Monday, December 7, 2009

Ripoti ya Kundi la UN: Tuchafuke tusafishe tujisafishe-kujadili ni uzalendo wa kutetea maslahi ya taifa

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA AWALI YA KURUGENZI YA MAMBO YA NJE YA CHADEMA KWA SERIKALI NA WATANZANIA KUHUSU RIPOTI YA KUNDI LA WATAALAMU WA UMOJA WA MATAIFA YATOLEWA

CHADEMA yatimiza ahadi ya kuitafsiri ripoti na kuichambua katika lugha ya Kiswahili.
“Tuchafuke tusafishe tujisafishe: kujadili ni uzalendo wa kutetea maslahi ya taifa”-Mkurugenzi wa Mambo ya Nje (CHADEMA), John Mnyika
Tunamtaka Waziri Masha ajibu tuhuma toka ripoti ya Kundi la Wataalamu wa UN zizazohusu Usalama wa Raia kama sehemu ya utetezi ambao Tanzania itawasilisha UN kuanzia leo

Leo tarehe 7 Disemba 2009 tunatoa rasmi kwa umma kupitia mtandao wa www.chadema.or.tz taarifa ya awali ya kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA kwa serikali na watanzania kuhusu ripoti ya kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN). Tunatoa taarifa hii ikiwa ni sehemu ya kutekeleza ahadi yetu tuliyoitoa Disemba Mosi, 2009 wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari ya kuitafsiri taarifa ya UN kwa lugha ya Kiswahili na kuitoa hatua kwa hatua sambamba na maoni yetu ili watanzania waweze kuijadili kikamilifu na hatimaye tuweze kutoka na msimamo mmoja kama taifa kuhusu ripiti hiyo.

Napenda kuwasilisha kwa umma tafsiri ya kwanza na uchambuzi wa awali wa maudhui ya ripoti hiyo ya Kundi la Wataalamu wa UN kwa ajili ya kusambazwa, kusomwa na kutafakariwa na serikali na watanzania kwa ujumla. Aidha ni muhimu Umoja wa Mataifa (UN) nao ukayatafakari masuala haya wakati inayapitia Moani ya Serikali ya Tanzania kuhusu Ripoti husika ambayo serikali kupitia kwa Balozi wake wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa (Dr Mahiga) imetangaza kuwa itayawasilisha leo tarehe 7 Disemba 2009. Watanzania na Umoja wa Mataifa(UN) wazingatie kuwa maoni hayo ya Serikali inayoongozwa na CCM si msimamo wa Watanzania wote kwa kuwa si wananchi, wala vyama vyao, wala wawakilishi wao(kwa maana ya wabunge wa kambi zote) wamehusishwa katika kuandaa ripoti husika. Hivyo, Watanzania na hata Umoja wa Mataifa, unapaswa kuzingatia kuwa mjadala kuhusu ripoti hii unapaswa kuendelea ili Taifa la Tanzania lipate msimamo wa pamoja kuhusiana na ripoti husika; ili wawakilishi wetu kwenye UN wakazungumze matakwa ya watanzania badala la maoni yao binafsi ama ya serikali inayoongozwa na chama kimoja ndani ya mfumo wa vyama vingi. Ni muhimu nikarudia pia kutoa rai niliyoitoa awali kwamba ripoti ya Kikundi cha wataalamu kilichoundwa na UN ipaswa pia kujadiliwa muktadha wa Orodha ya Mafisadi (list of shame) iliyotolewa na CHADEMA.

Nakubaliana na hoja kwamba Serikali ya Tanzania imechafuliwa katika Ripoti hiyo ya UN kwa baadhi ya viongozi wake, ama raia wake kutajwa kwa namna moja au nyingine katika ripoti hiyo; aidha serikali yenyewe kama taasisi imechafuliwa kwa kuonyeshwa kwamba haitekelezi kikamilifu maazimio ya Umoja wa Mataifa (UN) ambayo serikali yetu ni mwanachama. Lakini nchi ya Tanzania kama taifa, na watu wake wote kwa ujumla wake; hawajachafuliwa. Kama Nchi ya Tanzania, na wananchi wake wote wakatoa kauli ya pamoja ya kuwatetea watu wachache ndani na nje ya serikali waliotajwa katika kashfa hii; hapo ndipo tutakapochafuka wote kwa ujumla wake. Lakini kama Nchi yetu, na watu wake; tukakubaliana kuchukua hatua ya kusafisha uchafu unaoichafua sisi na taifa letu; ni wazi tutasafishika na heshima ya taifa letu itaendelea kulindwa na kujilinda kote duniani.

Kwa kutumia lugha ya picha; ni kama vile nchi yetu ni mtaro; sasa mtaro unaweza kuwa na uchafu, ukipiga kelele kwamba hakuna uchafu wakati uchafu unaonekana basi utaonekana una utamaduni wa uchafu ndio maana unaona ni jambo la kawaida kuwa kwenye mazingira ya uchafu; wewe ni mchafu. Lakini ukichukua hatua ya kuingia ndani ya mtaro, na zana zako za kusafishia; utachafuka kidogo, utaweza kusafisha mtaro, utatoka na utajisafisha. Mtaro utabaki safi, na wewe utabaki safi; na wewe na mtaro wako wote mtakuwa safi na kuitwa wasafi.

Kadhilika kwa Tanzania, mjadala huu kuhusu uchafu iliotolewa na ripoti ya UN unapaswa kuendelea ili tuujue vizuri uchafu wenyewe wakati wa mjadala huu tutaonekana kuwa tuna uchafu lakini tutaweza kuingia tukachafuka kidogo tukausafisha na nchi yetu itabaki ikiwa safi na sisi wenyewe tutathibitika mbele ya jamii ya kimataifa kuwa ni wasafi na hatupendi uchafu na unapojitokeza tunachukua hatua za kuuondoa.
Hivyo, naandika waraka huu kwa tahadhari kubwa ya kizalendo kwa kuwa najua suala hili linagusa kwa namna au nyingine vyombo vyeti na masuala tete yanayoelekezwa kwa nchi yetu yanayogusa jeshi, polisi, usalama wa taifa, chama tawala, serikali yake, na viongozi wake. Mambo ninayoandika pia yanagusa genge la mafisadi na watumiaji vibaya wa madaraka; wengine wakiwa ni wafanyabiashara, wengine wakiwa ni viongozi, wengine wakiwa ni wahalifu waliokubuhu na waasi wenye kufanya mauaji.

Katika mukatadha huo, ni muhimu kwa wananchi kupuuza kauli za wenye kueneza uchochezi kwamba CHADEMA iache siasa zenye kuichafua Tanzania; eti itangulize ‘uzalendo’. Wananchi wajiulize ni nani anaichafua Tanzania; kati ya waliofanya ufisadi na/ama kutumia madaraka vibaya na kuitumbukiza Tanzania katika kashfa kama hizi za usafirishaji wa silaha na utoroshaji wa madini kutoka maeneo yenye vita vya wenyewe kwa wenyewe au mtu anayetaka mjadala kuhusu suala hili ili utoke msimamo wa pamoja wa wazalendo wote wenye kukerwa na mambo hayo ili kulirudisha taifa kwenye mkondo unaostahili wenye kulinda heshima ya Tanzania kitaifa na kimataifa?

Hawa wangetaka kutanguliza maslahi ya pamoja ya Tanzania wasingekurupuka kutoa kauli ya serikali ya CCM bila kushirikisha umma wa watanzania ama wawakilishi wa wananchi. Viongozi wa serikali hawana haki ya kusema kwa niaba ya watanzania katika masuala tata bila kupata maoni yetu au ya kambi yetu bungeni. Wananchi tuwaambie wazi watu kama hao kwamba; kila wanachokisema ni msimamo wao na serikali ya chama chao au taasisi zao; hakiwakilishi msimamo wa watanzania wote.

Waambie wazi kuwa kama wanataka watanzania tusivuane nguo hadharani; walio kwenye mamlaka ; kabla ya kutoa kauli, walau waombe maoni ya wawakilishi wa wananchi au taasisi zinazowakilisha wananchi; diplomasia iliyokomaa inatambua umuhimu wa maridhiano baina ya viongozi kabla ya kutoka hadharani katika masuala tete ya kitaifa. Tuko tayari kwa majadiliano kama watanzania kuhusu suala hili ili tutoke na msimamo wa pamoja kama taifa. Kuhoji uzalendo wa wanaotaka watanzania waliotajwa kwenye ripoti ya Kikundi cha Wataalamu kilichoundwa na UN ni sawa na kuwatetea mafisadi ama waliotumia vibaya madaraka yao waliotuhumiwa kwenye ripoti husika.

Ikumbukwe kuwa tuhuma za Tanzania kujihusisha na vita vya DRC zilianza toka wakati taifa hili linaasisiwa. Tofauti ya watawala wa sasa ni kwamba uongozi wa Nyerere ulikuwa unasema wazi kuwa unasaidia waasi, na UN inajua. Lakini wakati ule walioitwa waasi ni wazalendo waliokuwa wakipambana dhidi ya watawala wa kidikteta ambao walikuwa ni makuwadi wa ubeberu na ukoloni mamboeleo katika Afrika. Sera ya wakati huo ya mambo ya nje ya Tanzania ilikuwa ni kuleta ukombozi Afrika nzima (hata ikiwa ni kwa kuunga mkono vita vya msituni) na kueneza umajumuhi wa kiafrika (Pan Africanism).

Serikali ya sasa ipo tofauti; kwanza haina msimamo endelevu; pili, sera yake ya mambo ya nje haieleweki; tatu, masuala ya sasa ya usafirishaji wa silaha ama utoroshaji wa madini toka maeneo yenye vita ambao yanasemwa kuwa yanafanywa na serikali ama watanzania yanahusu zaidi miradi binafsi ya watu ambayo wanaindesha kwa ama kuzitumia taasisi za kiserikali au kuruhusu mianya kwa kutowajibika kusimamia utawala wa sheria ikiwemo kuheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa (UN) ambayo nchi yetu imetia saini.

Hivyo wapenda demokrasia na maendeleo ndani na nje ya Tanzania wanapaswa kuunga mkono rai tuliyoitoa Disemba Mosi, 2009: Kwamba wazalendo wote, waliokerwa na Tanzania ‘kuchafuliwa’ na ripoti hiyo ya Kikundi cha Wataalamu wa UN, wanapaswa kuwashinikiza watanzania wote wanaoishi Dar es salaam, Kigoma na kote duniani ambao wametajwa kwenye taarifa hiyo kwa majina yao; wajitokeze kutoa kauli za kusafisha majina yao, tukiridhika na hoja zao, katika utetezi wao; basi na sisi tutajiunga katika kundi la kuwatetea na kuwasafisha. Viongozi na taasisi za serikali zilizotajwa kwa namna moja au nyingine katika taarifa hiyo iwe kwa majina au kwa matukio zijitokeze kuelezea kutajwa kwao; tukiridhika na maelezo yao na vielezo vyao, tutajiunga katika kazi ya kizalendo ya kuwatetea na kuwasafisha. Na hii isiwe kwa taarifa ya UN pekee; iwe pia Orodha ya Mafisadi, katika vipengele vinavyohusiana na Kampuni za Meremeta, Tangold, Deep Green nk.

Kosa kubwa la Wizara ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa katika sakata hili ni kufikiri kwamba yenyewe tu ndiyo inayowajibika kulitolea ufafanuzi na taarifa kuhusu tuhuma zilizoibuliwa na Kundi la wataalamu lililoundwa na UN. Wakati umefika sasa wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwashinikiza Mawaziri wengine ambao sekta zao zimeguswa kutoa kauli za kujibu ama kufafanua hoja zilizoibuliwa ndani ya ripoti hiyo, ambayo tayari Wizara ya Mambo ya Nje ameshafanya kosa la kisiasa la kuitumbukiza serikali kwenye malumbano mapema kwa kuliibua suala hili na kuituhumu UN kabla hata Tanzania kufafanua ama kujieleza kwenye Kamati ya Vikwazo. Kwa kuanzia ni muhimu kwa Wizara ya Mambo ya Usalama wa Raia na ile ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa zikatoa maelezo na vielelezo kuhusu suala hili. Hivyo, mawaziri wanaopaswa kufutia kutoa kauli ni: Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Hussein Mwinyi na Waziri wa Usalama wa Raia; Lawrence Masha.
Ikumbukwe kuwa Tarehe 2 Disemba 2009 Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa Tanzania haihusiki kwa namna yoyote ile katika kashfa ya kuwapatia silaha waasi wa serikali za mataifa mengine kama ilivyotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari. Mratibu wa Udhibiti wa Silaha hapa nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Dominick Hayuma, amesema kuwa taarifa za Kundi la Wataalamu lililoteuliwa na UN hazina ukweli wowote. Amesema kuwa Tanzania ina uhusiano mkubwa na serikali za nchi jirani na ndiyo maana majeshi ya polisi katika ukanda wa nchi za Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika na zile za kusini mwa Afrika (SADC) zinashirikiana katika masuala ya operesheni kwa lengo la kudhibiti kwa pamoja vitendo vya kihalifu. Amesema kuwa kuna baadhi ya mashirika ya ndani na nje ya nchi wanakusanya taarifa za uongo kwa lengo la kujipatia fedha ama kuleta uchochezi baina ya nchi moja na nyingine.
Nichukue fursa hii kuwatahadharisha wataalamu wetu wa polisi kutokuingizwa kutoa kauli za kisiasa katika mambo yanayostahili maelezo na vielelezo. Ni vizuri zikatolewa kauli za kisera kuhusu masuala hayo; ushahidi wa kuingia ama kutoka kwa silaha za kijeshi katika nchi yetu uko wazi hata kwa wananchi waoishi katika mikoa ya mpakani na nchi za eneo la maziwa makuu. Wananchi ni muhimu wawatake polisi ambao tunawalipa kwa kodi zetu, wakae mbali na mijadala ya kisera na ya kisiasa ili kutenganisha kati ya jeshi na propaganda za wanasiasa. Tabia hii ya kutumwa na viongozi wa CCM ndio ambayo inafanya Polisi wetu kushiriki katika kuiba kura na kuhujumu wapinzani wakati wa uchaguzi. Polisi wetu wajue kwamba mishahara midogo wanayolipwa na maslahi duni wanayoyapata ni matokeo ya uongozi mbovu wa serikali hiyo hiyo ya CCM inayofanya waweke pembeni maadili ya taaluma zao; na kuitetea na hata kuipigania nyakati za uchaguzi. Hivyo, polisi ikae mbali na mapambano ya kisiasa baina ya vyama, ikiwemo mapambano ya hoja kwa ajili ya kupata msimamo wa pamoja wa watanzania. Polisi ibaki na jukumu la kusimamia sheria na kuhakikisha kwamba utawala wa sheria unazingatiwa badala ya kukanusha tu bila maelezo na vielelezo ripoti ya Kundi la wataalamu wa UN ambayo imewataja kwa majina watanzania wanatuhumiwa kuvunja sheria lakini polisi haijawakamata mpaka sasa.

Ni muhimu kwa Wizara ya Usalama wa Raia hususani kupitia kwa Waziri Lawrence Masha ikitoa tamko ikiwemo kutoa maelekezo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwachunguza watu wote na taasisi zote za Tanzania zilizotuhumiwa kwenye ripoti hiyo likiwemo jeshi la polisi lenyewe. Wizara ya Usalama wa Raia ijibu maswali na kufafanunua masuala yafuatayo, ikiwemo kwa kutoa maelezo na vielelezo kwa Umoja wa Mataifa kwamba: Je, taarifa ya kwamba polisi waliizunguka meli inayotuhumiwa katika ripoti hiyo ya Kundi la Wataalamu wa UN anaizungumziaje? Je, polisi hao walikuwa wa nchi gani? Kama ni watanzania walikwenda kufanya nini kwa maelekezo ya nani? Aidha ripoti ya Kundi la Wataalamu, inataja kwamba yapo maduka ya masonara yaliyokuwa yananunua madini yaliyotoroshwa kutoka DRC? Na kwamba kwa maelezo ya mmojawapo wa wamiliki wa maduka yaliyotajwa kwenye taarifa hiyo alidai kwamba kuna wakati ambapo idara ya uhamiaji iliwahi kuendesha msako dhidi ya wafanyabiashara hao? Je, serikali inayazungumziaje madai hayo? Je, serikali yake iko tayari kuwachunguza raia wote wa kigeni wanaotajwa kwenye ripoti hiyo wanaoishi mpaka sasa Dar es salam, Kigoma na kwingineko katika nchi yetu? Je, Wizara yake inamzungumziaje raia wa DRC aliyetajwa katika ripoti ya Kundi la Wataalamu wa UN kwa jina la Bande Ndagundi, ambaye anatuhumiwa kuishi nchini kwa zaidi ya miaka 27 anayejishughulisha na biashara zinazohusiana na masuala ya kijeshi? Je, Waziri Masha au wawakilishi toka Wizara yake wamewahi kuwasiliana na mtu huyo anayedaiwa kuendelea kuishi Dar es salaam? Ni muhimu kwa Wizara hususani Waziri husika kutoa kauli kuhusu mtu huyu kwa kuwa imeelezwa kwa uwazi ikiwemo kwa yeye mwenyewe kusema kwenye barua zake ikiwemo ile ya tarehe 17 July 2009 kuwa ana mawasiliano ya karibu na viongozi wa juu wa serikali, polisi, jeshi na chama tawala.

Masuala haya na mengine mengi zaidi nikayoyachambua kadiri siku zinavyokwenda yanapaswa kujadiliwa na wananchi ama wawakilishi wao; ili tuweze kutoka na msimamo wa pamoja. Pia UN na Kundi la Wataalamu wake kuiuliza serikali itoe maelezo ya kina wakati wa mapitio ya taarifa husika. Ni utaratibu wa kawaida kwamba ufuatiliaji kama huu uliofanywa kwa kuwa ulihusu Tanzania; serikali itapewa fursa kuandika ripoti ya nchi (country report) kufafanua mambo ambayo yametajwa kabla ya kamati ya vikwazo kufanya maamuzi yake ama kuikubali ripoti husika na mapendekezo yake ama kutoa maelekezo mbadala ya kutaka uchunguzi zaidi katika maeneo ambayo Kundi la Wataalamu limeeleza katika ripoti yake kuwa uchunguzi wake bado haujamilika. Inashangaza kwamba serikali inatumia nguvu kubwa, kubeza ripoti hii na kutishia wanahabari wasiendelee kuandika wakati ripoti imeweka bayana kwamba uchunguzi bado haujakamilika; serikali itaweka wapi uso wake kama uchunguzi zaidi ukaibua uchafu zaidi? “Tuchafuke tusafishe tujisafishe: kujadili ni uzalendo wa kutetea maslahi ya taifa”


Imetolewa na:


John Mnyika
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa
0754694553


No comments: