Tuesday, December 15, 2009

Miaka 48 ya Uhuru: Tusake mabadiliko ya kweli tupate uhuru wa kweli-2

Katika makala yangu iliyotangulia nilieleza kwamba kumbukumbu ya miaka ni wakati wa kutafakari taifa letu lilipotoka, lilipo na tunapotaka liende. Takafakari hii haipaswi kufanyika tarehe 9 Disemba pekee bali ni mchakato unaopaswa kuendelezwa na mtanzania yoyote mwenye kuamini kwamba uhuru wa kweli, si uhuru wa bendera bali ni uhuru dhidi ya umasikini, ujinga, maradhi na ufisadi. Uhuru wa kweli, ni uhuru wenye kuleta maendeleo kisiasa, kijamii na kiuchumi. Katika makala hiyo iliyotangulia niliitathmini hali ya kiuchumi miaka 48 baada ya uhuru na kuhimitimisha kwamba; uhuru wa kiuchumi katika taifa letu utapatikana kupitia mabadiliko ya kweli, yenye kuhimili misukosuko ya ukoloni mamboleo; na kujenga taifa lenye kutumia vizuri rasilimali katika kutoa fursa kwa raia wake. Leo tutafakari sekta nyingine.

Nchi hii imewekwa rehani kijamii; ndoto ya waasisi wa taifa hili la kujenga taifa lenye uhuru na umoja inafifia. Viongozi wa CCM wanatembea kifua mbele wakizusha mijadala ya ukabila na udini yenye kuligawa taifa. Umoja kati yao umetoweka na sasa wanaparuana wao kwa wao. Chini ya sera mbovu za CCM matabaka yanazidi kumea katika taifa, pengo kati ya masikini na matajiri linazidi kukua kila kukicha. Umasikini unazidi kuongezeka. Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kwamba kati ya mwaka 2005 Rais Kikwete na CCM walioahidi maisha bora kwa kila mtanzania mpaka sasa; katika kila watanzania kumi; saba wamesema kwamba hali yao ya maisha haijawa bora. Na kati yao; asilimia hamsini hali yao imekuwa mbaya zaidi. Nyufa hizi ni tishio kwa amani ya nchi yetu.

Miaka 48 baada ya uhuru, huduma za kijamii zinazidi kudorora; kwa kiwango cha huduma hizo na hata upatikanaji hususani kwa watanzania masikini. Elimu ni sehemu ya uhuru wa kweli kwa vijana; kwa Tanzania ya leo mfumo mzima wa elimu ujenga matabaka. Ukiwa mkoani Dar es salaam na kutembelea shule mbalimbali kuanzia chekechea mpaka sekondari; baina ya shule binafsi na za umma, utofauti wa mazingira ya kusomea ni wa kiwango cha juu. Pamoja na kuongezeka kwa idadi ya madarasa katika shule za umma, bado kuna tatizo la ubora wa madarasa yenyewe yaliyojengwa kwa ukilinganisha na kiwango cha fedha za michango ya wananchi zilizotumika. Kijana wa mtazanzania wa kawaida anasoma katika shule yenye kiwango duni cha elimu kutokana na uhaba wa walimu na vifaa vya kufundishia. Ishara ya kuporomoka huko kwa elimu, ni wimbi la viongozi wa serikali hiyo hiyo inayosimamia kususa kusomesha watoto wao katika shule za umma. Tunahitaji sera na uongozi mbadala; huu ni wakati wetu, tusidanganyike.

Vijana wa vyuo vikuu ni wajibu wao kuwa mstari mbele kusaka mabadiliko; kwani ni mashuhuda wa namna ambavyo serikali inavyofanya matumizi ya anasa, fedha za umma zikipotea kwa ufisadi. Hatima ya yote mzigo unarudi kwa mwanafunzi na wazazi wake kupitia sera za uchangiaji ambao wengine imewanyima fursa ya kusoma.


Miaka 48 baada ya uhuru vijana wanapoteza maisha yao kwa wingi kwa magonjwa yanayoweza kutibika kama malaria na hata kipindupindu. Pamoja na sera ya uchangiaji kuwa mzigo wa watanzania walio wengi bado vifaa na madawa havipatikani hususani katika hospitali na zahanati za umma. Vijana wa kike wajawazito, ambao kila mara matukio ya vifo vya watoto wao kutokana ubovu wa huduma za afya wanaweza kutoa vizuri zaidi kilio hiki. Chini ya utawala wa sasa huduma za jamii kwa ujumla zimegeuzwa bidhaa badala ya kuwa huduma; ikiwemo huduma kama elimu, afya, maji nk. Ni wakati wetu; tusidanganyike. Tuunganishe nguvu mabadiliko ya kisera na kiuongozi yatayowezesha huduma za kijamii kuwa bora na kuwafikia watanzania walio wengi. CHADEMA ni chama cha mrengo wa kati; tunaamini kwamba hata katika mfumo wa soko ni lazima kwa taifa kuwa na mifumo ya ulinzi wa kijamii (social security) inayogusa makundi mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii.

Miaka 48 baada ya uhuru, ahadi za serikali ya CCM kwa makundi maalum mathalani wanawake, wazee, vijana na wenye ulemavu zimekuwa ni maneno matupu bila vitendo. Sera zao zinatutazama kama watu tunaohitaji kusaidiwa badala ya kuwa wadau wa msingi wa kimaendeleo. Ni wakati wetu; tusidanganyike. Chini ya uongozi mbadala, badala ya wazee wetu kuonekana kuwa kundi linalopaswa tu kubebwa na kuhudumiwa, sera mbadala zitaboresha kiwango na mifumo ya malipo ya wastaafu na kupanua wigo wa mifuko ya kijamii kujumuisha ajira ambazo haziko kwenye mkondo uliozoeleka.

Uboreshaji wa mifumo ya wastaafu itawezesha wazee wetu kuwa na fursa ya kupata huduma za msingi na kuwa na kipato stahili cha kuwakimu hata baada ya kumaliza utumishi wao kwa taifa. Laana ya wazee wastaafu wanaotangatanga na kulazimika kudai haki zao kwa nchi zenye kuwatezwa zinapaswa kuwa chachu ya kufanya mabadiliko.

Pamoja na CCM chini ya Rais Kikwete kujigamba kuweka mstari wa mbele wanawake, sifa hizo zipo kwenye vyombo vya kitaifa vya uteuzi tu. Ni wakati wetu; tusidanganyike. Tunahitaji uongozi na sera mbadala kubadili mifumo ya kisiasa na mitazamo ya kijamii kuweza kujenga taifa lenye kutoa fursa kwa makundi yote ya kijamii kuweza kushindana na kushinda.

Ni muhimu nikakumbusha kuwa athari kubwa zaidi ya kiuchumi ambayo inataathira pia kwa hali ya kijamii ni utegemezi ambao taifa letu limeingizwa kwa kutegemea misaada kutoka nje huku rasilimali za taifa zikifyozwa kibeberu. Ni ukoloni huu mpya ndio ambao unanifanya nitamke kwamba tunahitaji kudai uhuru wa Tanzania. Tunahitaji uhuru wa kweli. Wakati wetu ni huu, tusidanganyike. Mwanafalsafa Frantz Fanon, aliwahi kusema kwamba kila kizazi lazima, nje ya uvungu uvungu kiutambue utume wake; ama kiutumize au kiusaliti. Kizazi cha wakati huo, kilidai uhuru, na kujenga misingi ya taifa(national building) ingawa misingi hiyo imekuja kuvurugwa na kuturudisha kwenye ukoloni mambo leo(neo colonialism). Ni wajibu wa kizazi chetu; kudai uhuru wa kweli, uhuru dhidi ya umasikini, ujinga, maradhi; hatuwezi kudai uhuru huo bila kumpiga vita adui ufisadi. Wajibu wa kizazi chetu ni kuweza kupambana katika mazingira ya ushindani wa ndani na nje ya nchi yetu; kujenga taifa tukitazama kizazi chetu na kijacho.

Pigo kubwa kwa mwelekeo wa taifa letu, na utumwa wa kiutamaduni unaoendelea kumea. Vijana wanaweza kubebeshwa mzigo wa lawama wa kuiga tamaduni za kigeni kwa kiwango chenye kupoteza utaifa wetu; ukweli ni kuwa chanzo cha yote haya ni uongozi usio na maono. Unapokuwa na uongozi wenye sera ambazo hata vyombo vya habari vya umma vinakuwa ni vioo vya tamaduni za nchi zingine; usitegemee vijana kubeba urithi wa nchi yao. Viongozi wetu wanapaswa kujifunza, nchi zilizofanya mapinduzi ya kiuchumi; muhimili thabiti wa mwelekeo wao ni tamaduni zao. Kinyume chake, nchi zenye viongozi wabinafsi; viongozi wasiojiamini, viongozi wasiowajibika, ni matokeo ya utamaduni wa ufisadi. Ni wakati wetu, tusidanganyike. Tunapoazimisha miaka 48 ya uhuru, tuhamasishe mabadiliko ya kweli; kwa kuweka mkazo katika kujikwamua kifikra; kuanzia katika desturi zetu; fasihi zetu; muziki wetu; michezo yetu; familia zetu: vyote vituelekeze katika kujenga taifa lenye kukumbuka tulipotoka na kutengeneza mweleko mwafaka wa vizazi vijavyo. Maneno ya Wimbo wa Bob Marley (Redemption Song) ya mwito wa kujikwamua kutoka utumwa wa kiakili yanafumbo linaloposwa kufumbuliwa katika kutafuta mabadiliko kupata uhuru wa kweli.

Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje(CHADEMA) anayepatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.or.tz na http://mnyika.blogspot.com/

No comments: