Thursday, June 30, 2011

Hoja Binafsi kuhusu uvamizi wa viwanja vya wazi vya umma

Mtakumbuka kwamba mwezi Machi 2011 niliwaeleza kwamba nimewasilisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni hoja binafsi kuhusu uvamizi/uuzwaji wa viwanja vya wazi ili ipangiwe tarehe ya kuwasilishwa na kujadiliwa kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Hata hivyo, toka wakati huo uongozi wa Manispaa umekuwa ukipiga danadana hoja hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa pamoja na kuwa katika kipindi husika kumefanyika vikao viwili vya baraza la madiwani. Katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Kinondoni cha kawaida cha tarehe 18 Juni 2011 hoja hii haikuingizwa kwenye taratibu kama kanuni zinavyohitaji. Ili kuongeza msukumo kwa hatua kuchukuliwa kwa haraka zaidi kama sehemu kuisimamia serikali naomba kuwajulisha kuwa nimeamua kuchukua hatua zifuatazo:

Mosi; kutumia bunge kuhoji kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa na serikali kuu baada ya ripoti ya kamati ya uchunguzi. Hii ni kwa sababu ufisadi uliofanyika katika ardhi umehusisha pia baadhi ya maofisa wa serikali kuu hususani wa Wizara ya Ardhi. Aidha, mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti yamehusisha pia masuala ambayo mengine yako juu ya halmashauri yakitaka hatua kutoka kwa jeshi la polisi ngazi za juu, TAKUKURU ngazi za juu, uongozi wa Mkoa wa Dar es salaam, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI nk. Ili ufuatiliaji uwe rahisi, nitataka ripoti nzima ya kamati ambayo mpaka sasa imefanywa kuwa siri; iwekwe hadharani.

Pili; Kuiwasilisha hoja binafsi husika kwa umma (nakala inafuata hapa chini); ili hatua zisipochukuliwa katika kipindi cha miezi hii miwili ambayo nipo bungeni Dodoma tuanze maandalizi nikirejea tushirikiane na madiwani wa kata husika kuunganisha nguvu ya umma katika mitaa yenye viwanja husika mpaka kieleweke. Wakati mimi nikiendelea na hatua za kibunge, naendelea na mawasiliano na madiwani pamoja na uongozi wa manispaa ili nao waharakishe kuanzia sasa kuchukua hatua kupitia kamati mbalimbali za manispaa kwenye masuala ambayo wana mamlaka nayo kabla ya kikao kijacho cha baraza la madiwani.HOJA BINAFSI KUHUSU UUZWAJI/UVAMIZI WA VIWANJA VYA UMMA KWENYE BAADHI YA KATA ZA JIMBO LA UBUNGO KATIKA MANISPAA YA KINONDONI

Maelezo ya Hoja

Nawasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa Kanuni ya 19 ya Kanuni za kudumu za Halmashauri na kanuni nyingine kwa nafasi yangu ya ujumbe wa baraza husika kuwa:

KWA KUWA katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 mpaka 2010 pamekuwepo malalamiko mbalimbali ya wananchi kuhusu uvamizi ama uuzwaji wa viwanja vya umma maarufu kama viwanja vya wazi katika maeneo ya kata mbalimbali za jimbo la Ubungo.

KWA KUWA kutokana na malalamiko hayo tumekuwa tukitoa shinikizo wa serikali kuweza kuchukua hatua za haraka ikiwemo kwa kuweka hadharani baadhi ya taarifa za uuzwaji ama uvamizi wa viwanja vya umma.

KWA KUWA hatimaye tarehe 24 May 2010 Rais Jakaya Kikwete wakati akifanya majumuisho ya ziara ya kukagua hali ya maji katika mkoa wa Dar es Salaam alikiri kuwa yapo maeneo mengi ya wazi yaliyovamiwa na kuwa madiwani wanahusika na sakata hilo.

KWA KUWA kufuatia kauli hiyo ya Rais na malalamiko ya umma Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitembelea Manispaa ya Kinondoni tarehe 15 Juni 2010 na kubaini mapungufu kadhaa ya kiutendaji kuhusiana na masuala ya ugawaji wa ardhi yakiwemo maeneo ya umma yaliyozoeleka kuitwa viwanja vya wazi.

KWA KUWA kufuatia malalamiko mengi ya wananchi aliyoyapokea na pia kufuatia habari mbalimbali zilizotolewa na vyombo vya habari aliunda kamati maalumu ya kuchunguza maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa katika mkoa wa Dar es Salaam. Kamati hiyo iliundwa tarehe 18 Juni 2010 na pamoja na mambo mengine ilipewa hadibu za rejea ambazo ziliiongoza kamati tajwa kufanya kazi yake.

KWA KUWA taarifa ya tume hiyo ilibaini kuwa Manispaa ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na maeneo mengi ya wazi yaliyovamiwa. Maeneo hayo yanahusisha pia viwanja vya wazi katika kata mbalimbali za jimbo la Ubungo ambalo mimi ni mbunge wake na mjumbe wa baraza la madiwani.

Msingi wa Hoja

Ninaomba kuwasilisha hoja binafsi katika baraza hili ili kupata maelezo na vielelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa na Manispaa kuhusu maelekezo ya kamati katika maeneo yafuatayo;

Kiwanja Na. 1022 Kitalu E Sinza. Kamati ilibaini kuwa katika kiwanja hiki kuna Ofisi ya Afisa Mtendaji na banda lenye vyumba vitano vya biashara na msingi wa jengo ambalo halijakamilika. Kamati ilishauri pamoja na mambo mengine kuwa ufanyike uchunguzi wa kipolisi kwa kuwa eneo hilo bado lipo wazi. Nataka kujua kama huo uchunguzi umefanyika na nini kimebainika katika uchunguzi huo.

Eneo karibu na kiwanja Na. 636 Kitalu E Sinza. Eneo lilibainika kuwa wazi ila limemegwa pande zote mbili na kuna matofali machache yamewekwa. Kamati ilielekeza kuwa Halmashauri irudishe mipaka ya kiwanja hiki na hatua ya kulitangaza kama eneo la wazi kwa mujibu wa sheria.Je Halmashauri imesharekebisha mipaka na kulitangaza eneo kuwa wazi? Na kama bado Halmashauri ina mpango gani wa kutekeleza agizo hilo na lini?

Eneo karibu na viwanja Na. 281, 282, 283 na 287 Sinza B. Eneo hili limejengwa ofisi ya Mtendaji kata Sinza D. Kamati ilishauri kuwa eneo lililobaki litangazwe kama eneo la wazi kwa mujibu wa sheria na sehemu ilipojengwa ofisi ya kata eneo hilo lipimwe.
Naomba kupata maelezo kama ushauri huo wa kamati umetekelezwa na Halmashauri.

Eneo karibu na viwanja Na. 411, 413,414 na upande mwingine kinapakana na 698 na 609 Sinza Block D, sehemu kubwa ya eneo hili ipo wazi na pia kimechimbwa kisima cha umma na kuna jiwe la msingi lenye shina la wakereketwa wa chama cha mapinduzi (CCM). Kamati ilishauri eneo lipimwe na kutumika kama eneo la wazi kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa sheria. Je halmashauri imeshapima eneo hilo na kuwaondoa wavamizi hao waliobainika?

Kiwanja Na. 814, 818 Sinza Block D. eneo hili hutumika kama makazi ya watu na ndiyo waliondeleza eneo hilo. Kamati ilishauri Halmashauri kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini uhalali wa umiliki wa wananchi hao. Je uchunguzi huo umeshafanyika na kama ndiyo, uchunguzi huo ulibaini nini na baraza la madiwani lilipokea taarifa hiyo?

Eneo jirani na viwanja Na. 480 na 481 Sinza Block D. Eneo hili lipo wazi na kamati imeshauri Halmashauri eneo hili lipimwe ili libaki kuwa wazi kwa matumizi yaliyokusudiwa. Je Halmashauri imepima eneo hili na kulitangaza kuwa wazi ili kuepuka wavamizi?

Eneo jirani na kiwanja Na. 37 Sinza Block D ambalo kumejengwa msikiti na mmiliki wake hajulikani. Kamati ilishauri kuwa Halmashauri wafanye uchunguzi wa kina kubaini uhalali wa umiliki huu na hatua stahiki zichukuliwe. Je uchunguzi huo umeshafanyika?

Eneo jirani na viwanja Na. 75 na 77 Sinza Block D. Eneo hili limezungushiwa ukuta na mtu binafsi. Halmashauri ilishauriwa kufanya uchunguzi ili kubaini uhalali wa umiliki wa eneo hili na hatua stahiki zichukuliwe. Je uchunguzi umefanyika na ni hatua gani zilizochukuliwa?

Eneo linalopakana na viwanja Na. 63, 99 Sinza Block D ambalo limejengwa Kanisa la Assemblies of God, Shule ya chekechea, ofisi ya CCM, gereji na pia kuna jengo la ghorofa limejengwa hapo. Halmshauri pia ilishauriwa kufanya uchunguzi wa kina na hatua stahiki zichukuliwe ili kubaini uhalali wa umiliki wa taasisi hizo (kanisa na CCM) na watu binafsi. Je uchunguzi huo ulishafanyika na hatua gani zilizochukuliwa?

Eneo lililopo mkabala na kiwanja Na. 475 Sinza B ambapo kumejengwa shina la wakereketwa wa CCM, mama lishe na pia kuna biashara ya pool inaendelea. Halmashauri ilishauriwa ifanye uchunguzi wa kina na hatua stahiki zichukuliwe. Je ushauri huo ulizingatiwa na Halmashauri?

Eneo karibu na kiwanja Na. 23 Sinza C. Eneo hili hutumika limejengwa ofisi ya Afisa Mtendaji wa mtaa na pia kuna vibanda vya biashara. Kamati ilipendekeza kuwa sehemu ya ofisi imegwe na eneo lililobaki lipimwe na kutangazwa kama eneo la wazi. Je Halmashauri imezingatia ushauri huo?

Eneo karibu na kiwanja Na. 24 Sinza C, ambalo limengwa makazi ya watu. Halmashauri pia ilishauriwa ifanye uchunguzi wa uhalali wa umiliki na hatua stahiki zichukuliwe. Je Halmashauri imezingatia ushauri huu na ni hatua gani walizochukua?

Eneo karibu Na. 765, 789, 790, na 797 Sinza C. Hapa kuna sehemu hutumika kama maegesho ya magari na pia kuna kibanda cha kukaangia chipsi. Kamati ilishauri kuwa Halmashauri itoe amri kuwa wamiliki wa magari kuondoa magari yao na pia upimaji ufanyike na kulitangaza eneo hilo kuwa wazi. Je Halmashauri imeshawaondoa wamiliki wa magari hayo na kuwa wasiendelee kulitumia eneo hilo? Je upimaji na kulitangaza eneo hilo kuwa wazi umeshafanyika?

Eneo la wazi lililozungukwa na viwanja Na. 21, 23, 25, 27, 29 Sinza B. Eneo hili kuna shina la wakereketwa wa CCM ,vibanda vya mama lishe, sehemu za kutengenezea mageti, magenge na kontena la kuuzia vinywaji vikali na baridi. Halmashauri ilishauriwa kuwaondoa wavamizi hawa ili eneo libaki kuwa wazi. Je Halmashauri imeshawaondoa wavamizi hawa?

Eneo la wazi lililozungukwa na viwanja Na.72-74. Eneo limewekwa shina la wakereketwa wa CCM Kawawa kuna mama lishe na vioski. Kamati ilibaini kuwa eneo hili kwa mujibu wa mipango miji ni la wazi na kuishauri Halmashauri iwapeleke mama lishe kwenye maeneo yanayostahili na kupima eneo husika na kulitangaza kuwa wazi. Je nini kimefanyika mpaka sasa na je eneo limeshapimwa na kutangazwa kuwa wazi?

Eneo la wazi linalozungukwa na viwanja Na. 1, 2, 89, 90, 141 na 142 Sinza E. Katika eneo hili kumejengwa nyumba za makazi, Baa na asilimia ndogo ya eneo lipo wazi (baadhi ya namba ya viwanja hivyo ni 655 na 690). Kamati ilishauri kuwa Halmashauri iendelee na uchunguzi na hatua stahiki zichukuliwe. Je uchunguzi huo ulishafanyika?

Eneo la kiwanja cha michezo na Shule ya Msingi Sinza E. Kiwanja kimemilikishwa kwa CCM na kuna vibanda vimejengwa kuzunguka eneo lote na ndani linatumika kama maegesho ya magari. Kamati ilishauri kuwa eneo litumike kwa matumizi yaliyopangwa na shughuli ambazo hazihusiani ziondolewe. Je Halmashauri imeshawapa taarifa CCM kuhusu hili na kutangaza eneo husika kutumika kwa matumizi yaliyopamgwa?

Eneo la wazi jirani na viwanja Na. 77, 79, 81, 151-154, eneo hili limejengwa makazi ya watu na sehemu za biashara. Kamati imeshauri kuwa Halmashauri ifanye uchunguzi wa kina na kuchukua hatua zinazostahiki. Je Halmashauri imechukua hatua gani mpaka sasa?

Viwanja Na. 9 na 10 Sinza A. Wamiliki wa viwanja hivi viwili wamefunga barabara ya kuingia eneo la wazi. Kamati ilishauri kuwa Halmashauri ichukue hatua ya kufungua barabara husika ili eneo la wazi litumike kwa matumizi yaliyopangwa. Je Halmashauri imeshafungua barabara hiyo? Na kama bado nini kinachelewesha utekelezaji huo?

Kiwanja Na. 846 Sinza A. Eneo hili limejengwa nyumba ya makazi na biashara. Katika eneo hili taratibu za kubadili matumizi inasemekana zilifuatwa; je ni kweli?

Jirani na viwanja Na. 38, 40, 44, 46 na 48 Mtaa wa Kibesa Makurumla. Eneo hili limejengwa ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Makurumla. Kamati ilishauri kuwa eneo la ofisi limegwe na taratibu ya kubadilisha matumizi zifuatwe na eneo lililobaki litangazwe kuwa wazi na litumike kama sehemu ya starehe na michezo kwa mujibu wa sheria. Halmashauri imefikia hatua gani juu ya kutekeleza ushauri huo?

Jirani na viwanja Na. 18 na 19 Mtaa wa Malala Makurumla. Kuna wavamizi wasiorasmi wanalitumia eneo hili kama gereji. Kamati ilishauri kuwa wavamizi waondolewe na kutokana na uhaba wa maeneo ya wazi katika maeneo hayo, eneo hilo litumike kama kiwanja cha wazi. Je Halmashauri imeshaweka utaratibu mbadala kwa ajili ya gereji husika ?

Jirani na viwanja Na. 73, 78, 80, 82, 84 na 86 Mtaa wa Mengo Makurumla, eneo hili limevamiwa na wavamizi wasiorasmi. Ushauri wa kamati ni sawa na uliopo hapo juu. Je Halmashauri imeshaweka utaratibu mbadala kwa wajasiriamali husika?

Eneo la wazi lililopo Mtaa wa Kagera Makurumla limevamiwa na na kuna ofisi ya CCM Tawi la Karume Kata ya Makurumla na pia kuna banda linalotumika kama sehemu ya biashara. Kamati ilibaini kuwa wahusika walishapewa notisi ya kuondoka na hivyo Halmashauri ichukue hatua ya kuwaondoa wavamizi hao. Je Halmashauri imewaondoa wavamizi hao?

Eneo la wazi nyuma ya Ubungo terminal (“buffer zone” ya reli) limejengwa vibanda vya biashara. Kamati ilibaini kuwa eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya reli hivyo basi vibanda hivyo viondolewe ili kuacha eneo litumike kama ilivyokuwa imepangwa. Je Halmashauri imeshaweka utaratibu mbadala wa kuwapa wafanyabiashara hao maeneo ya biashara ikiwa bado kuna azma ya kuboresha matumizi ya reli kwa usafiri wa ndani ya mkoa wa Dar es salaam?

Eneo lipo jirani na kiwanja Na. 148 ambalo limejengwa nyumba ya makazi ya kudumu ya mtu binafsi. Kamati ilishauri kuwa Halmashauri iwasilishe taarifa kuhusu mwendelezaji huyo na kama ni mvamizi apelekewe notisi na kumtaka aondoe jengo hilo. Naomba kujua kama taarifa ya Halmashauri ilishawasilishwa au la.
Nyuma ya jengo la RUBADA na Kanisa la KKKT na Anglikana. Eneo hilo limejengwa shule ya msingi Ubungo Plaza kwa mpango wa MMEM. Kamati ilishauri kuwa eneo lililobakia litumike kwa matumizi michezo na burudani na si vinginevyo. Je, hatua zipi zimechukuliwa?

Na viwanja vingine vya kata zingine za jimbo la Ubungo kwa kadiri ya ripoti ya Kamati/Tume iliyoundwa na Mkoa wa Dar es salaam na taarifa za nyingine.

Kwa kuwa maeneo hayo yalitengwa kwa mujibu wa sheria (Public Recreation Grounds Cap. 320) na kwa kuwa maeneo hayo ni muhimu kwa ajili ya matumzi ya umma naomba kutoa hoja kwa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kupitisha maazimio mahususi kuhusu viwanja husika kwa lengo la kulinda sheria na hazi za wananchi kuhusu ardhi.

Aidha naomba kutoa hoja kwa baraza la madiwani wa Manispaa ya Kinondoni lielezwe hatua za kisheria na kiutawala ambazo zimechukuliwa kwa wahusika kutokana na uvamizi na/au uuzwaji huo.

Naomba pia kutoa hoja kwa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kupitisha maazimio yatakayowezesha vitendo vya namna hiyo kutojirudia ikiwemo kwa kupitia kata zingine na kuchukua hatua stahili.

Kadhalika naomba kutoa hoja baraza la madiwani wa Manispaa ya Kinondoni lipitishe azimio kwamba mamlaka husika ziweze kufanya ziara ya kutembelea viwanja husika ili kuweza kuchukua hatua na kuhakikisha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati husika.
Naomba kutoa hoja kwamba baraza la madiwani lipitishe azimio la kutaka kuletwa mapendekezo ya mpango kabambe wa matumizi endelevu ya viwanja vya umma katika Manispaa ya Kinondoni.

Naomba kutoa hoja;John Mnyika (Mb)
Mjumbe wa Baraza la Madiwani
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
19 Machi 2011

3 comments:

mwananchi said...

Ndugu diwani na mbunge, naomba ufuatilie suala hili kwa makini na mrejesho ufanyike mara kwa mara kuhusiana na sakata hili. Sina hakika eneo la mwenge kijijini ambalo maeneo ya wazi nayo yamevamiwa utalishughulikia vipi ukizingatia kuwa lipo chini ya ushirika wa mwenge kijijini

Anonymous said...

KAma mwanzo na sasa na siku zote.
Ukweli huwa unasimama. Mungu anapenda wasema kweli. Tupo pamoja!!

Anonymous said...

Kwa kweli naona Mungu kajibu maombi yetu, inaumiza sana kuona viwanja vya wazi vya umma kuuzwa na watoto kukosa sehemu ya kuchezea, mfano hapa sinza 'C' kiwanja cha wazi cha umma kumejengwa kiwanda kidogo cha uselemala. Yaan full kelele na vumbi na viongozi wa mtaa wanaangalia tu.Mnyika kwa kweli lifanyie kazi hili. by H