yaliyotajwa kwenye taarifa hiyo alidai kwamba kuna wakati ambapo idara ya uhamiaji iliwahi kuendesha msako dhidi ya wafanyabiashara hao? Je, serikali inayazungumziaje madai hayo? Je, serikali yake iko tayari kuwachunguza raia wote wa kigeni wanaotajwa kwenye ripoti hiyo wanaoishi mpaka sasa Dar es salam, Kigoma na kwingineko katika nchi yetu? Je, Wizara yake inamzungumziaje raia wa DRC aliyetajwa katika ripoti ya Kundi la Wataalamu wa UN kwa jina la Bande Ndagundi, ambaye anatuhumiwa kuishi nchini kwa zaidi ya miaka 27 anayejishughulisha na biashara zinazohusiana na masuala ya kijeshi? Je, Waziri Masha au wawakilishi wake wamewahi kuwasiliana na mtu huyo anayedaiwa kuendelea kuishi Dar es salaam? Ni muhimu kwa Waziri kutoa kauli kuhusu mtu huyu kwa kuwa imeelezwa kwa uwazi ikiwemo kwa yeye mwenyewe kusema kwenye barua zake ikiwemo ile ya tarehe 17 July 2009 kuwa ana mawasiliano ya karibu na viongozi wa juu wa serikali, police, jeshi na chama tawala.

Masuala haya na mengine mengi zaidi nikayoyachambua kadiri siku zinavyokwenda yanapaswa pia UN na Kundi la Wataalamu wake kuiuliza serikali itoe maelezo ya kina wakati wa mapitio ya taarifa husika. Ni utaratibu wa kawaida kwamba ufuatiliaji kama huu uliofanywa kwa kuwa ulihusu Tanzania; serikali itapewa fursa kuandika ripoti ya nchi (country report) kufafanua mambo ambayo yametajwa kabla ya kamati ya vikwazo kufanya maamuzi yake ama kuikubali ripoti husika na mapendekezo yake ama kutoa maelekezo mbadala ya kutaka uchunguzi zaidi katika maeneo ambayo Kundi la Wataalamu limeeleza katika ripoti yake kuwa uchunguzi wake bado haujamilika. Inashangaza kwamba serikali inatumia nguvu kubwa, kubeza ripoti hii na kutishia wanahabari wasiendelee kuandika wakati ripoti imeweka bayana kwamba uchunguzi bado haujakamilika; serikali itaweka wapi uso wake kama uchunguzi zaidi ukaibua uchafu zaidi?

Kwa hiyo nautoa ujumbe huu leo, Tanzania ikiungana na Nchi zingine duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya walemavu, ambao wengine wametoka na vita hususani mabomu ya ardhini(land mines) yaliyotapakaa kila kona ya Afrika; kuomba ujumbe huu usambazwe wote au kwa kunukuliwa sehemu na njia zote za mawasiliano ya umma; iwe ni magazeti, radio, televisheni na TEKNOMA(ICT). Ukiwa hapa nyumbani na umeguswa na ujumbe huu, tuma neno CHADEMA kwenda namba 15710 kwa wateja wa Zain na Vodacom pekee kwa sasa; aidha kwa maoni au ushauri niandikie kupitia mnyika@chadema.or.tz; ruksa kwa waandishi kunukuu sehemu za taarifa hii kwenye habari zao za kesho na ruksa wa wahariri kuchukua taarifa hii na kuitoa yote au maudhui yake kwenye makala siku yoyote ili ujumbe ufike kwa watanzania wengi zaidi mjadala uendelee mpaka tupate msimamo wa pamoja.

Kwa wanahabari, nawaombeni muendelee kuzingatia maadili ya taaluma yenu kufikisha ujumbe huu kwa umma bila ya hofu wala upendeleo (Without favour or fear) kwa maslahi ya Taifa letu. Kwa magazeti nawapongeza Dar Leo, Majira, Tanzania Daima, The Citizen Nk kuandika habari hii baaada ya mkutano wangu na waandishi wa habari pamoja na mbinu nyingi za serikali na maswahiba wake kujaribu kuzuia habari husika. Kwa redio nawapongeza Clouds FM, VOA kupitia Radio Free Africa na East African Radio kwa kuendeleza majadiliano kuhusu taarifa hii. Kwa Kibonde, bado kipindi cha Jahazi mnastahili kutoa ufanuzi mzuri zaidi kwa watanzania, mfano wasikilizaji wenu wamenieleza kuwa mmebeza kuwa Membe hawezi kumjibu Mnyika kwa kuwa ni sawa na Lipuli na Manchester United, lakini kumbukeni kwamba mpira unadunda dakika tisini; hivyo matokeo yatabikiriki. Nirudi kwenye hoja yenu niliyoambiwa mmepotosha kwamba ufisadi wa watu binafsi isihusishwe serikali; tafadhali wapeni ufafanuzi sahihi wasilikilizaji wenu ambao wengi wao ni vijana wenzangu; kwamba huwezi kutenganisha tuhuma zinazohusu viongozi wa serikali na taasisi zake na serikali yenyewe. Jadilini masuala husika kama nilivyoyachambua kwa kirefu katika taarifa hii. Kwa TV, sina ya kupongeza mpaka sasa; kuwa pamoja na baadhi yao kuwepo kwenye mkutano na waandishi wa habari hakuna aliyediriki kutoa hoja mbadala; wakati wote taarifa ambazo zimeendelea kutolewa ni za kipropaganda za serikali na taasisi zake. Nisamehewe kama kuna makosa ya uchapati, nimeitoa taarifa hii tukiwa katikati ya kikao cha Kamati kuu ya CHADEMA ambacho kimekaa hivi sasa kujadili pamoja na mambo mengine Hali ya Kisiasa ikiwemo kashfa hii kwa Taifa.





2 comments:

Anonymous said...

Childish and giberish. Kama Mnyika ndiye Waziri wa Mambo ya Kimataifa wa CHADEMA, basi chama kimefilisika. Aliyoandika hapo hayaeleweki wapi yanaanzia na kuishia. Halafu yaliyoandikwa yameandikwa kitoto kama mwanafunzi wa sekondari. Ni vema kwa msomaji kujisomea mwenyewe ripoti ya UN na kujiamualia mwenyewe juu ya yaliyoandikwa kuliko kusoma huu utumbo na propaganda.

Anonymous said...

Mi mbona nimesoma nimeona kuna hoja humo? au kwa sababu amehusisha na Meremeta ndio inakuwa ngumu kueleweka?