Wednesday, December 29, 2010

Hoja ya katiba mpya kuwasilishwa bungeni

Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, leo anatarajia kuwasilisha rasmi kwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano taarifa ya Hoja Binafsi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.

" Nachukua fursa hii kutoa taarifa kwamba Jumatatu (leo) nitakwenda kuwasilisha kwa Katibu wa Bunge taarifa ya Hoja Binafsi kuhusu Mchakato wa Katiba Mpya," alisema katika taarifa yake.

Desemba 19, mwaka huu, Mnyika alikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kudokeza kusudio lake la kuwasilisha hoja hiyo katika mkutano wa pili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakaoanza Februari mwakani. Vilevile aliahidi kwamba atawasilisha taarifa ya hoja hiyo wiki moja baada ya kukutana na waandishi wa habari.

" Taarifa hiyo nitaiwasilisha kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kifungu cha 55 (1) kwa ajili ya Bunge kupitisha maazimio ya kuweka utaratibu wa kiusimamizi na wa kisheria wa kuratibu mchakato mzima wa kuandikwa kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema Mnyika katika taarifa yake hiyo jana.

Hata hivyo, alisema tangu aeleze kusudio lake, baadhi ya watu wamekuwa wakiipotosha hoja yake kupitia vyombo vya habari.

Alisema ieleweke kwamba yeye kama Mbunge, anapokwenda kuwasilisha hoja hiyo kuhusu katiba mpya anafanya hivyo kama sehemu ya kutimiza wajibu wa kuwawakilisha wananchi na kulinda ukuu wa katiba katika taifa.

" Izingatiwe kwamba ibara ya 8 (1) imeeleza bayana kwamba mamlaka na madaraka ni ya wananchi na kwamba ibara ya 63 (2) (3) imeeleza kwamba Bunge ndicho chombo kikuu chenye madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri serikali kupitia kupitisha mipango, kutunga sheria nk. Ibara ya 98 (1) imekwenda mbali zaidi kwa kutoa mamlaka kwa bunge kutunga sheria kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya kikatiba," alisema na kuongeza kuwa:

" Hivyo, hoja binafsi ninayokwenda kuiwasilisha ni kwa ajili ya Bunge kwenda kutimiza wajibu huu wa kikatiba ambao wabunge wote tumeapa kuulinda na kuutetea, kufanya hivyo hakuwezi kuwa tendo la ’unafiki’," alisisitiza.

Mnyika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, alisema pamekuwepo pia na upotoshoji unaoeleza kuwa anakusudia kwenda kuwasilisha rasimu ya katiba mpya bungeni kupitia hoja binafsi.

" Izingatiwe kwamba siendi kuwasilisha rasimu ya katiba mpya, kwa kuwa sio jukumu la mtu mmoja, au chama kimoja, au taasisi moja, au dini moja kuandaa katiba; ni jukumu la Watanzania,” alisema.

Mnyika alifafanua kuwa anachokwenda kuwasilisha bungeni ni hoja binafsi kwa ajili ya Bunge kuazimia kuweka utaratibu utakaoanzisha, kusimamia na kuwezesha Serikali kuratibu mchakato wa katiba mpya utaohakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu kuandika katiba kupitia tume inayohusisha wadau, elimu kwa umma, mkutano mkuu wa taifa wa katiba, kura ya maoni (referundum) na kadhalika.

Alisema mtu binafsi, taasisi, chama au dini kinaweza kuwa na maoni yake kuhusu katiba ambayo kinaweza kuyatoa kwa njia ya taarifa au hata kuandaa rasimu sifuri, lakini hatimaye lazima kuwe na mfumo wa pamoja ili kuwe na makubaliano ya kitaifa kwa kuwa katiba sio mali ya chama chochote, dini yoyote au mtu yeyote, bali ni sheria mama na mkataba kati ya wananchi na Serikali.

Alisema suala la Bunge kuweka maazimio na utaratibu ikiwemo kutunga sheria ya kuratibu mchakato wa mabadiliko ya katiba ni la muhimu na la haraka wakati huu ambao tmakundi mbalimbali ya kijamii yamejitokeza na kuweka misimamo yao wazi ya kutaka katiba mpya na mengine kutangaza kuanza kuandika miswada ama rasimu ya katiba husika.

Alisema kusipokuwa na utaratibu wa haraka wa pamoja, kila mdau atakwenda kwa mfumo wake hali ambayo inaweza kuzalisha mpasuko katika jamii kutokana na suala la katiba mpya.

" Sio jambo baya makundi ya kijamii kuandaa rasimu sifuri za katiba, lakini kama kila kundi likaandaa rasimu yake halafu utaratibu wa kuunganisha maoni ya makundi mbalimbali kupitia chombo kinachokubalika na kinachohusisha wadau wote kuchelewa taifa linaweza kuingia kwenye malumbano, ndio maana ni muhimu kwa utaratibu huo kuwekwa kupitia mkutano wa bunge wa Februari," alisema. Alisema hoja binafsi anayokwenda kuiwasilisha bungeni haihusu maadhui ya katiba bali inahusu mchakato, ingawaje katika kuiwasilisha kuna masuala ya kimaudhui yatajitokeza kama sehemu ya kujenga hoja.

Alisema kama mwakilishi wa Chadema kwenye Kongamano la Madai ya Katiba Mpya, anatumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi na wadau kuendelea kutoa maoni kuhusu rasimu sifuri ya katiba iliyopitishwa na Kongamano la Wadau tarehe 17 Februari mwaka 2007 baada ya kuwasilishwa na Kamati ya Wataalamu iliyoongozwa na Dk. Sengondo Mvungi. Alisema katika kongamano hilo pamoja na kueleza ubora wa rasimu hiyo sifuri ikilinganishwa na katiba inayotumika kwa sasa wajumbe walieleza kasoro zilizopo kwenye rasimu sifuri ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya rasimu husika kukabidhiwa katika vyombo vya maamuzi hivyo kongamano likaazimia kwamba rasimu husika isambazwe na kila mshiriki kwa wadau kwa ajili ya kupata maoni.

Katika muktadha huo kongamano liliazimia kuipokea na kujadili rasimu ya sifuri kama mkusanyiko wa mawazo ya awali yaliyotoka kwa wadau kwa ajili ya kuchochea mjadala na fikra za umma kuhusu mchakato wa Katiba mpya.

"Maoni yaliyopokewa na Chadema kama mdau katika kipindi cha 2007 mpaka 2010 kwa ujumla yanaeleza kwamba rasimu sifuri iliyotolewa ina ubora zaidi ya katiba inayotumiwa sasa na Tanzania hasa katika maeneo ya: Muundo wa shirikisho; kuwatambua Watanzania; kutambua mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, kuwepo kwa maadili/tunu na misingi mikuu ya taifa, haki za binadamu nyingine zimeongezwa na zile zilizokuwemo awali zimepewa tafsiri pana, kupewa uzito wa ulindwaji, madaraka ya rais yamepunguzwa, mawaziri wanateuliwa nje ya wabunge, wabunge kuwepo wa majimbo, wa uwiano na wabunge wa taifa kutoka katika wagombea urais waliofanya vizuri; tume ya uchaguzi imeundwa na watu huru na kuwekewa uwakilishi mpana zaidi; uwakilishi katika kutunga katiba umepanuliwa kujumuisha wadau wa kisekta. Suala ni namna na hatua za kufanya ili serikali ikubaliane na matakwa ya umma kuhusu katiba mpya," ileleza taarifa hiyo.

Chanzo: Nipashe 27/12/2010

No comments: