Tuesday, August 21, 2012

Taarifa Fupi kuhusu Kazi za Maendeleo Jimboni Ubungo (AMUA)


UTANGULIZI:
Kwa nyakati mbalimbali kumekuwepo na mijadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu utendaji kazi wangu katika kuwezesha maendeleo Jimboni Ubungo. Mijadala hiyo imeshika kasi jana tarehe 20 Agosti 2012 siku nzima baada ya habari kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti la Tanzania Daima “Mnyika kinara bungeni” ambayo imerejea rekodi za bunge na kuniweka katika orodha ya wachangiaji wa mara kwa mara bungeni.

Napokea kwa unyenyekevu pongezi zilizotolewa na wachangiaji mbalimbali lakini izingatiwe kuwa michango yangu bungeni ni matokeo ya heshima mliyonipa ya kuwawakilisha. Aidha yapo maoni machache ambayo yametoa tafsiri tenge kuhusu kazi ya mbunge na wengine mmetaka nieleze nimefanya kazi gani za maendeleo jimboni Ubungo.

Tarehe kama ya leo 21 Agosti 2005 nilianza mchakato wa kuwa kugombea ubunge nikiwa kwenye chakula na watoto yatima, tarehe kama hiyo mwaka 2010 nilianza kampeni za uchaguzi mitaani Ubungo, tarehe hii hii kwa mwaka huu wa 2012 naomba niitumie kutoa taarifa fupi ya utekelezaji kwa masuala ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2011/2012 uliomalizika tarehe 30 Juni 2012; taarifa ya kina ya utekelezaji nitaitoa nitakapotimiza miaka miwili ya utendaji.

AHADI NILIZOTOA WAKATI WA UCHAGUZI WA MWAKA 2010
Kabla ya kueleza kazi nilizofanya katika kutimiza majukumu ya kibunge katika kuwezesha maendeleo jimboni ni muhimu nikawapa rejea ya ahadi nilizotoa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010 ili kupata msingi  wa kupima utekelezaji.

Wakati wa kampeni nilitoa ahadi chache na kuelekea mwishoni mwa kampeni niliorodhesha ahadi zote na kuziweka kwenye maandishi ikiwa ni mkataba kati ya mbunge na wananchi wa kutumika kama rejea katika kipindi cha miaka mitano ya utumishi 2010 mpaka 2015.

Ahadi hizo ziko katika kipeperushi cha AMUA ambacho tulikisambaza kwenye kaya mbalimbali jimboni wakati wa kampeni, ahadi hizo nilizirudia mara baada ya kuchaguliwa na zinapatikana hapa:  http://mnyika.blogspot.com/2010/11/ujumbe-wa-mbunge-shukrani-twende-kazi.html

UTEKELEZAJI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA NA NUSU
Toka kuapishwa mwezi Novemba 2010 mpaka mwezi Juni 2012 ni takribani mwaka mmoja na na miezi tisa  ya kuwatumikia wananchi wa Ubungo kwa nafasi niliyochaguliwa ya mbunge wa Ubungo; hizi ni baadhi katika orodha ya za maendeleo ambazo nimeshiriki jimboni:

ELIMU:
Akili na vipaji ambavyo kila mwanadamu amejaliwa ndiyo mtaji mkuu wa kujikwamua kimaisha. Katika muktadha huo katika kipindi husika nimesimamia yafuatayo kuwezesha elimu bora:

Mbunge amefuatilia kupitia vikao vya manispaa ya Kinondoni na kupitia ziara jimboni, maswali bungeni ili kuhakikisha ruzuku ya bajeti ya elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, inafika na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya elimu na huduma zingine za muhimu katika Jimbo la Ubungo, katika mwaka 2012/2013 nitafuatilia kwa karibu zaidi kasoro zilizobainika katika mwaka 2011/2012 .

Katika kipindi husika mbunge ameendelea kutetea haki na maslahi ya walimu na wanafunzi wakiwemo wa elimu ya juu wa Jimbo la Ubungo. Aidha, nimeshiriki katika kuwezesha uamuzi wa kuhamisha fedha katika mafungu mengine yasiyokuwa ya lazima kuelekeza katika matengenezo ya madawati kwa shule za msingi na sekondari ambapo zaidi ya madawati 7,000 yamesambazwa katika Jimbo la Ubungo kutoka Manispaa ya Kinondoni, Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) na kutoka Sekta Binafsi. Kwa ushirikiano na madiwani tumefuatilia kuhakikisha mgawo wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule za msingi na sekondari katika kata mbalimbali kutoka katika Manispaa ya Kinondoni na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF), orodha ya shule na viwango vya fedha vilivyotumika inaweza kupatikana katika Ofisi ya Mbunge. 

Mbunge amependekeza sehemu ya fedha za mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo (CDCF) kutumika kutoa elimu maalum ya kuwawezesha wananchi kujua haki zao, fursa zilizopo na namna ya kujiendeleza,   haswa kwa akina mama, vijana na walemavu. Mfano; haki za mirathi kwa wajane na kukuza vipaji kwa vijana. Hata hivyo, utekelezaji wa kazi hii haukuwezekana kwa kutumia CDCF kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kutokana na utata kuhusu tafsiri ya shughuli za kuchochea maendeleo zinazoweza kutengewa fedha kutoka kwenye mfuko, hivyo shughuli hiyo itazingatiwa kwa ukamilifu kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 baada ya kibali kupatikana.

Ili kuziba pengo nje ya CDCF katika mwaka 2011/2012 kupitia ofisi ya mbunge Ubungo na Asasi ya Maendeleo Ubungo (UDI) tumefanya programu ya “Toa Kitabu Kisomwe” na pia kuunganisha vijana na wanawake na elimu maalum kupitia taasisi zingine.

Mbunge amechangia asilimia 20 (20%) ya mshahara wake kwa mwezi kwenye masuala mbalimbali ya elimu, orodha ya baadhi ya michango kwa shughuli za elimu kwa wanafunzi na walimu wa msingi, sekondari na vyuo inaweza kurejewa katika Ofisi ya Mbunge (majina ya waliopewa michango yamehifadhiwa kulinda faragha).

Kazi hizi zitapanuliwa zaidi katika mwaka wa fedha 2012/2013 kupitia Mfuko wa Elimu Ubungo tutakaouzindua karibuni.

AJIRA: 
Katika kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa vijana na wanawake kuweza kujiajiri mbunge alifanikiwa kushawishi Manispaa ya Kinondoni kuongeza fedha za mikopo kwa vikundi vya kina mama na vijana ambapo awali zilikuwa zikitengwa milioni 20 tu, na hivyo milioni zaidi ya 200.

Orodha ya vikundi vilivyopatiwa mikopo na mitaji mpaka sasa katika Jimbo la Ubungo inapatikana kwenye Ofisi ya Mbunge. Aidha, mbunge ametetea wafanyabiashara wadogo kuendelea kutengewa maeneo ya biashara na katika mwaka 2011/2012 amewezesha kamati maalum inayohusisha wafanyabiashara na Manispaa kuundwa kwa ajili ya kuwezesha wafanyabiashara wa Ubungo kupatiwa maeneo katika masoko yaliyotengwa. Katika mwaka 2012/2013 hatua zitaendelea kuchukuliwa kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo ambao hawajapata maeneo mpaka sasa.

Mbunge amefanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha nguo cha Urafiki ili kuzungumza na wafanyakazi na menejimenti katika kuisimamia serikali kushughulikia matatizo yaliyojitokeza katika kiwanda na kuathiri ajira na ujira bora. Matokeo ya ziara ya mbunge na ufuatiliaji bungeni yamefanya kiwanda hicho kutembelewa pia na kamati ya bunge na mawaziri husika ambapo hatua zimeanza kuchukuliwa, katika mwaka wa fedha 2012/2013. Mbunge ataendelea kufuatilia kwa karibu matatizo yanayoendelea kuhusu ufisadi na uwekezaji katika kiwanda husika.

Aidha, mbunge amefuatilia pia masuala ya ajira katika viwanda vilivyofunguliwa kwenye maeneo ya uwekezaji wa kiuchumi (EPZ/SEZ) yaliyopo katika jimbo la Ubungo ikiwemo kutaka kutengwa kwa maeneo maalum ya wawekezaji wadogo.

Katika kupanua wigo wa ajira mbunge amefuatilia pia kuhusu viwanda vingine vilivyobinafsishwa au kuuzwa miaka ya nyuma katika Jimbo la Ubungo mathalani Ubungo Garments;  Ubungo Spinning Mill;  Polysacks Ltd; Tanzania Sewing Thread; Coastal Diaries (Maziwa) na  Kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI); na hatimaye serikali imemjibu kuwa waraka utawasilishwa kwenye baraza la mawaziri ili kurejesha viwanda vilivyodidimizwa kinyume cha masharti ya mikataba. Katika utekelezaji wa hatua hiyo, mbunge amependekeza kuwa miongoni mwa maeneo ya viwanda yatakayorejeshwa kutengwe eneo maalum kwa ajili ya wenye viwanda vidogo vidogo katika jimbo la Ubungo ili kupanua wigo wa ajira hususan kwa vijana katika mwaka wa fedha 2012/2013.

Mbunge ameunga mkono jimboni na ndani ya bunge madai ya ujira bora na stahili za wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi kama walimu, madaktari/manesi, polisi, madereva nk. Hata baada ya nyongeza ndogo ya mishahara iliyopatikana kufuatia shinikizo la migomo kutoka vyama vya wafanyakazi, mbunge ataendelea kuungana na wafanyakazi na wabunge wengine katika kutaka kuboreshwa kwa maslahi ya wafanyakazi na mazingira ya utoaji huduma hususan katika sekta za elimu, afya, usalama na mahakama. Katika ya masuala ambayo aliyapata kipaumbele katika mwaka wa fedha 2011/2012 ni nyongeza ya posho ya lishe (rationing allowance) kwa askari polisi kutoka laki moja mpaka laki moja unusu suala ambalo serikali imelitekeleza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013.

MIUNDO MBINU:
Msimamo wangu katika kipindi chote umekuwa kwamba pamoja kuunga mkono uwekezaji kwenye upanuzi wa barabara kuu, ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa fly overs, miradi hii kwa ujumla wake iliyotengewa zaidi ya bilioni 240 inachukua muda wa kati na muda mrefu hivyo kukamilika kwake ni mpaka mwaka 2015 au zaidi. Hivyo ili kupunguza msongamano katika barabara kuu ya Morogoro, pamoja na mbinu zingine mbunge amekuwa mstari wa mbele kutaka barabara za pembezoni zijengwe kwa haraka; hatimaye baada ya ufuatiliaji wa mara kwa mara kupitia ziara jimboni, vikao vya manispaa, vikao vya bodi ya barabara, ziara jimboni, mawasiliano kwa barua na mamlaka husika na kuhoji bungeni Serikali imekubaliana na mapendekezo tuliyowasilisha hivyo maamuzi yamefikiwa kuwa barabara husika zihudumiwe na Serikali kuu (TANROADS) badala ya Manispaa.

Jumla ya shilingi bilioni 10.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara zifuatazo:  Mbezi Luis kupitia Goba mpaka Mbezi Tangi Bovu; Mbezi kwa Yusuph- Msakuzi- Mpiji Magohe mpaka Tegeta/Bunju; Mbezi-Malambamawili-Kinyerezi, Kimara-Mavurunza-Bonyokwa; Ubungo Maziwa-External, Kimara-Kilungule-Makoka-Makuburi, Kimara-Matosa-Mbezi; Ubungo-Msewe-Chuo Kikuu na nyingine katika maeneo mengine.

Katika mwaka wa fedha 2012/2013 Mbunge ataendelea kuisimamia serikali ili itenge bilioni 100 kujenga kwa kiwango cha lami barabara tajwa za pembezoni za kupunguza msongamano haraka zaidi na pia kuboresha usafiri wa maeneo ya pembezoni kwa kuwa baadhi ya barabara hizo zilitengenezwa kwa kiwango cha changarawe kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 lakini zimeharibika tena baada ya mvua zilizonyesha katika jiji la Dar es salaam.

Katika mwaka wa fedha 2011/2012 tumefuatilia madaraja mbalimbali kujengwa ikiwemo Daraja Golani, Msewe, Matosa nk pia kupitia mfuko wa maendeleo ya Jimbo (CDCF) vivuko kwa watembea kwa miguu vimejengwa Makurumla na Msigani; orodha zaidi ya matengenezo ya barabara yaliyofanyika inaweza kurejewa katika Ofisi ya Mbunge.

Kufuatia ufuatiliaji wa karibu kwa njia mbalimbali hatua imechukuliwa ya kupeleka umeme katika eneo la Goba Matosa (hata hivyo bado kuna malalamiko ya eneo lilirukwa la Mgeni Chongo) ambalo tunaendelea kufuatilia.

Aidha, miradi iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu ya kupeleka umeme katika miradi ya maji ya King’ongo na Kilungule inaendelea kutekelezwa kwa haraka zaidi. Mbunge amefuatilia mara kwa mara ahadi ya Rais ya kupunguzwa kwa gharama za umeme na hatimaye ahadi imetolewa ya utekelezaji kuanza kuanzia Januari 2013, pia kanuni za Februari 2011 zimetungwa kuhusu kurejeshwa kwa gharama kwa wateja wanaolazimika kuvuta umeme zaidi ya umbali wa kawaida.

Katika mwaka 2012/2013 mbunge ataendelea kuisimamia serikali kurekebisha kanuni hizo kwa kuwa zina vifungu visivyotekelezeka na kutaka pia gharama za nguzo na nyinginezo ziwekwe kwenye bili ya mteja kama umeme uliolipiwa kabla. Orodha ya maeneo mengine katika Jimbo la Ubungo ambayo ufuatiliaji umefanyika kuhusu kusambaziwa umeme inapatikana katika Ofisi ya Mbunge.

MAJI:
Katika kufuatilia masuala ya maji nilianza kwa kufanya Kongamano la Maji katika Jimbo la Ubungo mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka husika na wadau wengine katika kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi.

Hatua nyingine zote nilizochukua baada ya hapo zilikuwa ni za ufuatiliaji kuwezesha utekelezaji wa haraka. Nikiri kwamba katika hatua za awali ushirikiano kutoka DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji ulikuwa mdogo kwa kiwango cha kuamua kuwaunganisha wananchi kupitia ‘maandamano ya maji’ kwenda DAWASCO. Toka wakati huo ushirikiano umeongezeka kwa upande wa DAWASCO ambapo nimeshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya kutembelea maeneo yenye matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha baadhi ya maeneo kuanza kutoka maji.

Pia, wakati wa hatua hizo nimewaonyesha DAWASCO biashara haramu ya maji iliyokuwa ikiendelea na baadhi ya maeneo wamechukua hatua ikiwemo kwa watendaji wao. Hata hivyo, udhaifu wa kimfumo uliopo ni mkubwa kuliko hatua ambazo zimeweza kuchukuliwa mpaka sasa. Katika mazingira hayo nilianza pia kutaka hatua za DAWASA na tayari nao nimefanya nao ziara ya kikazi kwenye vyanzo vya maji pamoja na matenki ya maji, na kutaka hatua za haraka za ushirikiano kati ya DAWASA na DAWASCO.

Kwa maana ya miradi ya muda mrefu ya mwaka 2013/2014 kumetengwa fedha kuanzia mwaka 2012/2013 zaidi ya bilioni 200 kutokana na fedha za MCC na Mkopo wa India kwa ajili ya upanuzi wa vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini, ujenzi wa Bwawa la Kidunda na ujenzi wa mabomba mengine miradi ambayo itagusa wananchi wa Ubungo. Hata hivyo, hatua hizi za muda mrefu hazileti matumaini bila hatua za haraka ambazo zilipaswa kuchukuliwa katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Katika kuwezesha hatua za haraka kwa mwaka wa fedha 2011/2012 nilifuatilia ratiba ya mgawo wa maji kuweza kutolewa kwa mbunge na kwa ngazi za kata na mitaa na kufuatiliwa ili mgawo uwezeshe kuheshimiwa bila ya upendeleo wa baadhi ya maeneo au hujuma kwa ajili ya kuwezesha biashara haramu ya maji. Ofisi ya mbunge wakati wote imetaka kupatiwa taarifa pale mamlaka husika au ngazi tajwa zinaposhindwa kufuatilia ratiba husika ili kuweza kuingilia kati. Kuanza kuweka miundombinu ya maji katika maeneo yaliyorukwa kwenye awamu ya kwanza ya uwekaji wa mabomba, tayari utekelezaji umeshaanza katika maeneo ya Mbezi na maeneo mengine utafanyika kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2013 kwa mujibu wa ahadi zilizotolewa na DAWASCO/DAWASA kwa mbunge.

Katika kutekeleza ahadi ya kuhamasisha ujenzi wa visima kwenye maeneo ambayo hayafikiki kirahisi na mtandao wa maji ya bomba kama suluhisho la muda, huku tukifuatilia ufumbuzi wa kudumu katika maeneo hayo, mbunge amefuatilia uchimbaji wa visima uliokuwa umesimama katika maeneo ya Mavurunza/Bonyokwa, Kilungule na King’ongo kwa kwenda maeneo husika, kuziandikia mamlaka zinazohusika na kuhoji kwenye vikao vya manispaa, bungeni na kufanya ziara za ukaguzi wa maendeleo ya miradi.

Uzinduzi kwa miradi ya Mburahati ulifanyika mwanzoni mwa mwaka 2011 na hatimaye sasa uzinduzi wa maeneo yaliyotajwa utafanyika katika mwaka huu wa 2012 kwa kuratibiwa na DAWASA na Wizara ya Maji.

Aidha, uchimbaji wa visima kama hivyo unaendelea katika maeneo ya Saranga na Malambamawili. Aidha, kupitia miradi ya Manispaa ikiwemo mradi unaofadhiliwa na benki ya dunia mbunge amefuatilia uchimbaji katika maeneo ya Mpiji Magohe, Msakuzi, Makoka na Msumi ambao unasuasua kutokana na udhaifu wa kiutendaji.

Mbunge ameunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau wengine wa maendeleo Jimboni Ubungo katika masuala ya maji hususani Shirika la Kibelgiji (BTC) katika maeneo ya Kwembe na Kibamba na amewasiliana na DAWASA/DAWASCO kwa ajili ya hatua za kusaidia miradi husika na TANESCO kwa upande wa kuweka transfoma yenye uwezo mkubwa zaidi ili kuwezesha pampu za maji kwenye maeneo husika ziweze kufungwa. Orodha ya maeneo mengine yaliyochimbwa visima vidogo ipo katika Ofisi ya Mbunge.

Mbunge amefanikiwa kufanya suala la maji kuwa moja ya masuala yanayojadiliwa mara kwa mara kwenye vikao vya Manispaa ya Kinondoni hali ambayo haikuwepo kabla. Aidha alipendeza na hatimaye ukafanyika ufuatiliaji wa miradi iliyo chini ya jamii au mamlaka za ngazi ya chini iliyokwama kwa muda mrefu na hivyo kukosesha wananchi maji katika maeneo mbalimbali ambayo hayapewi huduma ya moja kwa moja na DAWASA/DAWASCO. Kati ya miradi hiyo baadhi imefufuliwa kama wa Msewe Golani na mingi inaendelea kusuasua ikiwemo ya kata ya Goba. Mbunge amependekeza kwa DAWASA kwamba maeneo ambayo hayakuwa yakihudumiwa na DAWASCO ikiwemo ya kata ya Goba yachukuliwe moja kwa moja na mamlaka husika kwa kuwa kutokana na ongezeko la watu maeneo hayo hayawezi kuhudumiwa kwa ufanisi na kamati za maji kama ilivyokuwa miaka ya zamani.

Mbunge amefuatilia pia masuala ya bei na ubora wa maji na kuitaka bei ya maji inayotozwa kwenye Viosk inaendana na viwango vilivyopangwa na mamlaka husika (EWURA), kufuatia hatua hizo operesheni zimefanyika katika maeneo ambayo yanatoza maji kinyume na bei iliyotangazwa na DAWASCO imeingia mikataba na waendeshaji wa vioski husika kuhusu bei elekezi. Hata hivyo, changamoto imeendelea kuwa ni usimamizi wa utawala wa sheria katika kuhakikisha bei inayotozwa ni ile inayopaswa kutoswa kwa mujibu wa maagizo ya EWURA. Katika kipindi husika mbunge ametaka pia EWURA itoe bei elekezi kwa upande wa maji katika jiji la Dar es salaam kwa upande wa sekta binafsi ili kudhibiti pia biashara holela ya maji ya kwenye malori. Katika mwaka wa fedha 2011/2012 EWURA iliahidi kutoa kanuni za kudhibiti biashara husika hatua ambayo mpaka sasa haijachukuliwa, suala ambalo mbunge atalifuatilia katika mwaka wa fedha 2012/2013.

UWAJIBIKAJI:
Mbunge amekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ufisadi na matumizi mabaya ya fedha ngazi mbalimbali ili kuchangia katika  kuhakikisha fedha nyingi zinazopatikana kila mwaka zinatumika kuwahudumia wananchi, ikiwemo kwa kutaka kushughulikiwa kwa mapungufu yaliyoanishwa na wakaguzi wa hesabu katika vipindi vilivyopita. Mathalani mbunge amefuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Ukaguzi Maalum (Special Audit) ya Kituo cha Mabasi cha Ubungo uliofanyika mwaka 2009 lakini utekelezaji wa matokeo ulikuwa ukisuasua. Alifanya hivyo kupitia bungeni na katika vikao vya halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na hatimaye baadhi ya mapendekezo yametekelezwa ikiwemo kumwondoa mkandarasi aliyekuwa akikusanya mapato chini ya kiwango; aidha mbunge ataendelea kufuatilia mapendekezo mengine kuhusu mikataba mibovu iliyoingiwa katika kituo husika.

Mbunge amefanya hivyo vile vile kuhusu vitega uchumi vingine vya Jiji la Dar es salaam ikiwemo Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA). Aidha, kwa kushirikiana na madiwani amefuatilia pia miradi hewa au ya chini ya kiwango iliyofanyika katika miundombinu, elimu na maji na hatua mbalimbali zimechukuliwa kama zinavyoelezwa katika Taarifa za Ofisi ya Mbunge.

Mbunge kupitia uwakilishi bungeni na kupitia hatua zingine nje ya bunge amezifuatilia mamlaka za serikali kuhusu masuala mbalimbali yanayowagusa wananchi wa Ubungo, mathalani EWURA katika nishati/mafuta, SUMATRA katika usafiri na TANESCO katika umeme.

Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge atafanya ziara za kikazi pamoja na mamlaka husika katika maeneo mbalimbali yenye kero ili kuziwezesha kuendelea kuchukua hatua zaidi kuhusu maeneo hayo kwa ajili ya kuchangia katika maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.

Mbunge amefanya mikutano na wananchi katika kata zote 14 za Jimbo la Ubungo kwenye maeneo mbalimbali ya kiserikali na ya kichama kwa ajili ya kutimiza wajibu wa uwakilishi kabla na baada ya vikao vya bunge.

Aidha mbunge ameshiriki katika mikutano ya wakazi ya masuala ya maendeleo jimboni kama ambavyo imetajwa katika Taarifa ya Utendaji. Mbunge amewezesha ofisi ya mbunge kuwa vitendea kazi pamoja na wasaidizi wawili wakati wote baada ya kukwama kupata vifaa kutoka kwenye mfumo wa kawaida wa kiserikali.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2011/2012 maombi ya mbunge kupata ofisi ya kutumia jimboni kutoka kwenye majengo ya manispaa au ya wilaya yalikataliwa na katika mwaka 2012/2013 mbunge ataweka mkazo katika kufuatilia eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya mbunge.

Aidha, mbunge amewajibika katika kuisimamia serikali bungeni na kushiriki katika kutunga sheria. Rejea katika ofisi ya Mbunge kuhusu kazi za mbunge bungeni inaeleza masuala ambayo mbunge ameisimamia serikali bungeni, hatua zilizochukuliwa na serikali kupitia mchango wake na pia sheria ambazo amewasilisha majedwali ya marekebisho katika vifungu mbalimbali vilivyokubaliwa na vilivyokataliwa.

USALAMA:
Mbunge amechangia katika harambee ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Mavurunza ambapo vifaa vya awali vilichangiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) lakini pia fedha taslimu zilichangwa na mbunge kutoka mfuko wake binafsi. Aidha, kupitia CDCF mbunge amechangia pia kwenye ujenzi wa Kituo kidogo cha Polisi Golani Msewe na pia kituo cha Polisi Kata ya Sinza.

Pia, mbunge ameanza ufuatiliaji wa ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kimara katika eneo lenye nafasi tofauti na eneo la sasa la barabarani la Mbezi kwa Yusuph; kufuatia ufuatiliaji wa mbunge tayari Wizara ya Mambo ya Ndani imeiandikia barua Manispaa ya Kinondoni kuomba eneo.

Kadhalika, mbunge amefuatilia kuhusu eneo la ujenzi wa kituo cha Polisi kata ya Goba ambapo kwa mujibu wa taarifa toka ngazi ya kata eneo limekwishapatikana. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataweka kipaumbele katika kazi ambazo zilianza kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 ili ziweze kukamilika.

Mbunge ameshirikiana na polisi na viongozi wa kata/mitaa kufanya harambee kuhakikisha doria inakuwepo ili kupunguza vitendo vya wizi, ukabaji na ujambazi hususani kwenye maeneo yenye vitendo vingi vya uhalifu mathalani ya Kimara B kupitia ulinzi shirikishi na polisi jamii.

Aidha, ili kuwe na mfumo endelevu wa kuhudumia vikundi vya ulinzi shirikishi mbunge alipendekeza kwamba masuala ya ulinzi na usalama kuwa sehemu ya vipaumbele vya maendeleo katika mapato ya ndani ya Manispaa kama ilivyo kwa sekta za elimu, afya, barabara nk. Kwa usimamizi wa Meya pendekezo hilo liliingizwa kwenye baraza la madawani na kutakiwa kutekelezwa kupitia fedha zinazobaki katika kata kutokana na ufanisi katika makusanyo ya ndani ili kuimarisha ulinzi na usalama.

AFYA:
Mbunge aliguswa na kasi ya kupungua kwa fedha za wahisani katika bajeti ya afya kwa masuala ya matibabu kwa wanaoishi na UKIMWI/VVU, Wazee, Walemavu na wagonjwa wa kifua kikuu, hivyo pamoja na kuhoji bungeni na kutaka nyongeza ya bajeti kwenye Wizara ya Afya amechukua hatua jimboni kwenye ngazi ya Manispaa kwa kupendekeza kiwango cha fedha toka vyanzo vya ndani kuongezwa hatua ambayo imeanza kuchukuliwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2012/2013.

Kwa ajili ya afya mazingira mbunge alipendekeza kwamba tathmini ifanyike kuhusu mfumo mzima wa uzoaji taka katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo na Manispaa ya Kinondoni kwa ujumla kutokana na kukithiri kwa uchafu katika maeneo mbalimbali. Kufuatia pendekezo hilo Meya alifanya mkutano na wenyeviti wa mitaa na watendaji wengine ambapo maazimio ya hatua mbalimbali yalifikiwa ambayo yameboresha uzoaji taka katika maeneo machache. Hata hivyo, matatizo ya uchafu yameendelea katika maeneo mengi, hivyo katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataendelea kuisimamia serikali kuu na serikali za mitaa katika kuchukua hatua kubwa zaidi kuhusu udhaifu wa kimfumo ambao ulishababainishwa tayari unaochangia kasi ndogo ya uzoaji taka ngumu na uondoaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

ARDHI:
Mbunge amefuatilia kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wa eneo la Ubungo Maziwa wanapewa fidia stahiki. Aidha, mbunge amefuatilia na hatimaye fidia imeanza kulipwa kwa wananchi eneo la Riverside wanaopaswa kubomolewa kupisha njia mbadala ya kwenda Kibangu.

Hata hivyo, suala la fidia ya ardhi kwa upande wa wananchi wa Kwembe kupitisha ujenzi wa Chuo Kikuu eneo la Mlongazila limekwama kwa Serikali kuchukua msimamo wa kutoa fidia ya maendelezo/mali pekee. Mbunge anaendelea kufuatilia suala hilo katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa kushirikiana na wananchi waliofungua kesi mahakamani wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea. Kwa upande mwingine, kiasi cha shilingi bilioni 10 kimeweza kutengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa Ubungo walio karibu na mitambo ya umeme ambao walikuwa wanadai fidia toka mwaka 2004.

Mbunge amesisitiza kupitia vikao vya Mkoa, halmashauri ya Jiji, Manispaa na bunge kuhusu haja ya serikali kuweka kipaumbele katika kusimamia mpangilio mzuri wa makazi na kuhamasisha upimaji wa viwanja ili wananchi wapate hati na leseni za makazi kwa urahisi na kwa bei nafuu kutokana na matatizo ya gharama kubwa na ucheleweshaji yaliyoko hivi sasa. Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi amemjibu mbunge kuwa wizara itawekwa mfumo ili hati iwe inatolewa kwa haraka katika muda usiozidi miezi sita. Mbunge amefuatilia mradi wa urasimishaji unaofanywa na Ofisi ya Rais (MKURABITA) katika eneo la Kimara Baruti, aidha mbunge ametaka elimu kutolewa kwa wananchi na madiwani na watendaji wengine kuhusu namna fursa za upimaji na urasimamishaji zinavyoweza kutumiwa katika maeneo yao.

Mbunge amefuatilia vile vile taarifa kuhusu mji wa kiungani (Sattellite town) ya Luguruni na maeneo jirani ya mji huo na kubaini kasoro kama zinavyoelezwa katika Taarifa ya Utendaji, aidha Wizara imeahidi kwamba muendelezaji mwenza wa mji huo amepatikana na kwamba kasoro zinazoendelea zitarekebishwa.

Mbunge amefuatilia kupitia hoja binafsi na maswali katika manispaa na bungeni kuhakikisha viwanja vya umma vilivyouzwa kinyume na taratibu na viwanja vya wazi vilivyovamiwa, vinarejeshwa. Mfano: viwanja vya Makurumla, Sinza, Ubungo, Makuburi, Mbezi nk. Kufuatia hatua hizo, sehemu ya viwanja hivyo imejadiliwa kwenye baraza la madiwani la manispaa ya Kinondoni na pia Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi ametembelea kata ya Sinza na kuweka mabango kwa ajili ya wahusika kubomoa. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataendelea kufuatilia kwa karibu ili ubomoaji uanze.

HITIMISHO:
Nihitimishe kwa kurejea msimamo wangu kuhusu kazi za mbunge ambao nimekuwa nao miaka mingi kabla ya kuingia kwenye siasa na niliurudia mwanzoni mwaka 2010 wakati natangaza nia ya kugombea Ubunge:
“Naamini kwamba mbunge (ambaye pia kwa nafasi yake ni diwani katika halmashauri) ana wajibu katika maeneo makuu manne (kwa kadiri ya umuhimu) katika kuwezesha maendeleo Jimboni kwake na kwa taifa kwa ujumla:

Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.

Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.

Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa “mtoa bidhaa na huduma” (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla.

Haiwezekani wakati ambapo makisio yanaonyesha kwamba zaidi ya trilioni mbili (sawa na milioni milioni mbili) zinapotea kila mwaka kupitia misamaha ya kodi, upangaji bei hovyo kwa bidhaa za Tanzania, biashara haramu kati ya Tanzania na nchi za nje au makampuni ya kimataifa halafu wananchi wakubali kupumbazwa na bidhaa za milioni chache zinatolewa na viongozi wa umma walioshindwa kurekebisha hali hii”
, Mwisho wa kunukuu. Msingi wa msimamo huu unaweza kurejewa kwa ukamilifu hapa: http://mnyika.blogspot.com/2010/03/natangaza-rasmi-dhamira-ya-kugombea.html

Hivyo, ufanisi wa ubunge wangu upimwe kwa kuzingatia msimamo huo ambao niliwaeleza wananchi wakati wa uchaguzi hivyo nilichaguliwa ikifahamika wazi kuwa huo ndio wajibu ambao nitautekeleza katika kipindi cha miaka mitano.

Bado naendelea kuamini kwamba jimbo la Ubungo na taifa kwa ujumla tutapiga hatua ya haraka zaidi ya maendeleo kupitia mabadiliko katika mifumo yetu ya mgawanyo wa rasilimali na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na pia kwa kuweka mazingira bora ya kisera, kisheria na kiutendaji wa sekta binafsi.

Tuliyoyafanya mpaka sasa ni sehemu tu katika mahitaji makubwa ya maendeleo kutokana na pengo la miaka 50 ukilinganisha na fursa ambazo taifa letu linazo; hata hivyo naamini miaka mitatu iliyobaki itafanya miaka mitano ya kuisimamia Serikali iliyopo madarakani hivi sasa pamoja na udhaifu wote uliokuwepo kuleta tofauti katika maendeleo majimboni. Ni katika muktadha huo wakati mwingine tunazimika kuwakilisha na kuwasilisha matakwa ya wananchi namna hii: http://www.youtube.com/watch?v=ES4OMOD_xME tukiamini kwamba watawala wenye dhamana kwa sasa ya kukusanya kodi watasikiliza na kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya wananchi.

Aidha, baada ya kazi mkutano wa nane wa bunge naomba kutumia fursa mjadala utakaofuatia taarifa hii kupata maoni yenu kuhusu masuala ninayopaswa kuyapa kipaumbele katika kuwawakilisha na kuwatumikia jimboni katika kipindi cha mwezi Septemba mpaka Oktoba 2012 kabla ya kuanza kwa mkutano wa tisa wa bunge na pia kuhusu maandalizi ya mwaka 2013. Kero nyingi zinazoendelea kuwepo kwa sasa ni neema iliyojificha (blessing in disguise) ili tuendelee kuunganisha nguvu ya umma kuendeleza wimbi la mabadiliko. 

Narudia tena kuwakumbusha kuwa nguvu ile ile tuliyoitumia kwenye kutafuta kura na kulinda kura ndio naiomba toka kwenu katika hatua hii ya kufanya kazi za kuwezesha maendeleo kwa kutimiza wajibu kila mmoja wetu kwa nafasi yake, kuisimamia serikali na kuunganisha rasilimali za wadau wengine; 

Maslahi ya Umma Kwanza.

Nimeandika taarifa hii leo tarehe 21 Agosti 2012 siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
Jimboni-Ubungo





Sunday, August 12, 2012

Kauli ya awali kufuatia madai ya kizushi na kijinga ya CCM kuwa CHADEMA imepewa mabilioni na nchi za nje

Katika mitandao ya kijamii kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa CCM kutoa madai mbalimbali ya uzushi katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu CHADEMA baada ya CHADEMA kuendelea kutekeleza mikakati na mipango yake ya kuwaunganisha watanzania kupitia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ katika kuchangia vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika maeneo mbalimbali nchini. Nitatoa tamko kamili na kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa iliyotolewa kwa ukamilifu, hata hivyo kuhusu madai yaliyokwisha sambazwa kwenye mitandao ya kijamii na CCM nachukua fursa hii kutoa kauli ya awali kama ifuatavyo:


Kuibuka huku kwa CCM na kufanya propaganda chafu ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna ambavyo watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali hivyo CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa chafu. Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete anapaswa kueleza watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina baraka zake na za serikali anayoiongoza kwa kurejea pia madai yaliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven Wassira kuwa CHADEMA itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa mbinu mbalimbali.

CCM kwa kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya usanii kuhalalisha fedha haramu kama ilivyofanya kwenye chaguzi zilizopita baada ya viongozi waandamizi wa CCM na makada wake kuchota fedha za chafu kifisadi kama zile za kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na vyanzo vingine vichafu na kuzisafisha kupitia harambee za hadaa zilizofanywa na CCM kwa nyakati mbalimbali; inataka kuichafua CHADEMA inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi ili kukatisha tamaa umma wa watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko.

Viongozi wa CCM wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na kujaribu kuwapotosha watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu wachache wanaweza kudanganyika kwa muda mchache lakini si watu wote wakati wote; na kwamba watanzania wa leo kwa uwingi wao hawawezi kudanganyika na uzushi wa kijinga wa CCM.

Ni ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua kuchangia mabadiliko ya kweli.

Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na narudia kwa mara nyingine tena kuitaka CCM itaje majina ya serikali, taasisi ama makampuni ya nje ambayo CCM inadai kwamba CHADEMA imepokea mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au inatarajia kupokea.

Badala ya CCM kuisingizia CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha ya vigogo wa Serikali inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao wanaelezwa kuwa na akaunti nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta, gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.

CCM ilipaswa ieleze watanzania sababu za kuendelea kusuasua kujivua magamba ya ufisadi kinyume na maazimio ya CCM yaliyofikiwa baada ya msukumo wa CHADEMA kutaja orodha ya mafisadi kwa kuwa kati ya mafisadi hao ni pamoja na viongozi wa CCM walioiingiza nchi katika mikataba mibovu.

Ikumbukwe kwamba madai haya si mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 akidai kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka mataifa ya ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano ya kuiondoa CCM madarakani.

Itakumbukwa kwamba wakati huo nilimtaka ataje nchi hizo na kueleza kusudio la kumchukulia hatua zaidi na kwa upande mwingine niliyataka mataifa hayo ya Ulaya yatoe kauli kuhusu madai hayo. Izingatiwe kwamba mataifa hayo yalikanusha madai hayo ya CCM na Sophia Simba mwenyewe alikana kuwa hakuna madai hayo dhidi ya CHADEMA.

Nimeelezwa kuwa CCM imetoa madai mengine ya uzushi kuwa CHADEMA inapewa mabilioni toka nje kwa kuwa nchi imegundua rasilimali za mafuta na gesi na kudai kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiweka nchi rehani.

Madai haya yaliwahi kutolewa pia na Katibu wa CCM wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba na nikamtaka Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe kutaja nchi hizo na mikataba hiyo hata hivyo mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote wa CCM na Serikali aliyejitokeza kutaja CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni kutoka nchi gani na kwa mikataba gani.

CCM inatoa madai hayo kuhamisha mjadala baada ya CHADEMA wa uongozi bora, sera makini, mikakati sahihi na oganizesheni thabiti kuwa mstari wa mbele katika kutetea rasilimali za taifa na watanzania kutambua kwamba taifa letu litaepushwa kutumbukia kwenye laana ya rasilimali kwa kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na kuichagua CHADEMA.

CCM na Serikali yake ndiyo imekuwa kinara wa kupokea fedha kutoka nje kwa kisingizio cha misaada na kuingia mikataba mibovu na mataifa ya nje pamoja na makampuni ya kigeni na kuachia mianya ya uporaji wa rasilimali za nchi na CHADEMA imeanika hali hii kwenye orodha ya mafisadi kwa kutaja majina ya viongozi waliohusika kwenye mikataba ya madini na tutaendelea kufanya hivyo hata katika masuala ya mafuta na gesi ambayo tayari vigogo wa Serikali inayoongozwa na CCM wameshaanza kuingia mikataba mibovu na kuingiziwa fedha katika akaunti zao za nje ya nchi.

Hivyo, badala ya CCM kutoa madai ya uzushi kuhusu CHADEMA kuingia mikataba na serikali au makampuni ya nje, CCM ieleze watanzania imechukua hatua gani mpaka sasa juu ya viongozi na wanachama wake waliongia mikataba mibovu kwenye rasilimali muhimu nchini ikiwemo madini, mafuta, gesi na maliasili zingine za taifa letu na kutoa mikataba hiyo hadharani ili watanzania waweze kuchukua hatua za kufanya mabadiliko ya kweli.

Hivi karibuni Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema kwamba serikali inayoongozwa na CCM haitarudia makosa ya kuachia mianya ya ufisadi kwenye gesi; hivyo CCM ilipaswa wakati huu kuwaomba radhi watanzania kwa ufisadi uliofanyika kwenye madini na rasilimali nyingine na kuishukuru CHADEMA kwa kuendelea kuwaunganisha watanzania wakati wote kusimamia mabadiliko ya kweli.

CCM badala ya kutishia kuwa ina mikataba inayoihusu CHADEMA ingetoa mikataba hiyo na hali hii ya CCM inayoongoza Serikali kudai CHADEMA kufanya mikakati, mipango na shughuli iliyo kinyume cha sheria bila vyombo vya dola kuchukua hatua ni ishara ya CCM kukiri wazi kuwa chama legelege chenye serikali legelege kimeshindwa kuongoza nchi na badala yake kimejikita katika propaganda chafu.

CHADEMA tangu kuanzishwa kwake imekuwa na makubaliano ya ushirikiano (MOU) bila masharti yoyote na vyama rafiki vya ndani ya Afrika na duniani na makubaliano hayo yamekuwa yakifikiwa kwa uwazi ikiwa ni sehemu ya CHADEMA kuwa na mtandao wa kimataifa na hayajawahi kuhusisha wala hayatawahi kuhusisha CHADEMA kusaidiwa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kufanya kazi zake kama inavyodaiwa na CCM.

CHADEMA kimekuwa chama kiongozi kwa nyakati mbalimbali kueleza viwango cha matumizi yake ya fedha na vyanzo vya fedha husika huku kikitegemea kwa kiwango kikubwa michango ya wanachama na wapenzi wa chama hapa nchini pamoja na kutumia kwa ufanisi ruzuku inayotolewa kwa vyama vya siasa.

CCM imekuwa na kawaida ya kutoa madai ya uzushi wakati mwingine yakiambatana na kutoa nyaraka za kughushi inazodai kuwa ni za CHADEMA. Ikumbukwe kwamba wakati wa uchaguzi wa mdogo wa Igunga, CCM ilitoa madai ya uzushi kuwa CHADEMA inafadhiliwa na nchi za nje ikiwemo kupewa mafunzo ya ugaidi na kudai kuwa tayari magaidi wameingizwa na CHADEMA toka nje katika uchaguzi huo; hata hivyo katika mwenendo wa kesi ya uchaguzi ya Igunga Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama aliyetoa madai hayo alitoa ushahidi mahakamani kwamba CHADEMA haijawahi kuleta magaidi bali kauli hizo za CCM zilikuwa ni za siasa za uchaguzi.

Hivi karibuni, CCM imeghushi waraka mwingine na kuusambaza kile ilichodai kuwa ni maazimio ya kamati kuu ya CHADEMA ya kupanga migomo ya walimu, madaktari na mipango mingine ya kuhujumu serikali; hata hivyo waraka huo ulidhihirika wazi kuwa ni wa kughushi.

Mikakati yote hiyo michafu hupangwa na CCM mara kwa mara wakati ambapo CHADEMA inaanza operesheni Sangara na mikakati mingine ya kuleta mabadiliko nchini na kujipanga kuiondoa CCM madarakani kama ilivyo sasa ambapo CHADEMA inaendelea na operesheni katika mkoa wa Morogoro hivyo watanzania wanapaswa kuipuuza CCM na kuendelea kujiunga CHADEMA na kuchangia mabadiliko kwa hali na mali mpaka kieleweke.

John Mnyika (Mb)

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

12/08/2012- Dodoma

Thursday, August 9, 2012

Maboresho madogo kukurahisishia kuramba (browsing) blog hii.

No. 1
Nashukuru sana kwa kuendelea kuwa nami katika harakati za kuleta mabadiliko ya kweli katika ngazi ya jimbo na taifa. Napenda kutangaza maboresho madogo ambayo yamefanyika katika blog hii kukurahisishia msomaji kuramba au ku-browse.

Maboresho yenyewe ni kama ifuatanyo;
Kurasa kuu za Blog hii; sasa ni rahisi kufungua kurasa kuu za Blog hii. Baada ya kubofya na kuingia katika blog hii, msomaji ataona chini tu ya picha kuu ya Blog eneo la kubofya na kuingia katika kurasa zote kuu. Kurasa hizi ni HOME; CHANGIA na WASILIANA NA MBUNGE. Kurejea katika kurasa kuu yenye taarifa zote zilizochapishwa kwenye Blog hii, bofya katika kurasa ya "HOME". Kupata maelezo ya namna ya kuchangia harakati za Mbunge na Chama, bofya "CHANGIA". Na kupata maelezo ya namna ya kuwasiliana na Mbunge, bofya "WASILIANA NA MBUNGE".

Sunday, August 5, 2012

MKUTANO WA MTANDAONI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA HIFADHI ZA JAMII KWA HATI YA DHARURA KUREJESHA FAO LA KUJITOA

Ndugu wafanyakazi na wadau wa hifadhi ya jamii,

Nawashukuru kwa kushiriki mkutano huu wa mtandaoni (online meeting) wenye ajenda moja ya kupokea maoni ya kuwezesha kuwasilishwa kwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii kwa hati ya dharura kurejesha fao la kujitoa.

Toka juzi tarehe 3 Agosti 2012 nilipotoa taarifa kwa umma ya kueleza kusudio la kuwasilisha muswada husika katika mkutano wa Bunge unaoendelea nimepokea mwito wa wafanyakazi wa baadhi ya migodi nchini kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwenda kwenye migodi husika kwa ajili ya kupokea maoni. Aidha, kufuatia kusudio hilo yametolewa pia maoni na wafanyakazi wa sekta nyingine katika Jimbo la Ubungo na maeneo mengine nchini kwenye mitandao ya kijamii na kupitia simu kuhusu haja ya kukusanya maoni kuhusu muswada husika.

Mkutano huu ni mwanzo wa mchakato wa kuitika mwito huo na kuzingatia maoni yaliyotolewa na tutaelezana ratiba ya ukusanyaji wa maoni ya ziada kupitia mikutano na njia nyingine za mawasiliano kwa ajili ya kufanikisha azma husika kwa haraka.

Friday, August 3, 2012

Muswada binafsi kwa hati ya dharura: Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii

Leo tarehe 03 Agosti 2012 kwa mujibu wa Kanuni ya 68 (7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kwa kuzingatia kuwa marekebisho yamefanyika kwenye ratiba ya bunge ambapo Mkutano wa Bunge sasa umepangwa kuahirishwa tarehe 16 Agosti 2012 na hoja za wabunge zimeondolewa kwenye ratiba.

Nimeomba muongozo ama Serikali itoe kauli bungeni ya kutengua tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ili kuwezesha mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa au uongozi wa Bunge uruhusu niwasilishe muswada binafsi wa sheria kwa hati ya dharura tarehe 16 Agosti 2012 kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye sheria husika ili kuruhusu mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa.

Pamoja na hatua hiyo ya kuomba muongozo nimechukua hatua ya ziada ya kumwandikia Katibu wa Bunge kumweleza kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi juu ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).

Thursday, August 2, 2012

NITATOA KAULI KESHO KUFUATIA MIGOGORO MIGODINI KUTOKANA NA KUFUTWA KWA FAO LA KUJITOA BAADA YA MAREKEBISHO YA SHERIA ZA MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII

Tarehe 27 Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali itoe maelezo maelezo kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa wafanyakazi ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits); suala ambalo Chama Cha Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kililikanusha.

Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya Hotuba yake tarehe 28 Julai 2012 hakutoa majibu yoyote bungeni kuhusu suala hilo hali ambayo imesababisha migongano kuendelea katika migodi mbalimbali kuhusu madai hayo hali ambayo kwa taarifa nilizozipata tarehe 1 na 2 Agosti 2012 inaweza kusababisha migomo migodini.

Naendelea na mawasiliano na wadau mbalimbali wa sekta ya madini na kesho tarehe 3 Agosti 2012 nitatoa kauli ya kina kuhusu hatua za ziada ambazo kwa nafasi ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na mbunge nitachukua kuhusu hali hiyo.

Ikumbukwe kwamba tarehe 27 Julai 2012 nilieleza bungeni kuwa ufafanuzi uliotolewa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa barua yenye Kumb. Na. AE/164/334/Vol II/2 umekataliwa katika migodi mbalimbali na kuhoji Wizara ya Nishati na Madini imechukua hatua gani kuepusha migogoro iliyoanza kujitokeza baina ya wafanyakazi wa migodini na serikali kufuatia kupitishwa kwa vifungu husika vya sheria vyenye kuagiza mafao kutolewa baada ya kufikisha umri wa hiyari wa kustaafu wa miaka 55 au umri wa lazima wa miaka 60.

Wednesday, August 1, 2012

BUNGE LISIZUIWE KUINGILIA KATI MGOGORO KATI YA WALIMU NA WANAFUNZI DHIDI YA SERIKALI KWA KISINGIZIO CHA KESI KUWA MAHAKAMANI

Tarehe 1 Agosti 2012 niliieleza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia swali langu la msingi bungeni kwamba serikali hutoa ruzuku (capitation grants) kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari za Umma zikiwemo za Jimbo la Ubungo, japo utekelezaji wa sera husika huwa unasuasua sana kwa kiwango kilichowekwa kutokulingana na mahitaji halisi ya wanafunzi; viwango vinavyotengwa katika Bajeti ni chini ya vinavyotajwa kwenye Sera na Fedha hazitolewi zote isipokuwa hutolewa kidogo kidogo na hazifiki kikamilifu mashuleni; nikahoji ni lini serikali itarekibisha hali hiyo ili kuboresha elimu nchini.

Ofisi ya Waziri Mkuu katika majibu yake imekiri kwamba kweli viwango vya ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa shule za msingi na sekondari havijafikiwa mpaka sasa na hata fedha zinazotengwa kwa mujibu wa bajeti hazitolewi kwa kiwango kilichopitishwa na bunge kwa kile alichoeleza kuwa ni makusanyo ya Serikali.

Niliuliza maswali mawili ya nyongeza; nilihoji ni lini serikali itatekeleza sera husika kwa kuwa upungufu wa ruzuku kwa shule za umma ni kati ya vyanzo vya kuporomoka kwa elimu kutokana na kuathiri uendeshaji wa shule ikiwemo upatikanaji wa vifaa shuleni, na kwa kuwa kwenye vyombo vya habari jana na leo kati walimu na wanafunzi wameeleza kwamba hali hiyo ni kati ya sababu za mgomo unaoendelea hivyo nikata serikali itoe kauli bungeni ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro unaoendelea.

Hata hivyo Spika wa Bunge alimkataza Naibu Waziri asijibu swali kuhusu mgogoro kati ya walimu na wanafunzi dhidi ya serikali na kutaka kujibiwa kwa swali ya lini ruzuku itaanza kutolewa kwa kuzingatia viwango vya sera hata hivyo serikali ilitaja kiwango cha fedha ya ruzuku kwa mwaka wa fedha 2012/2013 bila kueleza iwapo viwango kwa mujibu wa sera vitafikiwa kwenye ngazi zote ikiwemo katika shule za msingi.

Tuesday, July 31, 2012

Maoni yangu katika Sekta ya Afya: Bajeti na uhalisia!

Jana tarehe 30 Julai 2012 baada ya Hotuba ya Waziri wa Afya ya Ustawi wa Jamii kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013; Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii kuhusu Wizara husika na Maoni ya Kambi ya Upinzani nilitaka mjadala usiendelee mpaka kwanza wabunge tupewe nakala ya ripoti ya Kamati ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia mgogoro kati ya Serikali na madaktari na kuandaa mapendekezo ya kuboresha Sekta ya Afya nchini.

Nilifanya hivyo kwa kunukuu Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii ambayo pamoja na kuwa mwezi Februari 2012 bunge lilikataliwa kujadili masuala husika mpaka kwanza kamati hiyo ikapate ukweli wa pande zote mbili na kuwasilisha mapendekezo kwa bunge, taarifa ya Kamati hiyo kuhusu bajeti iliyowasilishwa jana haikueleza chochote nini kamati ilibaini baada ya kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya wala haikueleza ni ushauri gani iliutoa kwa serikali kuupatia ufumbuzi mgogoro uliokuwepo wala haikuwasilisha bungeni mapendekezo yoyote yaliyotokana na kazi waliyopewa na bunge. Aidha, Nilinukuu pia maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo yalieleza bayana kuwa mwezi Juni yalitolewa majibu yasiyokuwa ya kweli bungeni kuwa Taarifa ya Kamati hiyo iliwasilishwa bungeni.

Kufuatia hali hiyo, na kutokana na bajeti hiyo ya afya kuwa finyu huku ikiwa na utegemezi wa fedha kutoka nje kwa ziadi ya asilimia 90 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 wakati ambapo katika mwaka wa fedha 2011/2012 kiwango cha fedha ambazo wahisani walileta ni asilimia 36 pamoja na kuahidi kuchangia zaidi ya 90 kwenye fedha za maendeleo; hali ambayo itaendeleza migogoro kwenye sekta ya afya.

Nikataka ili bunge liweze kuisimamia serikali kushughulikia vyanzo vya migogoro kwenye sekta ya afya nchini; Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia madai ya madaktari iwasilishwe na kujadiliwa bungeni, majibu ya Naibu Spika aliyoyatoa ni kwamba taarifa hiyo haiwezi kuwasilishwa kwa bungeni kwa kuwa kuna kesi mahakamani baina serikali na Madaktari. Majibu hayo yamenifanya niwakumbushe taarifa hii ambayo niliitoa tarehe 29 Julai 2012 ili wadau wa afya mshiriki katika kutaka hatua muafaka toka kwa Serikali na Uongozi wa Bunge:

Sunday, July 29, 2012

Kufuatia uamuzi wa Spika wa Bunge jana jumamosi tarehe 28 Julai 2012 kukubali kuvunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini nimetakiwa kutoa maoni yangu kuhusu uamuzi husika kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na mbunge:

Kwa maoni yangu uamuzi huo ni sahihi lakini umechelewa na pekee hauwezi kurejesha heshima ya bunge kwa ukamilifu wala hautaweza kushughulikia uzembe na udhaifu ulioko kwenye bunge na kwenye serikali ikiwa hautaambana na hatua nyingine za ziada na za haraka.Kwa upande mwingine, uamuzi huo umedhihirisha nilichokisema kwa nyakati mbalimbali kuhusu uzembe wa kibunge pamoja na udhaifu wa serikali.

Ukiondoa tuhuma za wabunge wanaodaiwa kupokea rushwa ama kuwa na maslahi ya kifedha kwenye wizara, taasisi au mashirika wanayoyasimamia kwenye kamati mbalimbali, heshima ya bunge imeathiriwa vile vile na maamuzi mathalani uamuzi wa kuchaguliwa kwa mtuhumiwa wa ufisadi wa Rada Mbunge Andrew Chenge kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi.

Hivyo hatua zaidi zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuvunja na kamati zenye wajumbe waliotuhumiwa na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu za bunge ili kupunguza maslahi ya kifedha ama tuhuma za rushwa miongoni mwa wajumbe wa kamati. Aidha Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imalize kazi yake kwa dharura ili majina ya wahusika yatajwe ndani ya bunge na bunge lijadili kupitisha maazimio ya hatua za ziada za kuchukuliwa na vyombo huru vya kiuchunguzi na hatimaye watakaothibitika kuvunja sheria wafikishwe mahakamani. Pamoja na hatua hizo, Kamati za Vyama nazo zichukue hatua kwa wabunge wake watakaotajwa ili kudumisha misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa maslahi ya umma.

Hata baada ya hatua hizo, izingatiwe kuwa Bunge litaweza kujinasua kwenye uzembe ikiwa litatimiza kikamilifu wajibu wake wa kuisimamia serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 kuondoa udhaifu wa serikali kwenye sekta ya nishati na sekta nyingine muhimu za taifa kwa kuhakikisha maazimio yote ya bunge yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka kama nilivyoeleza kwenye maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni tarehe 15 Julai 2011 na tarehe 27 Julai 2012.

Friday, July 27, 2012

HOTUBA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI; WIZARA YA NISHATI NA MADINI

HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013

UTANGULIZI


Mheshimiwa Spika, awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Kanuni Kudumu za Bunge (Toleo la mwaka 2007) kifungu cha 99 (7) wa kuishauri na kuisimamia serikali; kwa kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Mheshimiwa Spika, nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi waliouniunga mkono kwa hali na mali katika kipindi chote cha misukosuko ya kusimamia ukweli na uwajibikaji: katika kuifuatilia serikali na kuunganisha wadau wengine kuwezesha maendeleo katika jimbo la Ubungo; wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wetu; wakati wa operesheni za kuhamasisha mabadiliko katika maeneo mengine nchini na katika uwakilishi wa wananchi bungeni. Utaratibu wa kupokea maoni na kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo kupitia mikutano na wananchi pamoja na katika mtandao wa http://mnyika.blogspot.com tutaendelea nao. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.

Sunday, July 22, 2012

PICHA ZA ZIARA ZA VIONGOZI WA CHADEMA, Ndago Mkoani Singida

Mbunge wa jimbo la Ubungo jijini Dar-es-salaam,John
Mnyika,akihutubia wakazi wa kijiji cha Ndago jimbo la Iramba magharibi.

Baadhi ya Viongozi wa CHADEMA waliokuwa
katika mkutano huo ,kulia Dr Kitila Mkumbo
 

Saturday, July 21, 2012

Singida:Polisi wasogeza muda.

Polisi wamesema tuongeze muda wa kusubiri kwa kuwa gari la kikosi chao toka  Dar es Salaam imepata tatizo. Tumewaeleza ikifika saa 11 jioni ama RPC aliyetuita atuhoji au turudi Dodoma hicho kikosi kilichokuja kitufate. Nimepata  hapa ushahidi wa nyaraka kuwa pamoja na vijana kikundi kidogo cha vijana wa CCM Ndago,Iramba waliofunguliwa jalada wakamatwe kwa kurusha mawe mkutanoni kuna vijana wengine toka Dar Es Salaam na maeneo mengine ya Singida ambao ni sehemu ya watuhumiwa na viongozi wa CCM wanahangaika kuwawekea dhamana. Taratibu ukweli unazidi kuibuka. Kuna njama zilipangwa na baadhi ya viongozi wa serikali, polisi na CCM juu yangu. Nasubiri nikiona kama wana muelekeo wa kuzitekeleza wakati wa mahojiano na polisi nitaweka mambo hadharani hatua kwa hatua.

Maslahi ya Umma Kwanza

John John Mnyika,
Mbunge Jimbo la Ubungo (CHADEMA)
18.07.2012

Wednesday, July 18, 2012

Mwito wa Polisi, Singida: Yanayojiri!

Nimefika Singida kuitikia mwito wa Polisi kutoa maelezo kuhusu mkutano nilioalikwa Iramba kwa nafasi yangu ya Mkurugenzi wa Habari na Uenezi.

Nimekutana na RPC, amesema kwamba nisubiri mpaka saa 10:30 alasiri ndiyo nikutane nao kwa kuwa kwa sasa kuna kikosi cha upelelezi toka Dar Es Salaam kimekwenda eneo la tukio. Nimemuuliza RPC maswali mawili;

1. Wameniita kutoa maelezo kama mtuhumiwa au shahidi?

Amenijibu kuwa ni mahojiano ya kawaida.

2. Kwanini mpaka sasa watuhumiwa 12 waliofunguliwa jalada NDG/RB/190/2012 kwa kurusha mawe kwenye mwanzo wa mkutano wakati Bwana Waitara akitoa hotuba ya utangulizi huku polisi wakiachia hali hiyo. Baada ya kufungua jalada na polisi wa juu kupigiwa simu kuwa kuna njama kati ya Polisi na CCM hali ilitulia, Waitara akamaliza hotuba yake, Dkt Kitila akasalimia name nikahutubia kwa amani na kwenda kwenye mkutano mwingine. Mauaji yalitokea baadae mbali na tulipohutubia.

John John MNYIKA,

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA)

18 Julai, 2012

Monday, July 16, 2012

Tutibu kiini cha tatizo Sekta ya Nishati ya Umeme!

Kwa nafasi ya Uwaziri Kivuli wa Nishati na Madini,nafahamu kuna ufisadi na ubadhilifu ndani ya TANESCO ambao uchunguzi ni muhimu kwa ajili ya uwajibikaji.Kusimamishwa kwa Mkurugenzi wa TANESCO na maafisa wengine wa shirika hilo kupisha uchunguzi ni muhimu,lakini si muarubaini wa uozo wa kimfumo katika sekta ya nishati nchini nitatoa vielelezo vya kina wakati nitakapo wasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni katika wizara ya Nishati na Madini.

Hata hivyo ni vyema nikatahadharisha mapema kuwa tukio hili linapaswa kutafakariwa kwa upana kwa kuwa linahusisha masuala mengi ambayo mengine Bodi ya Wakurugenzi imeyaacha nyuma ya pazia.Ukweli wote utakapotoka hadharani wengine zaidi watapaswa kuwajibika au kuwajibishwa kwa maslahi ya Taifa!

Kwa nyakati mbalimbali toka mpango wa dharura wa umeme uwasilishwe bungeni,nimekuwa nikiitahadhalisha na kuihoji serikali(kama sehemu ya jukumu langu la kibunge) kwa uzembe,ufisadi na udhaifu wa kiutendaji katika serikali ambao hasara yake utairejesha nchi katika mgao wa umeme hali ambayo imedhihirika hivi sasa!

Sunday, July 15, 2012

Majibu juu ya MAJI na hoja binafsi

Jana tarehe 13 Julai 2012 niliuliza swali la nyongeza bungeni kuhusu mtandao wa mabomba maarufu kama mabomba ya wachina kutokutoa maji kwa miaka mingi kwenye maeneo kadhaa ya Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla; nilihoji hatua za dharura za serikali za kuhakikisha mabomba hayo yanatoa maji badala ya kusubiri mpaka Disemba 2014 kama ilivyoelezwa katika hotuba ya Wizara ya Maji, nilihoji pia hatua zilizochukuliwa  kwa waliosababisha uzembe wenye kulitia hasara taifa kwa kuwa mabomba hayo yameanza kuharibika.

Katika majibu serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Maji Dkt. Binilith Mahenge ilieleza kuwa upo uwezekano wa sehemu ya miundombinu kuharibika au kuharibiwa na ili kuepusha hali hiyo serikali inatekeleza miradi ya kuongeza uzalishaji kutoka Ruvu chini, Ruvu juu na vyanzo vingine. Aidha, baada ya miradi hiyo kukamilika mtandao wa mabomba utahakikiwa na kama kuna kasoro zitarekebishwa na pia kama kuna ubadhirifu wowote utakao bainika Serikali itachukua hatua.

Ninachoweza kusema kwa sasa ni kuwa Hotuba ya Waziri wa Maji Prof, Jumanne Maghembe akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya matumizi ya fedha za Wizara ya Maji kwa mwaka 2012/2013 tarehe 9 Julai 2012 na majibu haya ya Naibu Waziri ya tarehe 13 Julai 2012 yanadhihirisha haja ya hoja binafsi niliyoiwasilisha ya kuomba bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.
Ikumbukwe kwamba Rais Jakaya Kikwete na mawaziri mbalimbali kwa nyakati mbalimbali waliahidi kwamba tatizo la maji kuwa historia katika mkoa wa Dar es salaam mwaka 2013;  kinyume na ahadi hiyo kauli mpya ya Waziri bungeni ni kuwa sasa miradi hiyo inakamilika mwaka 2014. Hata hivyo, uchambuzi wangu kuhusu bajeti iliyopitishwa mwaka 2011/2012 na 2012/2013 inaonyesha kwamba hata lengo hilo la 2014 haliwezi kufikiwa kwa kuwa kiwango cha fedha kilichotengwa ni kidogo pungufu ya kilichopaswa kutengwa kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa maendeleo, hivyo kama mwelekeo wa utekelezaji utakuwa wa kusuasua kama ilivyo sasa matatizo ya maji katika Jiji la Dar es salaam yatadumu mpaka zaidi ya mwaka 2016 tofauti na ahadi zinazotolewa na serikali.
Ikumbukwe kwamba Mwezi Februari 2011 Wizara ya Maji iliandaa waraka maalum wa kuiomba Serikali kutenga kiasi cha shilingi bilioni 653.85 Mpango Maalum 2011-2013 wa kuboresha huduma za majisafi na uondaji wa majitaka katika Jiji la Dar es salaam na kupitishwa na Baraza la Mawaziri lakini kiwango cha fedha kinachotengwa na serikali hakizingatii waraka huo na maazimio ya baraza la mawaziri kwa ukamilifu wake hali ambayo inahitaji bunge kuisimamia serikali kwa haraka.

Aidha, Wizara ya Maji haionyeshi kuichukulia kwa uzito unaostahili kashfa ya Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji; hivyo hatua za kibunge zinahitajika katika kuwezesha ukaguzi stahiki.
Kwa upande mwingine, wakati miradi ya muda mfupi ikiendelea kusubiriwa, wananchi wanahitaji maji ya haraka hivyo Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo wa kukamilika kuwa Oktoba 2012 katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa tofauti na ahadi ya Rais Kikwete aliyoitoa Kimara mwezi Mei mwaka 2010.
Nashukuru kwamba baada ya kueleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi tarehe 8 Juni 2012 hatua zifuatazo zimechukuliwa na Wizara ya Maji: Mosi, kwa mara ya kwanza Wizara imejibu barua yangu na kueleza hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa za kushughulikia kwa haraka matatizo ya maji katika Jimbo la Ubungo. Pili, Wizara imetoa mrejesho wa utekelezaji wa Mpango wa dharura wa Maji kwa jiji la Dar es salaam.
Hata hivyo, kwa kuwa maelezo na majibu yaliyotolewa hayajashughulikia kwa ukamilifu hatua saba ambazo nilipendekeza Wizara ya Maji ichukue nitaendelea kuchukua hatua katika mkutano huu wa nane unaoendelea kuwasilisha hoja binafsi kuomba bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.
Izingatiwe kwamba tarehe 8 Juni 2012 nilieleza kwamba nimewasilisha  kwa katibu wa bunge taarifa ya hoja pamoja na maelezo ya hoja; hivyo ninachosubiri hivi sasa ni kujulishwa iwapo hoja husika imekubaliwa kuwasilishwa bungeni katika mkutano wa bunge unaoendelea hivi sasa.
Kati ya hatua hizo saba amabazo bunge ni muhimu likapitisha maazimo ya kuisimamia serikali kwa mujibu wa katiba ya nchi ibara ya 63 (2) na (3) ni pamoja na ; Mosi,  kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kashfa ya taifa ya kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.
Pili; kuwasilisha  bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa bajeti kamili ya utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kusimamiwa ipasavyo kwa msukumo wa kibunge badala ya ahadi za ujumla za kwenye ziara.
Tatu; Serikali kueleza hatua zilizopangwa kuchukuliwa kufuatia ziara ya Wizara ya Maji kuhakikisha Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 unawekewa muda wa ukomo wa kukamilika ndani ya miezi mitatu katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.
Nne; Serikali kukubaliana na pendekezo nililotoa bungeni kwa nyakati mbalimbali la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.
Tano; Serikali kuhakikisha Wizara ya Maji inaisimamia EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali. Aidha, Serikali ihakikishe EWURA inaharakisha kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.
Sita; Serikali iwezeshe Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 iliyotolewa na CAG kwa haraka ili maoni na mapendekezo yazingatiwe mapema iwezekanavyo.
Saba; Serikali ihakikishe inawasilisha kwenye mkutano wa tisa wa bunge muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
Imetolewa Dar es salaam tarehe 14 Julai 2012 na:

John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
Bungeni-Dodoma




Thursday, July 12, 2012

OFISI YA WAZIRI MKUU HAIKUJIBU UKWELI BUNGENI SWALI LANGU KUHUSU MGOGORO KATI YA SERIKALI NA WALIMU


Ofisi ya Waziri Mkuu imejibu uongo  bungeni kuhusu uwepo wa mgogoro kati ya Serikali na walimu hivyo nakusudia kumwandikia Spika aagize swali hilo lijibiwe kwa ukweli na ukamilifu.
Tarehe 11 Julai 2012 wakati nikiuliza swali la nyongeza kwa ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya walimu watumishi wa umma katika Jimbo la Ubungo na nchi kwa ujumla kuwa ni lini serikali itakamilisha kushughulikia madai ya walimu kwa kuwa matatizo walimu yamedumu kwa miaka mingi kwa kiwango cha kufikia hatua ya walimu kutangaza mgogoro na serikali.
Akijibu swali langu kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Majaliwa Kassim Majaliwa hakueleza kwa ukamilifu ni lini serikali itakamilisha kushughulikia madai ya walimu badala yake akatoa majibu ya uongo kuwa walimu hawajatangaza mgogoro  na serikali.
Hata hivyo, ukweli ni kuwa walimu wametangaza mgogoro na serikali na ushahidi ni tamko la Serikali  yenyewe kuhusu migomo sehemu za kazi lililotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira tarehe  9 Julai 2012 ambalo limeeleza kuwa tayari Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kwa niaba ya walimu nchini kimeishawasilisha mgogoro katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi- Dar es salaam wenye usajili CMA/DSM.ILA/369/12.
Hivyo, naendelea kusisitiza serikali ichukue hatua ya kushughulikia vyanzo vya migogoro na watumishi wa umma badala ya kusubiri mpaka matokeo ya migogoro kama migomo na madhara mengine kwa nchi na wananchi ndio ianze kutumia nguvu kuidhibiti.
Migogoro kati ya serikali na watumishi wa umma ina athari kubwa; wakati migogoro ya madaktari huchangia katika kuathiri hali na uhai wa wagonjwa, migogoro kati ya serikali na walimu inachangia katika kudidimiza ubora wa elimu na kuathiri maisha ya wanafunzi.
Na wabunge  tupewe nafasi ya kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu wa mamlaka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) kwa kuletewa taarifa sahihi na pia kujibiwa maswali kwa ukweli na ukamilifu kabla ya serikali kwenda mahakamani baada ya majadiliano yake na watumishi wa umma kukwama kama ilivyotokea kwa madaktari.
Aidha, Spika aliwezeshe bunge kupokea taarifa maalum ya kamati ya bunge ya huduma za jamii kuhusu madai ya watumishi wa umma ambayo mengi chanzo chake ni ufinyu wa bajeti ili katika mkutano huu wa bunge la bajeti unaoendelea bunge liweze kujadili na kuisimamia serikali kushughulikia vyanzo vya migogoro badala ya matokeo.

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
13/07/2012

Saturday, July 7, 2012

Barabara za Kupunguza Msongamano na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi

Jana usiku tarehe 6 Julai 2012 Bunge limepitisha mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2012/2012. Mtakuwa mmeona wakati bunge lilipokaa kama kamati nilishika mshahara wa Waziri kutaka maelezo ya kisera juu ya mkakati wa serikali katika kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika barabara ya Morogoro inayopita Jimbo la Ubungo.


Nilitaka maelezo hayo kwa kuwa pamoja na kuunga mkono uwekezaji kwenye upanuzi wa barabara kuu, ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa fly overs, miradi hii kwa ujumla wake inachukua muda wa kati na muda mrefu hivyo kukamilika kwake ni mpaka mwaka 2016 au zaidi.

Nilitaka maelezo ni kwanini Serikali isizingatie vipaumbele vya mwaka wa kwanza wa mpango wa miaka mitano katika kuandaa bajeti ili pamoja na miradi hiyo niliyoitaja iwekeze kwa haraka kwenye barabara za pete/mzunguko (ring roads) za pembezoni ambazo zinaweza kujengwa kwa kiwango cha lami katika kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuchangia kwenye kupunguza foleni katika barabara kuu ifikapo mwaka 2013.

Kufuatia majibu ya Waziri nilihoji tena wakati bunge linapitisha vifungu vya miradi ya maendeleo kwenye kasma ya kuondoa foleni Dar e salaam ambayo imetengewa shilingi bilioni 10.5 tu, wakati ambapo mpango wa taifa wa miaka mitano uliopitishwa umeelekeza kifungu hicho kitengewe jumla ya fedha kwa miaka miwili 2011/2012 na 2012/2013 kiasi cha shilingi bilioni 100.1. Ikumbukwe kwamba mwaka jana serikali ilitenga bilioni 5 tu wakati mpango uliitaka serikali itenge bilioni 68 na nilipohoji wakati huo nilijibiwa kwamba ilikuwa ni kipindi cha mpito hivyo fedha zote zingeunganishwa mwaka huu kitu ambacho hakikufanyika.

Majibu ya kwamba Dar es salaam na Pwani kwa ujumla zimetengewa bilioni zaidi ya 900 yanajumuisha fedha za maendeleo kwa miradi iliyoanza 2010/2011, 2011/2012, 2012/2013 na ni miradi ya muda mrefu ya barabara kuu na madaraja makubwa kwa mikoa yote miwili.

Kwa hiyo bilioni 10.5 imegawanywa kidogo kidogo kwa barabara zifuatazo: Mbezi Luis kupitia Goba mpaka Mbezi Tangi Bovu; Mbezi kwa Yusuph- Msakuzi- Mpiji Magohe mpaka Tegeta/Bunju; Mbezi-Malambamawili-Kinyerezi, Kimara-Mavurunza-Bonyokwa; Kimara-Kilungule-Makoka-Makuburi, Kimara-Matosa-Mbezi; Ubungo-Msewe-Chuo Kikuu na nyingine katika maeneo mengine ya Dar es salaam kama zilivyoelezwa katika hotuba ya Waziri. Kwa kasi hii ndogo, itachukua takribani miaka kumi kuweza kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hizo ambazo jumla ya urefu wake ni kilomita 96 tu.

Nashukuru kwamba fedha zimetengwa kumalizia pia barabara ya Ubungo Maziwa- Bus Terminal na pia za kuanza ya kuelekea External, na pia bilioni zaidi ya 240 za mradi wa DART; hata hivyo, tuendelee kuungana katika kuisimamia serikali ili itenge bilioni 100 kujenga kwa kiwango cha lami barabara tajwa za pembezoni za kupunguza msongamano haraka zaidi wakati tukisubiri utekelezaji wa miradi ya muda wa kati na muda mrefu.

Tuendelee kuishauri Tume ya Mipango ambayo Mwenyekiti wake ni Rais kuingiza kwenye Mpango wa Mwaka wa Maendeleo Mwezi Februari 2013 ili hatimaye kiwango hicho cha fedha kiingizwe katika bajeti. Izingatiwe pia kuwa sehemu ya Barabara hizo ni ahadi za Rais alipotembelea Jimbo la Ubungo kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010 na kurudia tena ahadi hizo wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2010. Tuendelee kushirikiana katika kufuatilia kazi za maendeleo.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,



John Mnyika (Mb)

7/7/2012-Bungeni, Dodoma

Sunday, July 1, 2012

MAONI YA MBUNGE WA UBUNGO KUHUSU HOTUBA YA MH. DKT. JAKAYA KIKWETE RAIS WA TANZANIA KWA WANANCHI TAREHE 30 JUNI 2012




Leo tarehe 1 Julai 2012 kumesambazwa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari hotuba ya Mh. Dkt. Jakaya Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi inayotajwa kutolewa tarehe 30 Juni 2012.

Kufuatia hotuba hiyo na kufuatia mwito kutoka wachangiaji wa mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kutaka maoni yangu kuhusu hotuba husika, naomba nichukue fursa hii kutoa maoni kwa nafasi yangu ya ubunge kuhusu hotuba tajwa kama ifuatavyo:

Hotuba hiyo ya Rais imeibua mjadala na masuala ambayo yanahitaji kujadiliwa bungeni katika mkutano wa nane wa Bunge unaoendelea hivyo, serikali isiendelee tena kutumia kisingizio cha mahakama kulizua bunge kujadili masuala husika wakati yenyewe inayajadili na kuyatolea maelezo na maelekezo pamoja na kuchukua hatua hususani kuhusu suala la mgomo wa madaktari.

Hotuba hiyo ya Rais ukindoa suala la usafirishaji haramu wa watu nchini inaelekea kuwa ndiyo kauli ya Serikali ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliahidi kwamba ingetolewa bungeni lakini baadaye serikali ikasema haitatoa kauli. Uamuzi wa Serikali kuitoa kauli hiyo kupitia hotuba ya Rais una mwelekeo wa kukwepa wabunge wasijadili hotuba husika na pia wasitimize wajibu wa kikatiba wa ibara 63 (2) wa kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi.

Hivyo, Ofisi ya Rais na Ikulu wanapaswa kutoa maelezo kwa umma sababu za Rais kutolihutubia taifa tarehe 30 Juni 2012 kama ilivyotangazwa katika baadhi ya vyombo vya habari vya kielectroniki na badala yake hotuba ya Rais kusambazwa tarehe 1 Julai 2012 kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari na iwapo masuala ya hotuba hiyo kuhusu mgomo wa madaktari ndiyo yale ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikusudia kuyaeleza bungeni.

Aidha, kwa kuwa bunge litajadili mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kuanzia kesho tarehe 2 Julai 2012 na kuendelea ni muhimu wabunge wakajadili pia masuala ambayo Rais ameyaeleza kwa taifa na kutimiza wajibu wa kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) wa kuishauri na kuisimamia serikali.

Kuhusu Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini
Ni vizuri hotuba ya Rais imeeleza wazi kwamba tukio la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si la kwanza kutokea hapa Tanzania kwa kuwa kwa kipindi cha miaka kumi kumekuwa na ongezeko la usafirishaji haramu wa binadamu katika taifa letu kupitia mipaka ya mikoa mbalimbali hapa nchini. Kwa mbinu yoyote ile ambayo imetumika, matukio haya yanaashiria kwamba mipaka yetu haipo salama kwa kuwa kama malori na vyombo vingine vya usafiri vyenye watu wasio na hati za kuingilia nchini wanaweza kuingia kwa wingi kwa nyakati mbalimbali tafsiri yake ni kwamba nchi iko kwenye hatari ya kuingiziwa pia vitu vingine haramu ikiwemo madawa ya kulevya na silaha hali ambayo ni tishio kwa usalama wa nchi na maisha ya wananchi. Ni vizuri Rais amekutana tarehe 27 Juni 2012 na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuzungumzia tukio hilo; hata hivyo, zaidi ya kuwapongeza vyombo vya dola kwa kazi nzuri ya kudhibiti shughuli za biashara haramu, nilitarajia kwamba Rais kwa mujibu wa mamlaka yake ya ibara ya 33 (2) ya mkuu wa nchi, kiongozi wa serikali na amiri jeshi mkuu angeagiza uchunguzi ufanyike kuhusu udhaifu uliojitokeza na kuagiza hatua kuchukuliwa kwa walishindwa kudhibiti hali hiyo katika mipaka ambayo biashara haramu ya usafirishaji wa watu inapitia. Izingatiwe kwamba mianya hii katika mipaka yetu ina athari pana sio katika suala hili tu bali pia katika usalama wa maisha ya wananchi kama ilivyo katika mikoa ya Kigoma, Kagera na kwingineko ambapo uhai wa wananchi na mali zao uko mashakani kutokana na uvamizi toka kwa wahamiaji haramu. Aidha, athari za hali hiyo zimejitokeza katika usambazaji wa chakula toka kwenye hifadhi ya taifa ambapo pamoja na Serikali kutumia zaidi ya bilioni 27 kusambaza mahindi na nafaka nyinginezo bei za bidhaa hizo katika Soko la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo hazikushuka kutokana na vyakula hivyo kutoroshwa na kuuzwa nje ya nchi kutokana na udhaifu katika ulinzi kwenye mipaka.

Hivyo, ni muhimu wabunge wakati wa mjadala wa bajeti ya ofisi ya Rais wataka kuongezeka kwa uwajibikaji na usimamizi wa utawala wa sheria ili kudumisha amani nchini.

Hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa ni pamoja na bunge kuisimamia serikali kuhakikisha idara ya usalama wa taifa inafanya kazi kwa ufanisi zaidi katika kuvisaidia vyombo vingine vya dola kulinda mipaka ya nchi na pia matatizo ya maslahi katika vyombo vya ulinzi na usalama yanatatuliwa ili vyombo husika viweze kufanya kazi bila baadhi ya maofisa wake kujihusisha na vitendo vya ufisadi na kuruhusu biashara haramu za aina mbalimbali.

Kuhusu Mgomo wa Madaktari

Kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa; hotuba ya Rais imeendeleza kauli za upande mmoja ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali kuhusu mgogoro huo bila taifa kupewa fursa ya kupata maelezo na vielezo vya upande wa pili; hivyo kuwa serikali imetoa kauli yake hadharani badala ya bungeni au mahakamani, ni muhimu pia taarifa ya kamati ya bunge ya huduma za jamii iliyoshughulia suala hilo na kukutana na pande zote mbili itoe taarifa yake bungeni na kwa umma.

Katika hotuba yake Rais amewaeleza kwa kiwango kikubwa wananchi namna ambavyo madaktari wanasababisha mahangaiko kwa wagonjwa wengi na kusababisha vifo kwa wengine lakini hakueleza kabisa mchango wa serikali katika kusababisha hali hiyo. Hivyo, kwa kuwa pande zote mbili zinachangia katika athari zinazoikumba nchi na wananchi kutokana na mgomo; ni muhimu chombo cha tatu kikaingilia kati kuwezesha ufumbuzi kupatikana na chombo hicho ni bunge ambalo ndilo lenye wajibu wa kuisimamia serikali. Jitihada za kuwalazimisha madaktari kurejea kazini bila majadiliano ya pande mbili mbele ya chombo cha kuisimamia serikali kushughulikia chanzo cha mgogoro huo zinaweza kuleta ufumbuzi wa muda mfupi na athari za muda mrefu.

Ieleweke kwamba hata madaktari wakisitisha mgomo wa wazi kutokana na amri ya mahakama na agizo la Rais, migogoro katika ya serikali na watumishi wa umma wenye kusababisha migomo baridi ya chinichini ina madhara ya muda mrefu kwa taifa.

Mathalani, kutokana na migomo baridi na huduma mbovu katika sekta ya afya wananchi wa kawaida wamekuwa wakifa kutokana na magonjwa yanayotibika.

Migomo ya chini kwa chini ya walimu na mazingira mabovu yamekuwa yakisababisha kudidimia kwa elimu katika shule za umma; mwanafunzi aliyehitimu masomo yake bila kujua kusoma na kuandika hana tofauti na mgonjwa anayekufa kwa kukosa huduma.

Hali hii ya kugoma kusiko kwa wazi imeenza kujipenyeza mpaka kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuachia mianya ufisadi na kushindwa kusimamia utawala wa sheria kama ivyodhihirika kwa kuongezeka kwa vitendo vya biashara haramu katika taifa letu.

Rais amewaeleza wananchi kuwa kati ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari na kwamba katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa na pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba. Hata hivyo, katika masuala matano yaliyobaki, Rais hakueleza kwa wananchi nini ambacho serikali ilikuwa tayari kutoa kwa kila madai na kwa kiasi gani badala yake ameonyesha tu kwa ujumla kwamba madai hayo hayatekelezi.

Aidha, kufuatia hotuba hii ya Rais Madaktari nao wana wajibu wa kuueleza umma msingi wa madai yao na kwa kiwango gani walikuwa tayari kushuka kutoka katika madai yao ya awali, kinyume na hayo itaonekana kwamba madaktari waliingia katika majadiliano wakiwa na msimamo wa kutaka madai yao pekee ndiyo yakubaliwe wakati ufumbuzi wa mgogoro wa pande mbili hupatikana kwa win win (give and take).

Ni vizuri ikafahamika kwamba katika majadiliano, pande zote mbili huwa na mapendekezo yake; hivyo upo uwezekano kwamba yapo madai ambayo madaktari wameyatoa ambayo serikali haina uwezo wa kuyatimiza kwa kiwango walivyopendekeza na yapo ambayo serikali imeyakataa wakati ambao ina uwezo wa kuyatekeleza hata ikiwa kwa kiwango pungufu ya kile kilichopendekezwa na madaktari.

Suluhu katika mgogoro kama huo ambao kila upande una mapendekezo yake linapaswa kufanywa na vyombo vya usuluhishi; hata hivyo kuwa suala hili linahusu mgawanyo wa rasilimali za nchi na bajeti ya serikali, chombo chenye mamlaka ya kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi ni bunge.

Na kwa kuwa kamati ya bunge ya huduma za jamii ilikutana na pande mbili, ilikuwa muhimu kwa serikali kabla ya kupeleka shauri mahakamani kurejesha kwamba suala husika bungeni ambalo ndilo lenye wajibu wa kupendekeza vipaumbele vya mpango wa serikali na ndilo lenye kuidhinisha bajeti ya matumizi ya serikali.

Uamuzi wa serikali kukimbilia mahakamani kabla ya majadiliano ya bunge umechangia katika kusababisha mgomo wa madaktari, hivyo ushauri wangu kwa Rais Kikwete ni kwa serikali kufuta kesi iliyoko mahakamani ili bunge lipewe fursa ya kujadili ripoti yake kamati yake na kupitisha maazimio ya kuwezesha suluhu kati ya serikali na madaktari.

Mahakama iwe ni hatua ya mwisho baada ya mihimili miwili muhimu ya serikali na bunge kushindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoendelea wenye athari kwa nchi na maisha ya wananchi.

Rais Kikwete ameeleza taifa kwamba Serikali imeongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2 mwaka 2011/12; hata hivyo serikali inapaswa pia kulieleza taifa namna ambavyo kiwango hicho cha fedha kinapungua ukiweka kizio (factor) cha kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumumo wa bei ukilinganisha mwaka 2005 na 2012.

Ukweli ni kwamba bajeti ya Sekta ya Afya bado ni ndogo kwa kuwa serikali haijatimiza bado azimio la kutenga asilimia 15 kwa ajili ya bajeti ya afya pia, hata kiwango hicho cha ongezeko la fedha hakijaleta matokeo ya kutosha kutokana na matumizi kuelekezwa kwenye baadhi ya maeneo yasiyokuwa ya kipaumbele na kuwa na utegemezi wa kiwango kikubwa cha fedha za wahisani ambazo kwa mwaka huo wa 2011/2012 aliourejea Rais Kikwete hakikutolewa kwa kiwango kilichoahidiwa. Hivyo, Rais Kikwete awezeshe kuongezwa kwa fedha za ndani kwenye bajeti ya afya kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Katika madai mengine Rais Kikwete ameeleza kwamba pande mbili zilifikia makubaliano nusu nusu, hali ambayo inaashiria kwamba madaktari wana hoja ambazo zinahitaji majadiliano hivyo, ni muhimu bunge likapewa nafasi ya kujadili kuweza kuwakilisha pande zote mbili za serikali na madaktari kuhusu nini kinawezekana na nini hakiwezekani ili kulinusuru taifa na mgogoro unaoendelea.

Rais Kikwete ametumia kwa kiwango kikubwa madai ya madaktari ya ongezeko la mshahara kujaribu kuwachonganisha wananchi na madaktari kwa kuwa na madai yasiyotekelezeka. Hata hivyo, ni muhimu ikafahamika kwamba sio madaktari pekee ambao wana mgogoro na mwajiri wao yaani serikali kuhusu kiwango cha mshahara bali pia watumishi wengine wa umma ikiwemo walimu.

Nyongeza iliyotolewa na serikali ya kati ya asilimia 15 na 20 kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 ni tofauti na ahadi ambazo serikali imekuwa ikitoa kwa wafanyakazi za kuongeza mishahara na kupunguza kodi katika mishahara. Rais Kikwete na serikali warejee maoni na mapendekezo ya kambi rasmi ya upinzani kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na 2012/2013 kuhusu nyongeza za mishahara kwa watumishi wa umma na vyanzo mbadala vya mapato vya kuongeza kwa ajili ya kuwa na uwezo wa kutimiza mahitaji. Uwiano wa sasa wa matumizi ya mishahara kuwa asilimia 48 ya bajeti badala ya uwiano mzuri wa asilimia 35 kuwa mishahara na na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa; ni matokeo ya udhaifu wa serikali katika kupanua vyanzo vya mapato, kupunguza matumizi ya kawaida yasiyo ya lazima na kuongeza fedha katika miradi ya maendeleo hali ambayo Rais Kikwete kuliwezesha bunge kuisimamia serikali na kuirekebisha.


Kuhusu Suala la Dkt. Steven Ulimboka

Rais Kikwete ameeleza wananchi kuwa ameelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane; hata hivyo kauli hii inaashiria kukubaliana na hatua iliyochukuliwa na jeshi la polisi kuunda jopo la kuchunguza.

Nilitarajia Rais Kikwete kwa kutambua uwepo wa madai ya polisi kutuhumiwa kuhusika katika jaribio la mauji ya Dr Ulimboka angetangaza kuunda tume huru ya uchunguzi au walau angeongeza nguvu katika jopo la uchunguzi lililoundwa kwa kuunda timu ya maafisa waandamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama na usalama pamoja na wadau wengine kutoka taasisi huru.

Rais Kikwete anapaswa kutumia madaraka yake kwa mujibu wa katiba kuunda tume huru ambayo inadhihirisha kwa vitendo kwamba watuhumiwa hawajichunguzi wenyewe na kuwezesha matokeo ya uchunguzi kuaminika.

Narudia kuwasihi madaktari kuendelea kuokoa maisha ya wananchi katika kipindi hiki kigumu lakini wakati huo huo Rais Kikwete aiongoze serikali kuepusha athari zaidi katika sekta ya afya ya kuwa na mgogoro na madaktari kwa kuliwezesha bunge kujadili suala hili na kulipatia ufumbuzi ikiwemo kupitia nyongeza ya bajeti ya Wizara ya Afya. Nimemwandikia barua Spika Anna Makinda akiwa ni mkuu bunge kama muhimili mmojawapo wa dola kuweza kuchukua hatua stahili, naomba pande zote zizingatie maoni yanayotolewa na wabunge kwa niaba ya wananchi kwa maslahi ya taifa.

Maoni haya yametolewa leo tarehe 1 Julai 2012 na:

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma