Monday, June 27, 2011

Tahadhari na kauli za Pinda kuhusu Katiba Mpya

Tarehe 25 na 26 Juni 2011 Vyombo mbalimbali vya habari vimemnukuu Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitangaza kwamba katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itazinduliwa tarehe 26 Aprili 2014 katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano.
Kufuatia ahadi hiyo ya Waziri Mkuu, baadhi ya wananchi wa Ubungo na vyombo mbalimbali vya habari mmetaka kupata kauli yangu kuhusu tamko husika. Naomba kuwasilisha kwenu maoni yangu yafuatayo:

Pamoja na kutambua kwamba hatimaye Serikali imetangaza muda rasmi wa ukomo wa kukamilika kwa mchakato husika bado ahadi hiyo ya Waziri Mkuu Pinda inapaswa kupokelewa kwa tahadhari na anapaswa kutoa kauli ya kina bungeni itayoambatana na kuweka ratiba katika mipango, maazimio na sheria.

Hii ni kwa sababu katika Hotuba yake bungeni kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Bunge ya mwaka 2011/2012 Waziri Mkuu Pinda hakueleza tarehe hiyo badala yake alitoa tu kauli ya ujumla kwamba “Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba dhamira inatekelezwa ili nchi yetu iwe na katiba mpya kabla ya mwaka 2015”. Hivyo, ni muhimu ukomo huo wa Aprili 2014 kuwasilishwa rasmi bungeni kupitia kauli ya serikali au kupitia majumuisho ya hotuba ya Waziri Mkuu kabla ya mjadala wa muswada wa sheria na uzingatiwe katika mipango, maazimio na sheria.

Ikumbukwe kwamba tarehe 19 Disemba 2010 na 27 Disemba 2010 kupitia mikutano na wanahabari wakati nikieleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi kuhusu mchakato wa katiba mpya na kutoa taarifa ya hoja husika nilieleza bayana kwamba kati ya mambo ambayo yanapaswa kupangwa na bunge ni pamoja na muda wa mchakato wa katiba mpya; suala ambalo lisingezingatiwa katika mchakato uliotangazwa awali kufanywa na serikali bila kuanzia bungeni.

Nilieleza wasiwasi wa wadau mbalimbali kuwa ukomo wa muda usipowekwa kwa mujibu wa sheria ama maazimio ya bunge, serikali inaweza kuchelewesha mchakato mzima kwa kutoa visingizio mbalimbali ili usikamilike mapema kuwezesha maandalizi ya kisheria na kitaasisi kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia katiba mpya.
Aidha umma unapaswa kuipokea ahadi hiyo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa kupitia Semina Elekezi kwa wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wa mikoa kwa tahadhari kwa kuwa imeambatana na kauli tata kuhusu mchakato mathalani serikali kutokuwa na uhakika kuhusu wakati ambapo muswada wa sheria ya mapitio ya sheria ya marekebisho ya katiba wa mwaka 2011 utawasilishwa bungeni.

Waziri Mkuu Pinda amenukuliwa akisema kwamba muswada huo utawasilishwa bungeni mwishoni mwa mkutano wa nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa au mwanzoni mwa mkutano wa tano wa bunge utakaofanyika Oktoba 2011; wakati katika mkutano wa tatu wa bunge Waziri Mkuu aliahidi kwamba muswada huo utarejeshwa katika mkutano wa nne wa bunge.
Ikumbukwe kwamba tarehe 30 Machi 2011 nilitoa tamko la kueleza kushtushwa na maudhui ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011 (The Constitutional Review Act 2011) uliochapwa katika gazeti la serikali toleo No. 1 Vol. 92 la tarehe 11 Machi 2011.

Nilieleza kwamba maudhui ya muswada huo yamedhihirisha tahadhari niliyotoa mara kadhaa kwamba serikali haina dhamira ya kweli ya kuhakikisha panakuwepo na mchakato mzuri wa kuwa na katiba mpya; matokeo yake ni muswada huo uliowasilishwa kwa hati ya dharura kuondolewa katika ratiba ya kupitishwa katika mkutano wa tatu wa bunge kutokana na shinikizo la wadau mbalimbali. Hivyo, Waziri Mkuu Pinda anapaswa kutoa kauli bungeni kueleza bayana iwapo hati ya dharura ya muswada huo ilifutwa basi muswada husika uwasilishwe kwa kufuata taratibu za kawaida kwa mujibu wa kanuni za bunge.

Pia, umma unapaswa kuipokea kwa tahadhari ahadi hiyo ya Waziri Mkuu kwa kuwa imeambatana na kutolewa kwa maelekezo kwa wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala kuhusu maudhui ya mchakato wa katiba na kipi kinakusudiwa kufanywa na serikali wakati ambapo bado sheria haijapitishwa na bunge.

Maelekezo hayo ya Waziri Mkuu Pinda yanadhihirisha kwamba tayari serikali imeshachukua msimamo kuhusu mchakato utakaotumiwa kuandika katiba mpya hiyo; hali inayoashiria kuwa serikali ina dhamira ya kulitumia bunge kama muhuri (rubber stamp) ya kupitisha mchakato ambao tayari ulishapitishwa ndani ya serikali na maelekezo ya utekelezaji kuanza kutolewa kwa watendaji wa serikali ngazi ya chini kabla ya sheria kupitishwa.

Ikumbukwe kwamba tarehe 30 Machi 2011 nilitahadharisha kwamba muswada uliowasilishwa bungeni umelenga kuhalalisha yote ambayo yalitangazwa kufanywa na Rais kuhusu mchakato wa katiba mpya na kupingwa na wadau mbalimbali na yanataka kupewa uhalali kwa sheria inayotaka kutungwa na bunge kupitia muswada huo; mchakato ambao Waziri Mkuu Pinda ameurejea katika hotuba yake.

Kadhalika umma unapaswa kuipokea ahadi hiyo ya Waziri Mkuu Pinda kwa tahadhari kubwa kwa kuwa imeambatana na maelekezo ya kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya wawe mstari wa mbele kuongoza mchakato huo wakati inaeleweka wazi kwamba wadau mbalimbali wamelalamikia mamlaka waliyopewa watendaji wa serikali katika mikutano ya kukusanya maoni kuhusu katiba kwa mujibu wa muswada uliowasilishwa awali ambao wananchi walitaka vifungu husika vibadilishwe.

Ikumbukwe kwamba watendaji hao wamelalamikiwa kwa miaka kadhaa kutumia madaraka yao vibaya ikiwemo kudhibiti uhuru wa wananchi katika kutoa maoni kwenye tume mbalimbali ambazo zimewahi kuundwa na serikali nyakati za nyuma kwa masuala mbalimbali ikiwemo yanayohusiana na marekebisho ya katiba. Aidha kati ya mambo ambayo wananchi wameanza kuyatolea maoni kwenye maudhui ya katiba ni pamoja na kutaka kufutwa au kupunguzwa mamlaka ya wakuu wa mikoa na wilaya; hivyo kitendo cha kuwaweka mstari wa mbele katika mchakato ni dalili za serikali kutokuwa na dhamira ya kweli ya kutaka mabadiliko ya katiba.

Katika muktadha huo; na kwa kuwa serikali ilishawasilisha awali muswada wa katiba natoa mwito kwa Spika na Ofisi ya Bunge kuhakikisha kwamba bunge linachukua nafasi yake kuanzia hatua za msingi kuhakikisha suala hili la mchakato wa katiba mpya lipata uhalali wa umma kwa kurejea ibara 8 ambayo inatamka kwamba madaraka na mamlaka ni umma serikali inafanya kazi kwa niaba na Bunge ndicho chombo kikuu cha kusimamia wajibu huo kwa kutokana na mamlaka ya kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63(2) na (3) yanayohusu kutunga sheria na ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya katiba.

Hivyo, badala ya kusubiri mpaka mwishoni mwa mkutano huu wa bunge tarehe 29 mpaka 30 Agosti 2011 ndipo wabunge wapewe tena muswada wa mabadiliko ya katiba pamoja na marekebisho yake yaliyofanyika ikiwemo tafsiri katika lugha ya Kiswahili; utaratibu wa kikanuni ufanyike kuhakikisha taarifa ya serikali inatolewa mapema pamoja na muswada huo nyeti.

Kwa upande mwingine umma unapaswa kuzipokea kwa tahadhari kauli za Waziri Mkuu Pinda kuhusu mchakato wa katiba mpya kwa kurejea msimamo wa wake wa awali kuhusu mabadiliko ya katiba alioutoa wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari tarehe 17 Disemba 2010 ulikuwa na kumshauri Rais aunde jopo shirikishi ili kuratibu na kusimamia mchakato husika.

Izingatiwe kuwa tarehe 9 Februari 2011 nilitoa tamko la kupokea kwa tahadhari uamuzi wa Serikali kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kubadili misimamo ya awali kuhusu mchakato wa katiba mpya na kuamua kukubaliana na mwito wa kutaka mchakato husika uanzie bungeni kupitia kutungwa kwa sheria ya bunge ya kuratibu na kusimamia mchakato husika kwa kuwa maneno ya kauli zilizotolewa hayaambatani na vitendo vya dhati vya kuweka mchakato mzuri wa katiba mpya.

Uthibitisho wa mwelekeo huo ni kwamba Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/2012-2015/2016) uliotiwa saini na Rais Kikwete tarehe 7 Juni 2011 haukuweka kipaumbele haja ya katiba mpya kwenye eneo la utawala bora na utawala wa sheria. Aidha, bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 haikuweka bayana na kwa kiwango cha kutosha rasilimali kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya suala ambalo pamoja na maelezo ya Waziri wa Fedha wakati wa kuhitimisha hoja bado serikali ina wajibu wa kulitolea ufafanuzi wa kina katika mkutano wa Bunge unaoendelea.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)

1 comment:

togolai richard said...

pambana mkuu, tuko pamoja