Sunday, June 19, 2011

TAMKO JUU YA KAULI ZA WAZIRI MKUU PINDA KUHUSU POSHO

TAMKO LA KATIBU WA WABUNGE WA CHADEMA JUU YA KAULI ZA WAZIRI MKUU PINDA KUHUSU POSHO

Katibu wa Wabunge wa CHADEMA nimeshangazwa na kauli za Waziri Mkuu Mizengo Pinda alizozitoa bungeni tarehe 16 Juni 2011 wakati akijibu maswali ya papo kwa papo.
Waziri Mkuu Pinda ametoa kauli ya kuhalalisha posho za wabunge kwa hoja kwamba zinahitajika kwa ajili ya kuwapa watu wanaowaomba fedha nje ya ukumbi wa Bunge.
Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuifuta kauli yake, kwani inapotosha majukumu ya Bunge na Wabunge wake yaliyotajwa kwenye ibara ya 63 (2) na (3) ya kuisimamia serikali, kuwakilisha wananchi, kupitisha mipango na kutunga sheria. Kauli ya Waziri Mkuu Pinda inahamasisha siasa za fadhila (patronage) katika taifa, ambazo ndizo zimetumika na CCM kupandikiza mbegu ya rushwa katika uchaguzi kwa kisingizio cha takrima.

Kadhalika kauli ya Waziri Mkuu Pinda inadhihirisha hana dhamira ya dhati ya kutekeleza kwa ukamilifu na kwa haraka maagizo ya Rais Kikwete kinyume na Katiba Ibara ya 52 (3), ambayo inamtaka atekeleze au asababishe utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe.

Aidha, Waziri Mkuu Pinda ametoa kauli bungeni kuwa wabunge wengi wa CHADEMA wanazimezea mate posho hizo na kujaribu kuonyesha kwa umma kwamba hoja ya kutaka mabadiliko katika mfumo wa posho nchini ni ya wabunge wachache ndani ya CHADEMA.
Katibu wa Wabunge wa CHADEMA namtaka Waziri Mkuu Pinda aelewe kwamba suala la kutaka mabadiliko ya mfumo wa posho katika nchi yetu ni la pamoja kwa CHADEMA na natoa mwito aisome ilani ya CHADEMA kupata msingi wa msimamo huo.

Kama sehemu ya kuimarisha uchumi kwa kuondoa ubadhirifu Ilani ya CHADEMA ya Agosti 2010 kifungu cha 5.5.1 kipengele cha 5 imeeleza bayana kwa mifano kwamba serikali ya CCM imekuwa ikitenga kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya posho. Mfano katika mwaka 2008/2009 Serikali ya CCM ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 509 (Zaidi ya nusu trilioni kwa ajili ya posho mbalimbali) ambayo ilikuwa sawa na malipo ya mishahara ya mwaka mzima ya walimu 109,000. Aidha ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 ilieleza bayana kwamba Ofisi ya Rais Jakaya Kikwete ndiyo iliyoongoza kwa kujigawia posho ya zaidi ya Bilioni 148 kwa mwaka 2009/2010 huku Bunge likijagiwia Bilioni 36 katika kipindi hicho hicho.

Kipengele cha 6 kwenye Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 kimeeleza bayana kwamba Serikali ya CHADEMA itaweka utaratibu ili semina, warsha, mafunzo na vikao katika taasisi mbalimbali za umma zifanyike kama sehemu ya kazi bila uwepo wa posho maalum za vikao kwa siku (Sitting Allowances).

Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 imefafanua kuwa lengo ni kupunguza posho hizi kwa zaidi ya asilimia 80 zikiendana na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma kuendana na ujuzi, nafasi, wajibu ili wafanyakazi walipwe kwa haki kwa kile wanachofanya kwa haki. Uamuzi huu ungewezesha pia kuelekeza fedha zinazobaki katika miradi ya maendeleo.

Huo ndio msimamo ambao viongozi wa CHADEMA kwa umoja wetu ikiwemo wagombea wa nafasi mbalimbali tuliunadi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kwa wabunge walioshinda wa majimbo na viti maalum ndio msimamo watakaoendelea kuusimamia ndani ya Bunge huku Chama kikihamasisha miongoni mwa jamii kwa kuunganisha nguvu ya umma. Suala hilo pia limejadiliwa katika vikao vya kamati ya wabunge ya chama na kuzingatiwa katika Bajeti Mbadala (Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012) ambayo imeeleza bayana namna ambavyo kiwango cha posho kimepanda kwenye bajeti ya serikali kwa ari, nguvu na kasi zaidi na kufikia takrikabani trilioni moja.

Nilitarajia kwamba baada ya Serikali ya CCM kuchukua msimamo huo na kuuingiza kwenye Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano 2011/2012-2015/2016 uliosainiwa na Rais Jakaya Kikwete tarehe 7 Juni 2011 ambao kwenye ukarasa wa 17 unatamka bayana kwamba posho za vikao na nyinginezo zinapaswa kufutwa au kuwianishwa; Waziri Mkuu angeipongeza CHADEMA na wabunge wake kwa msimamo wao badala ya kubeza na kupotosha.

Kinyume chake na siku chache baada ya kauli ya Waziri Mkuu; Serikali ambayo yeye ndiye kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 52 (2) imefanya mkakati wa kupenyeza habari ya kuupotosha umma kwa kutumia orodha na saini za wabunge za mahudhurio ya vikao sanjari na habari ya kupindisha kutaka kuupotosha umma kwamba wabunge wa CHADEMA hawana dhamira ya dhati ya kutaka posho za vikao (Sitting Allowance) ziondolewe.
Ni vizuri Waziri Mkuu Pinda na watu wanaotumika ndani ya Serikali kutaka kuichafua CHADEMA na wabunge wake waelewe kwamba ambacho wabunge wa CHADEMA tunataka kwa umoja wetu ni kurekebishwa kwa mfumo mzima wa posho kama ambavyo tumeelezea katika Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 na Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Hali ya Uchumi na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

Katika kushinikiza msimamo huo kutekelezwa wabunge kwa nafsi na nafasi zao wanauhuru wa kutumia njia mbalimbali kufikia lengo hili la pamoja. Wapo walioandika barua kutaka posho zao zielekezwe katika taasisi za kimaendeleo na wapo ambao wakizielekeza fedha hizo kuchangia shughuli za maendeleo katika majimbo yao kuanzia Novemba mwaka 2010. Hata hivyo, katika kuendeleza msimamo wa pamoja ikiwa Waziri Mkuu hatafuta kauli yake ama Ofisi ya Bunge kutoa ufafanuzi ikiwemo hatua mahususi kuelezwa bungeni kuhusu serikali itakavyoanza kufanya mabadiliko katika mfumo wa posho katika utumishi wa umma wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti; tutakaa kikao cha Kamati ya Wabunge wa chama (Party Caucus) kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kifungu 109 na 110 kama sehemu ya kuweka msimamo wa pamoja kuhusu bajeti na kueleza hatua za ziada ambazo tutachukua kuhusu posho hizo za vikao (Sitting Allowance) na ubadhirifu mwingine katika serikali.

Aidha nachukua fursa hii kumtaarifu Waziri Mkuu Pinda kwamba posho ya kikao (Sitting Allowance) haijatajwa kwenye katiba wala kwenye sheria hivyo ni suala la kiutendaji ambalo yeye kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni anapaswa kuwasiliana na Spika kuharakisha taratibu za kuziondoa bila kuleta visingizio vya kikakatiba na kisheria.

Napenda umma wa watanzania ufahamu kwamba Katiba Ibara ya 73 imetamka tu kuwa wabunge watalipwa mishahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na bunge lakini kifungu hicho hakitaji aina ya posho wala viwango.
Aidha Sheria ya Utawala wa Bunge (National Assembly Administration Act) ya mwaka 2008 kifungu cha 19 kinataja aina ya posho ambazo zinaweza kutolewa kwa wabunge kama ambavyo Rais ataeleza kwa maandishi. Katika kipenge (d) sheria imetaja orodha (i) mpaka (iii) ya posho ambazo wabunge wanastahili kulipwa za usafiri, kujikimu na wasaidizi; katika orodha hiyo hakuna Posho ya Kikao (Sitting Allowance) ambayo inalipwa hivi sasa kwa kuwekwa kwenye akaunti za wabunge moja kwa moja na CHADEMA imetoa tamko la kutaka ifutwe mara moja kama sehemu ya mchakato wa kubadili mfumo mzima wa malipo ya posho kwa watumishi wa umma.

Kifungu 19 (d) (iv) kimempa mamlaka Rais ya kutoa posho zingine kwa wabunge kwa kadiri atakavyoelekeza; kifungu ambacho kimefanya utolewe waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais wa tarehe 25 Oktoba 2010 wenye kumbukumbu na. CAB111/338/01/83 masharti ya kazi ya mbunge ambao umeeleza viwango vya posho mbalimbali ikiwemo kutoa posho ya vikao (Sitting Allowance).

Hivyo, kwa kuwa Rais Kikwete amesaini tarehe 7 Juni 2011 Mpango wa Miaka Mitano wenye kulenga kuondoa posho hizo Rais Kikwete anapaswa kufuta posho hizo haraka kwa kutoa waraka badala ya kusubiri mabadiliko ya kisheria na kikatiba kama Pinda alivyoeleza bungeni. Aidha, hatua hiyo iende sambamba Rais Kikwete kuonyesha mfano kwa kupunguza gharama za posho mbalimbali za vikao na safari za nje ambazo zinatumiwa na ikulu.

Imetolewa tarehe 19 Juni 2011 na:

John Mnyika
Katibu wa Wabunge wa CHADEMA
Na Kambi Rasmi ya Upinzani

No comments: