Monday, June 27, 2011

Mgawo wa Fedha za Mfuko wa Jimbo

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika anatoa taarifa kwa umma kwamba utekelezaji wa miradi iliyochangiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) kwa mwaka wa fedha 2010/2011 awamu ya kwanza uko katika hatua za mwisho na kwamba mchakato wa uteuzi wa miradi ya awamu ya pili umeanza.

Ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu kwa mujibu wa Sheria namba 16 ya mwaka 2009 iliyounda mfuko husika, Mnyika ameitisha kikao cha kamati ya usimamizi wa mfuko wa jimbo ambacho kitafanyika tarehe 27 Juni 2011 katika ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni.
Pamoja na ajenda nyingine kikao hicho kitapokea taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika kukamilisha miradi iliyoteuliwa katika awamu ya kwanza.

Miradi inayoendelea kutekelezwa kutokana na fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo la Ubungo katika mgawo wa awamu ya kwanza iliyopangiwa jumla ya shilingi 70,245,433 ni pamoja na: Ukarabati wa Jengo la Kutoa huduma ya afya kwa wakinamama wajawazito na watoto Kata ya Kwembe Mtaa wa Msakuzi (27,245,433); Kuchangia ujenzi wa Kituo Kidogo cha Polisi Kata ya Ubungo Mtaa wa Msewe(6,000,0000); Ujenzi wa Vyoo katika Shule ya Sekondari ya Hondogo Kata ya Kibamba Mtaa wa Kiluvya (22,000,000); Ununuzi wa madawati 200 ya Shule ya Sekondari Mburahati katika kata ya Mburahati (13,000,000) na Kuchangia Vifaa vya Ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Kimara Mtaa wa Mavurunza.

Aidha, Mbunge anapenda kuwataarifu wananchi kwamba fedha za mfuko wa kuchochea maendeleo zilizotengwa kwa Jimbo la Ubungo katika mgawo wa awamu ya pili ni shilingi 69,819,663. Fedha hizo zimetolewa toka Serikali Kuu kwa vipindi viwili; Mei 2011 (Tshs 34,910,000) na Juni 2011 (Tsh. 34,909,663) na kuingizwa katika akaunti ya mfuko inayoratibiwa na Manispaa ya Kinondoni.

Mnyika amesema kwamba kikao cha kamati ya kusimamia mfuko atakachokiongoza kitaanza uteuzi wa miradi itayochangiwa na mfuko huo kutokana na mambo mbambali yaliyowasilishwa. Mnyika amehimiza wananchi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa maendeleo ya jimbo.

“Pamoja na kuwa mfuko huu unachochea jitihada hizo za maendeleo, bado naendelea kuunga mkono harakati za wadau wengine za kutaka mabadiliko katika mfumo mzima wa sheria iliyounda mfuko husika kutokana na kuiingiliana na majukumu ya mbunge kwa kuzingatia matakwa ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63(2) na (3). Hata hivyo wakati marekebisho hayo yakisubiriwa ni muhimu kuhakikisha uwajibikaji katika hatua zote” , amesema Mnyika.

Mnyika amesema kwamba maendeleo yenye kugusa watu wengi na sekta nyingi yanaletwa kwa kupitia uwajibikaji katika Baraza la Madiwani na Bungeni kwa kuzisimamia serikali za mitaa, serikali kuu na taasisi zake sanjari na kuunganisha nguvu ya umma ya sekta binafsi.

Imetolewa tarehe 26 Juni 2011 na:

Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge

2 comments:

Anonymous said...

noMi ni mwananchi wa Goba, wananchi wengi wanauliza, kile kikao chako cha mwisho Diwani wetu aliahidi, Kujenga Daraja linaunganisha Makongo na Goba na alisema mkandarasi alishapatikana na kazi itaanza mapema, lakini mpaka sasa kimya.

Alizungumzia kuwa Kituo cha polisi mpaka leo hamna kinachoendelea na wanchi wanauliza kama mtefunya wajinga au ?

Ishu ya tatu alisema tank la maji limesha jengwa na sasa tutapata maji kupitia tegeta B, lakini mpaka sasa kimya, wananchi nao wanauliza pia.

Mwisho wanaulizia swala barabara, mwaka huu tupo kwenye mpango wa rami,

OMBI LETU, KUNA TIMU YA GOBA-HAM UNITED HATUNA JEZI TULIKUWA TUNAOMBA MSAADA KUTOKA KWAKO. PIA TUNAOMBA UANZISHE MNYIKA CUP

MHESHIMIWA TUNAOMBA MAJIBU KWA HAYO MAOMBI NA MASWALI YETU
ndimi
Mwaikambo

MMATUMBI WA CHUMO said...

Mi ni mwananchi wa Goba, wananchi wengi wanauliza, kile kikao chako cha mwisho Diwani wetu aliahidi, Kujenga Daraja linaunganisha Makongo na Goba na alisema mkandarasi alishapatikana na kazi itaanza mapema, lakini mpaka sasa kimya.

Alizungumzia kuwa Kituo cha polisi mpaka leo hamna kinachoendelea na wanchi wanauliza kama mtefunya wajinga au ?

Ishu ya tatu alisema tank la maji limesha jengwa na sasa tutapata maji kupitia tegeta B, lakini mpaka sasa kimya, wananchi nao wanauliza pia.

Mwisho wanaulizia swala barabara, mwaka huu tupo kwenye mpango wa rami,

OMBI LETU, KUNA TIMU YA GOBA-HAM UNITED HATUNA JEZI TULIKUWA TUNAOMBA MSAADA KUTOKA KWAKO. PIA TUNAOMBA UANZISHE MNYIKA CUP

MHESHIMIWA TUNAOMBA MAJIBU KWA HAYO MAOMBI NA MASWALI YETU