Wednesday, December 30, 2009

UN na usalama wa raia toeni taarifa

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


UN ITOE TAMKO RASMI KUHUSU KIKAO CHA BARAZA LA USALAMA KILICHOJADILI TAARIFA YA TIMU YA WATAALAM JUU YA USAFIRISHAJI WA SILAHA NA UTOROSHAJI WA DHAHABU HARAMU DRC

Wizara ya Usalama wa Raia watoe kauli kuhusu hatua zilizofikiwa katika kumchunguza Bande Ndagundi na wengine wanaotajwa kwenye mtandao wa biashara ya silaha wanaoishi Tanzania

Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa (CHADEMA) inauomba Umoja wa Mataifa (UN) kutoa tamko rasmi kuhusu matokeo ya kikao cha Baraza la Usalama la UN kilichojadili hivi karibuni taarifa ya Timu ya Wataalamu iliyoundwa na umoja huo kufuatilia utekelezaji wa maazio ya UN kuhusu vita DRC ikiwemo usafirishaji wa silaha na utoroshaji wa dhahabu katika maeneo husika.

Haja ya kutaka tamko rasmi toka UN inatokana na taarifa zinazoendelea kusambaa kwa njia ya mtandao zinazoonyesha kwamba tayari vikao rasmi vya UN vimeshaijadili taarifa hiyo. Baadhi ya taarifa hizo ni pamoja na Ripoti Maalumu(Special Report) ya jarida la kimataifa la Africa Confidential ya hivi karibuni(inayopatikana kupitia
www.africa-confidential.com) taarifa hizo zinaonyesha kwamba Baraza la Usalama limekaa Novemba 20; Novemba 25 na mwezi Disemba kupitia taarifa husika.

Ni muhimu kwa Umoja wa Mataifa kutoa tamko hivi sasa kwa kuwa mwanzoni mwa mwezi Disemba UN kupitia ofisi yake ya Tanzania ulieleza kwamba taarifa ya timu ya wataalamu haikuwa rasmi mpaka baada ya kujadiliwa na vikao hivyo; sasa kama tayari vikao hivyo vimeshakaa kama inavyodokezwa katika vyanzo hivyo vya kimataifa ni wakati wa umoja wa mataifa kutoa tamko rasmi kuhusu maudhui ya ripoti yake rasmi.

Pia kwa kuwa serikali ya Tanzania ilitoa kauli kupitia Balozi wetu wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, Dr Augustine Mahiga kwamba ingewasilisha taarifa ya ufafanuzi wake kuhusu tuhuma zilizomo kwenye ripoti hiyo zinazoitaja taasisi za Tanzania na baadhi ya watanzania; ni wakati muafaka wa ripoti hiyo ya Serikali ya Tanzania kama imeshawasilishwa nayo kuwekwa hadharani na Wizara ya Mambo ya Nje au UN.

UN izingatie kuwa mpaka sasa Wizara ya Mambo ya Nje haijawasiliana rasmi na wawakilishi wa wananchi(wabunge), vyama vya siasa na wadau wengine wa msingi kupata maoni yao kuhusu tuhuma zilizomo kwenye ripoti husika ili kutoa msimamo wa pamoja hivyo ni muhimu kwa milango ya majadiliano kuhusu suala hili kuendelea kufunguliwa.

Tunapenda pia kuukumbusha Umoja wa Mataifa(UN) kuwa hali hii ya Serikali ya CCM kutoshirikisha vyama vingine na wadau wengine katika maamuzi ya msingi yanayohusu taifa inachangiwa hodhi (monopoly) ya chama kimoja bungeni; na hivyo kupunguza uwezo wa kambi ya upinzani kuiwajibisha serikali kikamilifu.

Hivyo, wakati tunatafakari ripoti ya Kikundi cha Wataalamu kilichoundwa UN; ni wasaa pia wa UN Tanzania kupitia UNDP kuongeza kasi ya kuisimamia serikali kutekeleza marekebisho ya kisheria na kitaasisi ya kuwezesha uchaguzi wa 2010 kuwa huru na haki. Hii ni kupitia programu yake ya kusimika demokrasia (deepening democracy program) na kusimamia vizuri mfuko wa uchaguzi wa mwaka 2010 (UN Basket Fund for Elections).

Wakati huo huo: Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa(CHADEMA) inaitaka Wizara ya Usalama wa Raia kauli kuhusu hatua zilizofikiwa katika kumchunguza Bande Ndagundi na wengine wanaotajwa kwenye mtandao wa biashara ya silaha wanaoishi Tanzania.

Itakumbukwa kwamba mwanzoni mwa mwezi Disemba Jeshi la Polisi kupitia kwa Mkuu wa Jeshi hilo(IGP) na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) walitoa kauli kwamba jeshi hilo limeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu wote waliotuhumiwa kwenye ripoti hiyo.

Mwezi unaelekea kumalizika bila taarifa kutolewa kuhusu kuendelea kwa uchunguzi huo; pamoja na kuwa masuala ya uchunguzi mengine ni ya siri, lakini hatua za mchakato wa uchunguzi ni jambo la kawaida kuelezwa ili kujenga imani kwa umma na wadau wote kwamba serikali imezipa uzito unaostahili tuhuma hizi kwa lengo la kusafisha taswira ya taifa letu kwa wananchi wake na jamii ya kimataifa kwa ujumla.

Ikumbukwe kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likitoa taarifa kuwa linafanya uchunguzi wa kina lakini baada ya hapo uchunguzi unaishia hewani ama matokeo yake hayawekwi hadharani. Mathalani mpaka sasa Jeshi la Polisi halijaeleza hatua zilizochukuliwa katika sakata ya Dr Wilbroad Slaa(Mb) kuwekewa vinasa sauti chumbani kwake; tuhuma za kushambuliwa kiharahamia viongozi wa CHADEMA zinazohusisha viongozi wa CCM katika chaguzi ndogo za Kiteto, Busanda na Biharamulo; nk.


Imetolewa tarehe 30 Disemba 2009 na:




John Mnyika
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje
mnyika@chadema.or.tz
0754694553

No comments: