Mihimili miwili ya nchi yaani bunge na serikali inapaswa kutoa uongozi thabiti wenye kuwezesha Tanzania kupata wabunge wanaokubalika na umma wa Bunge la Afrika Mashariki katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kwenye mkutano ujao wa bunge.
Ili kutimiza azma hiyo Spika wa Bunge Anna Makinda anapaswa kuwezesha marekebisho ya msingi ya kanuni zinazosimamia uchaguzi husika kabla ya katibu wa bunge kutoa tangazo la uchaguzi tajwa.
Aidha, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta anapaswa kutoa kwa umma na kwa vyama vya siasa muswada wa sheria ya uchaguzi wa Afrika Mashariki wa mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki ili uwe msingi wa marekebisho yanayopaswa kufanyika kabla ya uchaguzi husika kufanyika nchini.
Uchaguzi huu una umuhimu wa pekee kwa wananchi wa Tanzania ikiwemo wa Jimbo la Ubungo wakati huu ambapo jumuiya ya Afrika Mashariki ipo katika soko la pamoja na majadiliano ya kuwa na sarafu moja yanaendelea hali ambazo zina athari kwa nchi na wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Izingatiwe kuwa tarehe 10 Februari 2012 wakati wa kuahirishwa kwa mkutano wa sita wa Bunge Spika Makinda ametangaza kuwa uchaguzi wa wabunge wa kuwakilisha Tanzania kwenye bunge la Afrika Mashariki utafanyika katika mkutano wa saba wa Bunge unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 10 Aprili 2012.





