Saturday, June 25, 2011

Mgawo wa kizembe wa umeme; serikali iwajibike

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja anapaswa kuwajibika na kutoa kauli kwa umma na bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 49 ya Bunge kuhusu mgawo mkubwa wa umeme uliotangazwa na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuwa utaikumbuka mikoa 18 inayopata umeme kupitia Gridi ya Taifa.

Aidha kabla ya kusubiria kutoa kauli bungeni Waziri Mkuu anapaswa kuingilia kati kwa haraka kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na TANESCO ili kuharakisha maamuzi ya kupunguza muda wa mgawo unaoendelea hivi sasa.

Hii ni kwa sababu pamoja na kupungua kwa vina vya maji katika baadhi ya mabwawa zinazoelezwa; kwa sehemu kubwa mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa umechangiwa na sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali kuanzia Rais, Waziri Mkuu, Waziri mwenye dhamana na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi.

Maelezo ya kwamba mgawo huu umesababishwa na mitambo ya IPTL kuzalisha MW 10 badala ya MW 100 kutokana na upungufu wa mafuta mazito (HFO) yanatosha kwa serikali kuwajibika kutokana uzembe wenye kulitia hasara taifa kwa sababu suala hili lilikuwa likijulikana kwa miezi mingi bila hatua stahili kuchukuliwa.

Mara kadhaa tumetahadharisha kwenye vikao na hadharani mara kwa mara kuhusu suala hilo lakini inaelekea kuna ombwe na kiuongozi na kimaamuzi katika serikali ambalo linaambatana na hali mbaya ya kifedha ndani ya serikali inayoongozwa na CCM kutokana na fedha nyingi za umma kutumiwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Ikumbukwe kwamba katika mkutano wa pili wa Bunge kikao cha sita tarehe 15 Februari mara baada ya kauli za Mawaziri ambapo Waziri wa Nishati na Madini alitoa kauli ya serikali kuhusu hali ya umeme nchini na utekelezaji wa miradi ya umeme katika kipindi kifupi na cha kati nilitoa hoja ya dharura kwa mujibu wa kanuni 55 (3) (e) na kanuni ya 47 ili bunge lijadili jambo la dharura la mgawo wa umeme unaolikumba taifa.

Katika ya hatua za dharura ambazo zingejadiliwa kwa kina ni ufanisi katika matumizi ya mitambo ya IPTL ikiwemo kuboresha taratibu za upatikanaji wa mafuta mazito, kuharakisha mchakato wa kupata mitambo ya MW 260; kuharakisha kukamilisha mitambo ya MW 100 Ubungo, MW 60 Mwanza, kuwezesha upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya mitambo na hatua nyingine za dharura; iwapo hoja hiyo ingejadiliwa wakati huo bunge lingepitisha maazimio ya kuwezesha hatua za mapema kuchukuliwa kudhibiti mgawo mkubwa uliolikumba taifa mwezi Mei na unaoendelea kulikabili nchi hivi sasa.
Pamoja na bunge kutojadili suala hilo baadhi ya ushauri wa kurekebisha kasoro zilizoendelea ulitolewa kwa serikali kupitia kamati ya nishati na madini mwezi Februari 2011 hata hivyo kuna mwelekeo wa kutokuwa na uongozi thabiti katika serikali wa kukabiliana na tatizo la mgawo mkubwa wa umeme.

Tarehe 2 Aprili 2011 nilitoa kauli ya kuitaka serikali ieleze maandalizi ambayo yamekwishafanyika mpaka hivi sasa kukabiliana na tatizo la upatikanaji, usafirishaji na uhifadhi wa mafuta mazito (HFO) ambayo yatahitajika kwa kiwango kikubwa katika kuendesha mitambo ya kufua umeme wa dharura ikiwemo IPTL na ya MW 260 kufuatia hotuba ya Rais Kikwete ya Aprili Mosi 2011 akilihutubia taifa ambayo haikuonyesha namna ambavyo serikali imejiandaa ipasavyo kukabiliana na mgawo wa umeme unaolikumba taifa.

Tarehe 22 Mei 2011 wakati taifa likikumbwa na mgawo mkubwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukarabati wa visima vya gesi asilia inayotumika kuendeshea mitambo ya umeme nilitahadharisha kwamba mgawo mwingine mkubwa zaidi unaweza kutokea iwapo hatua zaidi na za haraka hazitachukuliwa kuhusu upatikanaji wa mafuta mazito, gesi asilia na uharakishwaji wa mchakato wa kupata mitambo ya dharura ya MW 260.

Kauli zilizotolewa na Serikali baada ya kumalizika kwa ukarabati wa visima vya gesi kwamba mgawo ulikuwa umemalizika bila ya serikali kuchukua hatua za haraka kuzirekebisha kasoro tulizozieleza ililenga kutoa matumaini hewa kwa wananchi ili kuvuta muda kwa ajili ya kutoa visingizio vingine mwezi Juni kwa matatizo ambayo yalifahamika mapema.

Aidha kutokana na udhaifu wa kiutekelezaji Waziri Mkuu Pinda amekwepa katika Hotuba yake ya Bajeti ya tarehe 24 Juni 2011 kuzungumzia tatizo la mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa badala yake ameeleza tu kwamba nishati ya uhakika itapatikana miaka michache ijayo. Hii ni kwa sababu Waziri Mkuu Pinda ameshindwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi wa MW 100 Ubungo na MW 60 Mwanza ambayo aliiahidi kupitia hotuba yake ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011 na mradi wa MW 200 Kiwira ambayo kama ingetekelezwa kwa wakati kuanzia ilipowekwa kwenye mipango ya serikali mwaka 2009 ingekuwa imekamilika mwanzoni mwa mwaka 2011 na hivyo taifa lisingekuwa na mgawo mkubwa wa umeme na kuingia gharama kubwa za mitambo ya kukodi kama ilivyo sasa.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kutoa majibu wakati wa majumuisho ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo kueleza kwa watanzania yeye kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni sababu za serikali kutokutekeleza kwa wakati mipango ya kulinusuru taifa kutokana upungufu wa umeme unaochangiwa na ukame hali ambayo aliifahamu tangu mwaka 2008 alipoingia madarakani. Ikumbukwe kwamba Waziri Mkuu Pinda aliingia madarakani wakati huo baada ya Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa kujiuzulu kufuatia maamuzi ya kifisadi yaliyofanywa na serikali wakati wa mgawo wa umeme kati ya mwaka 2006 mpaka 2007.

Kupitia kauli bungeni serikali ieleze ukweli kuhusu sababu za mgawo mkubwa wa umeme uliotokea mwezi Mei na unaoendelea hivi sasa na hatua ambazo serikali imechukua kwa waliosababisha hali hiyo. Aidha Serikali ieleze ukweli kwamba Waziri Ngeleja alitoa kauli potofu bungeni tarehe 15 Februari na Rais Kikwete alitoa ahadi hewa kupitia Hotuba yake kwa Taifa tarehe 1 Aprili 2011 kuhusu ukodishwaji wa mitambo ya MW 260 kwa ajili ya umeme wa dharura kuanzia mwezi Julai mwaka 2011. Serikali iwaeleze watanzania ukweli kuwa imeshindwa kutekeleza mpango huo na kueleza hatua mbadala za kurekebisha hali hiyo ili kuepusha mgawo huu ulioanza mwezi Juni kuendelea mpaka mwezi Disemba mwaka 2011 hali ambayo itakuwa ni janga kwa taifa.

Aidha serikali ieleze mikakati mahususi ya muda mfupi ya kushirikiana na sekta binafsi iweke mazingira wezeshi ya kisheria, kikanuni na kibajeti ya kuweka msingi wa utekelezaji wa miradi ya Somangafungu (MW 230), Mnazi Bay (MW 300), Kinyerezi (MW 240), maporomoko ya Ruhudji (MW 358) ili ikamilike kwa haraka zaidi kuliko ilivyopangwa hivi sasa.

Katika kauli hiyo serikali iwaeleze watanzania kupitia bunge mkakati mahususi wa kuwekeza katika kuongeza upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya kuendesha mitambo hiyo ya umeme na pia kama sehemu ya mpango wa nishati mbadala yenye kupunguza gharama za maisha zinazochangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na mzigo mkubwa wa kodi ambao utaendelea hata baada ya serikali kutangaza punguzo dogo la kodi na tozo.

Kwa uchumi na usalama wa nchi serikali ya Tanzania inapaswa kufanya maamuzi mazito na kuwasilisha maombi bungeni ya kutenga kiasi cha Shilingi Bilioni 131 ambacho kinahitajika kama sehemu ya kuchangia asilimia 15 ya mkopo kwa ajili ya mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam na baadaye hadi Tanga. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 ambayo imepitishwa serikali haijatenga kiasi hicho cha fedha hali ambayo itakwamisha utekelezaji wa mradi huo unaohitaji kati ya mwaka mmoja na miaka miwili kuweza kukamilika. Mradi huo usipotekelezwa kwa wakati ipo hatari ya baadaye ya kuwa na mitambo ya umeme ya gesi lakini ikakosekana gesi asilia ya kuiendesha na pia taifa litashindwa kutumia vizuri fursa ya kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kutumia nishati mbadala ambayo inapatikana hapa nchini.

Hatua hizi zinahitaji sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti zenye kuelewa kwamba sekta ya nishati ni roho ya taifa letu kwa sasa na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi uliofanyika katika sekta husika, kufanya mapitio ya mikataba, kuharakisha utekelezaji wa mipango kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi na kwa ujumla KUWAJIBIKA. Kupungua kwa uzalishaji na kuishi gizani miaka 50 baada ya uhuru ndio mafanikio ambayo serikali inayoongozwa na CCM inataka tujivunie! Poleni wananchi, serikali inapaswa kutuomba radhi! Kambi rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, kupitia kwa Msemaji wake Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini itaendelea kupitia Mkutano wa Nne wa Bunge kuifuatilia Serikali iliyoko madarakani kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa maslahi ya umma wa watanzania.

Wenu katika utumishi wa umma;

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
Bungeni, Dodoma-25 Juni 2011

9 comments:

Revolutionery said...

Nimefurahishwa na mtiririko wa hoja katika waraka wako huu. Natoa wito kwa chama (chadema) kuwahamasisha watanzania kuiwajibisha serikali hii ya ccm kwa kusababisha nchi kuwa gizani. Ni hakika kuwa nchi imekosa uongozi thabiti, ni wajibu wetu sasa kuchukua hatua badala ya kulalamika tu.

Naunga mkono juhudi zako katika kuwaelimisha watanzania na kuwatumikia. Usikate tamaa, tuko nawe bega kwa bega kuhakikisha ukombozi wa kweli unapatikana! Peopleeeeeees ............!

Ayoub C Kafyulilo said...
This comment has been removed by the author.
Mussa said...

Sio siri hawa viongozi wa CCM ni waongo sana,tufanye nguvu na wao wapate mgawo,eti hata kama wapo Dom huku majumbani kwao hakuna mgawo,ndo maana hawana uchungu,nao waupate wataobgeza spidi na kujali

Joseph said...

Hivi tatizo la upungufu wa gesi linaanzia wapi? Nilidhani gesi ya songosongo ilikuwa inatosha kuendesha mitambo ya sasa? Kumetokea nini? Gesi ya songo songo imekwisha?

Anonymous said...

well well well! uwepo wetu gizani, labda ni microcosm ya giza lililoko ndani ya nafsi (akili) za wale wanaondelea kuchagua giza (figuratively speaking) na kuuchukia mwanga. Itachukua muda kwa watanzania kung'amua kuwa Kura zao ni hatima yao. Hadi sasa sioni mwanga kwa jinsi watanzania wanavyoendelea kukubali kudanganyika kirahisi.

Anonymous said...

well well well! uwepo wetu gizani, labda ni microcosm ya giza lililoko ndani ya nafsi (akili) za wale wanaondelea kuchagua giza (figuratively speaking) na kuuchukia mwanga. Itachukua muda kwa watanzania kung'amua kuwa Kura zao ni hatima yao. Hadi sasa sioni mwanga kwa jinsi watanzania wanavyoendelea kukubali kudanganyika kirahisi.

Mavere said...

I am just disappointed that Ngeleja is too blind to see that wizara ile ni kubwa kwake

anajidhalilisha tu kuendelea kuwa pale, he needs to go ili kurudisha heshima yake

Anonymous said...

Hili swala la umeme linasikitisha sana.Sidhani kama kweli nchi yetu inatatizo kubwa hivi.
Waziri,unajisikiaje tunapokuwa na mgao usio na kichwa wala mkia?unajisikiaje kuturudisha kusomea vibatari?utajisikia vipi ndugu yako akiwa kwenye chumba cha upasuaji daktari kamchana tu umeme ukatike?unawafikiriaje wajasiriamali wadogo wadogo?maofisi mengi yanatumia mitandao unawaza nini?
UNAJISIKIA JE NCHI KUWA GIZANI WAKATI wa UONGOZI wako?
Maji ndo source pekee ya kutupatia umeme?

Kama shida sio wewe shida nini?na mpango mkakati wako ni upi juu ya swala hili?

UNAJIKIAJE???

Anonymous said...

U really touch ma heart....hv reasonable thinking imekosekana kweli kwa viongozi wetu na hasa sisi watanzania? yaani huu utawala uanatuchukulia for granted !!!! this is too much .JAMANI lets work up it will come a time when is to late even to think u can blink.Ila tuombe sana jamani tunakoelekea siko jamani.