Saturday, December 19, 2009

Taarifa kwa Umma: Serikali itoe tamko hatua iliyofikiwa

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA YA KURUGENZI YA MAMBO YA NJE YA CHADEMA KWA SERIKALI NA WATANZANIA KUHUSU RIPOTI YA KUNDI LA WATAALAMU WA UMOJA WA MATAIFA YATOLEWA

• CHADEMA tunahimiza watanzania kuipitia ripoti ya UN ambayo imetafsiriwa na kuchambuliwa katika lugha ya kiswahili.
• “Tuchafuke tusafishe tujisafishe: kujadili ni uzalendo wa kutetea maslahi ya taifa”-Mkurugenzi wa Mambo ya Nje (CHADEMA), John Mnyika
• Waziri Mwinyi atoe tamko la kujibu Tuhuma toka ripoti ya Kundi la Wataalamu wa UN zizazohusu Ulinzi na Jeshi


Taarifa inatolewa kwa umma kupitia vyombo vya habari kuhamasisha umma kupitia taarifa ya awali iliyotafsiriwa katika lugha ya Kiswahili kuhusu Ripoti ya UN inayopatikana kupitia www.chadema.or.tz ili kuendeleza mjadala wa umma kuhusu ripoti husika.

Aidha kupitia Kurugenzi ya Mambo ya Nje inatoa mwito kwa Serikali kuweza kutoa tamko kuhusu hatua zilizofikiwa za maandalizi ya taarifa ya Serikali kuhusu ripoti ya UN. Hii ni kwa sababu siku chache zimebakia kwa serikali kuwasilisha ripoti yake kwa Umoja wa Mataifa huku mpaka sasa serikali haijawasiliana na wananchi ama walau wawakilishi wa wananchi kupata maoni yao ili kujenga msimamo wa pamoja kama taifa kuhusu yaliyoibuliwa na ripoti husika.

Tunatoa mwito pia kwa Umoja wa Mataifa (UN) nao ukayatafakari masuala yaliyomo kwenye taarifa yetu ya awali wakati inapojiandaa kuipitia Taarifa ya Serikali ya Tanzania kuhusu Ripoti husika ambayo serikali kupitia kwa Balozi wake wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa (Dr Mahiga) imetangaza kwamba itawasilisha mwezi huu wa Disemba mwaka 2009. Watanzania na Umoja wa Mataifa(UN) wazingatie kuwa maoni hayo ya Serikali inayoongozwa na CCM si msimamo wa Watanzania wote kwa kuwa si wananchi, wala vyama vyao, wala wawakilishi wao(kwa maana ya wabunge wa kambi zote) wamehusishwa katika kuandaa ripoti husika. Hivyo, Watanzania na hata Umoja wa Mataifa, unapaswa kuzingatia kuwa mjadala kuhusu ripoti hii unapaswa kuendelea ili Taifa la Tanzania lipate msimamo wa pamoja kuhusiana na ripoti husika; ili wawakilishi wetu kwenye UN wakazungumze matakwa ya watanzania badala la maoni yao binafsi ama ya serikali inayoongozwa na chama kimoja ndani ya mfumo wa vyama vingi. Ni muhimu nikarudia pia kutoa rai niliyoitoa awali kwamba ripoti ya Kikundi cha wataalamu kilichoundwa na UN ipaswa pia kujadiliwa muktadha wa Orodha ya Mafisadi (list of shame) iliyotolewa na CHADEMA.

Aidha ikumbukwe kuwa tunakubaliana na hoja kwamba Serikali ya Tanzania imechafuliwa katika Ripoti hiyo ya UN kwa baadhi ya viongozi wake, ama raia wake kutajwa kwa namna moja au nyingine katika ripoti hiyo; aidha serikali yenyewe kama taasisi imechafuliwa kwa kuonyeshwa kwamba haitekelezi kikamilifu maazimio ya Umoja wa Mataifa (UN) ambayo serikali yetu ni mwanachama. Lakini nchi ya Tanzania kama taifa, na watu wake wote kwa ujumla wake; hawajachafuliwa. Kama Nchi ya Tanzania, na wananchi wake wote wakatoa kauli ya pamoja ya kuwatetea watu wachache ndani na nje ya serikali waliotajwa katika kashfa hii; hapo ndipo tutakapochafuka wote kwa ujumla wake. Lakini kama Nchi yetu, na watu wake; tukakubaliana kuchukua hatua ya kusafisha uchafu unaoichafua sisi na taifa letu; ni wazi tutasafishika na heshima ya taifa letu itaendelea kulindwa na kujilinda kote duniani.

Kwa kutumia lugha ya picha; ni kama vile nchi yetu ni mtaro; sasa mtaro unaweza kuwa na uchafu, ukipiga kelele kwamba hakuna uchafu wakati uchafu unaonekana basi utaonekana una utamaduni wa uchafu ndio maana unaona ni jambo la kawaida kuwa kwenye mazingira ya uchafu; wewe ni mchafu. Lakini ukichukua hatua ya kuingia ndani ya mtaro, na zana zako za kusafishia; utachafuka kidogo, utaweza kusafisha mtaro, utatoka na utajisafisha. Mtaro utabaki safi, na wewe utabaki safi; na wewe na mtaro wako wote mtakuwa safi na kuitwa wasafi.

Kadhilika kwa Tanzania, mjadala huu kuhusu uchafu iliotolewa na ripoti ya UN unapaswa kuendelea ili tuujue vizuri uchafu wenyewe wakati wa mjadala huu tutaonekana kuwa tuna uchafu lakini tutaweza kuingia tukachafuka kidogo tukausafisha na nchi yetu itabaki ikiwa safi na sisi wenyewe tutathibitika mbele ya jamii ya kimataifa kuwa ni wasafi na hatupendi uchafu na unapojitokeza tunachukua hatua za kuuondoa.
Hivyo, tunatoa taarifa hii kwa tahadhari kubwa ya kizalendo kwa kuwa najua suala hili linagusa kwa namna au nyingine vyombo vyeti na masuala tete yanayoelekezwa kwa nchi yetu yanayogusa jeshi, polisi, usalama wa taifa, chama tawala, serikali yake, na viongozi wake. Mambo tunayoyaandika yanagusa genge la mafisadi na watumiaji vibaya wa madaraka; wengine wakiwa ni wafanyabiashara, wengine wakiwa ni viongozi, wengine wakiwa ni wahalifu waliokubuhu na waasi wenye kufanya mauaji.

Katika mukatadha huo, ni muhimu kwa wananchi kuendelea kupuuza kauli za wenye kueneza uchochezi kwamba CHADEMA iache siasa zenye kuichafua Tanzania; eti itangulize ‘uzalendo’. Wananchi wajiulize ni nani anaichafua Tanzania; kati ya waliofanya ufisadi na/ama kutumia madaraka vibaya na kuitumbukiza Tanzania katika kashfa kama hizi za usafirishaji wa silaha na utoroshaji wa madini kutoka maeneo yenye vita vya wenyewe kwa wenyewe au mtu anayetaka mjadala kuhusu suala hili ili utoke msimamo wa pamoja wa wazalendo wote wenye kukerwa na mambo hayo ili kulirudisha taifa kwenye mkondo unaostahili wenye kulinda heshima ya Tanzania kitaifa na kimataifa?

Hawa wangetaka kutanguliza maslahi ya pamoja ya Tanzania wasingekurupuka kutoa kauli ya serikali ya CCM bila kushirikisha umma wa watanzania ama wawakilishi wa wananchi. Viongozi wa serikali hawana haki ya kusema kwa niaba ya watanzania katika masuala tata bila kupata maoni yetu au ya kambi yetu bungeni. Wananchi tuwaambie wazi watu kama hao kwamba; kila wanachokisema ni msimamo wao na serikali ya chama chao au taasisi zao; hakiwakilishi msimamo wa watanzania wote.

Waambie wazi kuwa kama wanataka watanzania tusivuane nguo hadharani; walio kwenye mamlaka ; kabla ya kutoa kauli, walau waombe maoni ya wawakilishi wa wananchi au taasisi zinazowakilisha wananchi; diplomasia iliyokomaa inatambua umuhimu wa maridhiano baina ya viongozi kabla ya kutoka hadharani katika masuala tete ya kitaifa. Tuko tayari kwa majadiliano kama watanzania kuhusu suala hili ili tutoke na msimamo wa pamoja kama taifa. Kuhoji uzalendo wa wanaotaka watanzania waliotajwa kwenye ripoti ya Kikundi cha Wataalamu kilichoundwa na UN ni sawa na kuwatetea mafisadi ama waliotumia vibaya madaraka yao waliotuhumiwa kwenye ripoti husika.

Ikumbukwe kuwa tuhuma za Tanzania kujihusisha na vita vya DRC zilianza toka wakati taifa hili linaasisiwa. Tofauti ya watawala wa sasa ni kwamba uongozi wa Nyerere ulikuwa unasema wazi kuwa unasaidia waasi, na UN inajua. Lakini wakati ule walioitwa waasi ni wazalendo waliokuwa wakipambana dhidi ya watawala wa kidikteta ambao walikuwa ni makuwadi wa ubeberu na ukoloni mamboeleo katika Afrika. Sera ya wakati huo ya mambo ya nje ya Tanzania ilikuwa ni kuleta ukombozi Afrika nzima (hata ikiwa ni kwa kuunga mkono vita vya msituni) na kueneza umajumuhi wa kiafrika (Pan Africanism).

Serikali ya sasa ipo tofauti; kwanza haina msimamo endelevu; pili, sera yake ya mambo ya nje haieleweki; tatu, masuala ya sasa ya usafirishaji wa silaha ama utoroshaji wa madini toka maeneo yenye vita ambao yanasemwa kuwa yanafanywa na serikali ama watanzania yanahusu zaidi miradi binafsi ya watu ambayo wanaindesha kwa ama kuzitumia taasisi za kiserikali au kuruhusu mianya kwa kutowajibika kusimamia utawala wa sheria ikiwemo kuheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa (UN) ambayo nchi yetu imetia saini.

Hivyo wapenda demokrasia na maendeleo ndani na nje ya Tanzania wanapaswa kuunga mkono rai tuliyoitoa Disemba Mosi, 2009: Kwamba wazalendo wote, waliokerwa na Tanzania ‘kuchafuliwa’ na ripoti hiyo ya Kikundi cha Wataalamu wa UN, wanapaswa kuwashinikiza watanzania wote wanaoishi Dar es salaam, Kigoma na kote duniani ambao wametajwa kwenye taarifa hiyo kwa majina yao; wajitokeze kutoa kauli za kusafisha majina yao, tukiridhika na hoja zao, katika utetezi wao; basi na sisi tutajiunga katika kundi la kuwatetea na kuwasafisha. Viongozi na taasisi za serikali zilizotajwa kwa namna moja au nyingine katika taarifa hiyo iwe kwa majina au kwa matukio zijitokeze kuelezea kutajwa kwao; tukiridhika na maelezo yao na vielezo vyao, tutajiunga katika kazi ya kizalendo ya kuwatetea na kuwasafisha. Na hii isiwe kwa taarifa ya UN pekee; iwe pia Orodha ya Mafisadi, katika vipengele vinavyohusiana na Kampuni za Meremeta, Tangold, Deep Green nk.

Kosa kubwa la Wizara ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa katika sakata hili ni kufikiri kwamba yenyewe tu ndiyo inayowajibika kulitolea ufafanuzi na taarifa kuhusu tuhuma zilizoibuliwa na Kundi la wataalamu lililoundwa na UN. Narudia tena kumuomba Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwashinikiza Mawaziri wengine ambao sekta zao zimeguswa kutoa kauli za kujibu ama kufafanua hoja zilizoibuliwa ndani ya ripoti hiyo, ambayo tayari Wizara ya Mambo ya Nje ameshafanya kosa la kisiasa la kuitumbukiza serikali kwenye malumbano mapema kwa kuliibua suala hili na kuituhumu UN kabla hata Tanzania kufafanua ama kujieleza kwenye Kamati ya Vikwazo. Kwa kuanzia ni muhimu kwa Wizara ya Mambo ya Usalama wa Raia na ile ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa zikatoa maelezo na vielelezo kuhusu suala hili. Hivyo, mawaziri wanaopaswa kufutia kutoa kauli ni: Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Hussein Mwinyi na Waziri wa Usalama wa Raia; Lawrence Masha.


Ikumbukwe kuwa Wizara ya Ulinzi ilishatoa kauli fupi ya kukanusha tu kwa ujumla bila kujibu hoja kwa hoja. Hatahivyo, pamoja na kuwa natambua kwamba ni muhimu kwa Jeshi letu, kutunza siri za mikakati yetu ya kijeshi. Wizara ya Ulinzi na Jeshi La Kujenga Taifa ina wajibu wa kutoa kauli za ufafanuzi; na awasilishe maelezo na vielelezo ili serikali ipeleke UN yenye kujibu maswali yafuatayo: Je, kwa kuwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania Burundi ambaye alikuwa ni mmoja wa majenerali wa jeshi, namba yake ya simu imetajwa kutumika kuwasiliana na waasi; JWTZ haina sera ya kuendelea kuwatumia maafisa wake waandamizi wa jeshi wanaoitwa wastaafu, wanaotumwa kwenye nchi zenye vita kama ilivyo DRC kuweza kufanya kwa barokoa ya ubalozi majukumu yanayoyofanana na uambata wa kijeshi? (Millitary attacheship). Kama hivyo ndivyo, wizara inaweza kutuambia ni mawasiliano gani ya kijeshi yalikuwa yakifanyika baina ya namba ya simu ya balozi wetu na makamanda wa vikundi vya waasi DRC hususani FDLR na maswahiba wao ndani FARDC? Kwa kuwa mabalozi wetu kuwasiliana na vikundi vya waasi katika nchi ambazo serikali yetu inatambua serikali zake za kiraia ni jambo lisilokubalika na halina uhusiano wowote na ‘siri kuu za jeshi’ wala ‘maslahi ya taifa’; kwanini nini serikali isituleze mawasiliano yaliyokuwa yakiendelea kama inavyotuhimiwa kwenye ripoti ya kundi la Wataalamu lililoundwa na UN? ( Ni muhimu kwa Waziri Mwinyi kutoa tamko hivi sasa kwa kuwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania Burundi ameshaondoka katika Ubalozi husika na hana tena kinga kamili ya Kibalozi. Je uamuzi wa Rais Kikwete kuteua Balozi Mpya wa Tanzania Burundi hivi karibuni unauhusiano wowote na kutajwa kwa jina la balozi wa Zamani katika ripoti ya UN?).

Kwa kuwa silaha za kivita ni kubwa, sio ndogo kama sindano kiasi kwamba zinaweza kupita bila kuonekana; Wizara ya ulinzi inazielezeaje tuhuma ya silaha kupitishwa Tanzania ambazo zimeelezwa na Kundi la Wataalamu wa UN kwa maelezo na vielelezo? Wizara inaweza kulieleza taifa silaha hizo zimekwenda nchi gani na kwa makubaliano gani ya kijeshi? Mwisho, kwa kuwa Kamati ya Vikwazo ya UN kuhusu DRC iliundwa toka mwaka 2004; pamoja na kuwa ripoti ya Kundi la Wataalamu wa UN imegusia zaidi miaka ya 2007 mpaka 2009; Wizara inazizungumziaje taarifa zilizozagaa katika mitandao mbalimbali zinazohusisha Meremeta, Tangold; Deep Green na makampuni mengine yaliyosajiliwa kwa majina ya vigogo wa serikali ya awamu ya tatu ambayo yanatajwa kuhusika na biashara haramu za silaha na utoroshaji wa madini toka maeneo yenye vita; kampuni ambazo mojawapo serikali imesema kwamba inahusika na JWTZ? Izingatiwe kuwa CHADEMA ilishaweka msingi wa taarifa hizo kwenye orodha ya mafisadi iliyotolewa 15 Septemba 2009.


Masuala haya na mengine mengi zaidi nikayoyachambua kadiri siku zinavyokwenda yanapaswa kujadiliwa na wananchi ama wawakilishi wao; ili tuweze kutoka na msimamo wa pamoja. Pia UN na Kundi la Wataalamu wake kuiuliza serikali itoe maelezo ya kina wakati wa mapitio ya taarifa husika. Ni utaratibu wa kawaida kwamba ufuatiliaji kama huu uliofanywa kwa kuwa ulihusu Tanzania; serikali itapewa fursa kuandika ripoti ya nchi (country report) kufafanua mambo ambayo yametajwa kabla ya kamati ya vikwazo kufanya maamuzi yake ama kuikubali ripoti husika na mapendekezo yake ama kutoa maelekezo mbadala ya kutaka uchunguzi zaidi katika maeneo ambayo Kundi la Wataalamu limeeleza katika ripoti yake kuwa uchunguzi wake bado haujamilika. Inashangaza kwamba serikali inatumia nguvu kubwa, kubeza ripoti hii na kutishia wanahabari wasiendelee kuandika wakati ripoti imeweka bayana kwamba uchunguzi bado haujakamilika; serikali itaweka wapi uso wake kama uchunguzi zaidi ukaibua uchafu zaidi? “Tuchafuke tusafishe tujisafishe: kujadili ni uzalendo wa kutetea maslahi ya taifa”


Imetolewa leo tarehe 20 Disemba, 2009 Mkoani Tanga; Tanzania:
John Mnyika
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa
0754694553No comments: