Monday, December 20, 2010

Madai ya katiba mpya sasa yahamia bungeni

Mjadala kuhusu madai ya kutungwa kwa Katiba mpya, huenda sasa ukahamia bungeni, baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kutangaza rasmi kusudio la kutaka kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuliomba Bunge liazimie kuanzisha haraka mchakato wa suala hilo.

Azimio lingine ambalo amesema anakusudia kuliomba Bunge lipitishe, ni kuweka utaratibu wa kuitisha Mkutano Mkuu wa Kikatiba ili kushirikisha watu wengi kujadili kwa mapana na marefu, kuundwa tume ya kuratibu mchakato wa Katiba mpya na kufanyika kura ya maoni ili kupata mawazo ya pamoja.

Alitangaza kusudio hilo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema kusudio lake limezingatia kanuni ya 55 (1) ya Bunge, hivyo ataliwasilisha kwa Katibu wa Bunge ndani ya wiki moja kuanzia sasa ili aweze kuiwasilisha rasmi hoja hiyo katika Mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza Februari 8, mwaka huu.

Hata hivyo, alisema changamoto kubwa aliyonayo, ni namna gani wabunge wa vyama vyote, watakubaliana naye ili kwa pamoja Bunge liweze kupitisha azimio la hoja yake binafsi.

Alisema hakuwa na wazo la kuipeleka hoja hiyo katika Mkutano wa Bunge wa Februari, mwaka huu, ingawa tangu mwanzo alikwishakuazimia kuwa angehakikisha anaipeleka ndani ya uhai wa Bunge la sasa.

Mnyika alisema uamuzi wa kuharakisha kuipeleka katika Mkutano wa Bunge ujao, unatokana na kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wiki iliyopita katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari ya kutaka yafanyike marekebisho ya Katiba na si kutunga Katiba mpya, kuunda jopo la wataalamu na kwenda kumshauri Rais Jakaya Kikwete.

Alisema kauli hiyo ya Pinda inawapeleka Watanzania kwenye njia mbovu; kwani suala la Katiba si la serikali wala Rais, bali ni la wananchi na pia njia zote hizo, serikali imekwishakuzipitia, lakini zikafeli.

Mnyika alisema sababu ya kwanza iliyomfanya akusudie suala hilo, ni Katiba kuwa sheria mama, kwenye Ibara yake ya 63 Kifungu kidogo cha (1) na cha (2) Ibara ya 98 (1), imetoa mamlaka kwa Bunge kutunga sheria na kubadili Katiba.

“Hivyo, nimeona mahali mwafaka pa kufanya hivyo ni bungeni,” alisema Mnyika.

Alisema sababu ya pili, ni Katiba kuwa mkataba kati ya mtawala na mtawaliwa na kwamba, katika kufikiwa mkataba wowote, mwenye mali ndiye anayepaswa kuanza mchakato.

Kutokana na hali hiyo, alisema katika suala la Katiba, wenye mali ni wananchi, hivyo kwa kuzingatia Ibara 63, ambayo imeipa Bunge mamlaka ya kuisimamia serikali, akiwa mwakilishi wa wananchi, ameona abebe jukumu hilo kwa vile mwananchi mmoja mmoja hawezi kuamua.

Alisema sababu ya tatu, ni uzoefu kuonyesha kuwa tume zote zilizowahi kuundwa na serikali kupitia Rais, hazikuweza kukata kiu ya wananchi ya kuleta mabadiliko ya Katiba na mapendekezo yake kuwekwa kabatini.

Mnyika alisema tume hizo ni kama ile ya Thabiti Kombo iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1976; ya pili ya marehemu Jaji Mkuu wa zamani, Francis Nyalali iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, mwaka 1991; na ya tatu ya Jaji Mstaafu, Robert Kisanga, iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa mwaka 1998.

Alisema maoni ya Tume ya Thabiti Kombo yalipelekwa Halmashauri Kuu (NEC) ya Tanu kisha baadaye yakapelekwa bungeni, ambako yalijadiliwa kwa saa tatu tu na kuipitisha Katiba ya sasa ya mwaka 1977.

Mnyika alisema kitendo cha maoni ya tume hiyo kupelekwa NEC ya Tanu, badala ya Bunge, kinathibitisha kwamba, Katiba iliyopo, ina mawazo ya chama kimoja na ndio maana ina udhaifu mkubwa na imewekewa viraka na kufanyiwa marekebisho mara 14 kwa miaka 33.

“Kuna katiba za baadhi ya nchi zina miaka 50, lakini hazijawahi kufanyiwa marekebisho,” alisema Mnyika.

Alisema mfano mwingine ni mapendekezo ya Tume ya Jaji Kisanga, ambayo kwanza Mkapa aliyeiunda, aliishambulia kuwa ilifanya mambo mengine zaidi, ambayo hakuituma na baadaye akachagua mambo aliyoyataka kwenye mapendekezo ya tume hiyo.

Mambo hayo ni kama suala la mgombea urais kutozidi asilimia 50 ya kura na kumpa rais mamlaka ya kuteua watu 10 kuwa wabunge, lakini yaliyohusu mabadiliko ya Katiba yakatupwa.

Mbunge huyo alisema sababu ya nne ya kudai Katiba mpya, ni kuwapo changamoto mpya zinazoikabili nchi, ambazo alisema Katiba iliyopo imeshindwa kuzitolea majibu.

Baadhi ya changamoto mpya, ambazo alisema Katiba iliyopo imeshindwa kuzitolea majibu, ni uchaguzi kuwa tishio la amani kutokana na kufanyika kwa misingi isiyokuwa huru na haki. Nyingine ni marekebisho ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanyika baada ya kufikiwa maridhiano ya kumaliza chuki na uhasama wa kisiasa miongoni mwa Wazanzibari visiwani humo, ambayo alisema baadhi ya vifungu vinapingana dhahiri na Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Changamoto nyingine mpya, alisema ni kupungua kwa utamaduni wa uwajibikaji serikalini, ambako kumesababisha kukithiri kwa ufisadi nchini na hivyo kuhitajika Katiba mpya.

Alisema hakuna ulazima wa kuunda jopo la wataalamu kwa ajili ya kushughulikia Katiba iliyopo kama ilivyotamkwa na Waziri Mkuu Pinda, kwani huko nyuma suala hilo lilifanywa, lakini halikuzaa matunda yaliyotarajiwa na wananchi.

Kutokana na hali hiyo, alisema iwapo jopo hilo litaundwa, itakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za walipakodi.

Akijibu swali kwamba, Katiba wanayoidai, wananchi wengi hawaijui, Mnyika alikiri, lakini akasema sababu ya wananchi wengi kutoishika wala kuisoma Katiba iliyopo, ni upatikanaji wake kuwa adimu na ghali.

Hata hivyo, alisema hali hiyo haimaanishi kuwa hawajui udhaifu wa Katiba hiyo, kwani taarifa za tume zilizoundwa na serikali, ni ushahidi tosha kwamba, wanaujua vyema.

Alisema japo wananchi wengi hawaijui Katiba, hoja zao zinathibitisha kuwa wanajua udhaifu wake na kutolea mfano wa namna, ambavyo wamekuwa wakihoji kuhusu haja ya kuwapo tume huru ya uchaguzi.

Mnyika alisema wananchi wametoka kwenye mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini Katiba iliyopo bado inashikilia mawazo ya zamani, huku uundwaji wake ukiwa umefanyika bila kuushirikisha umma.

Katika hatua nyingine, Mnyika, ambaye pia ni Katibu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amelaani kitendo cha polisi cha kumpiga Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) kwa vile ni kinyume cha sheria, haki za binadamu, utawala bora, Katiba, sheria za Jeshi la Polisi, kinga, haki na madaraka ya Bunge.

Chanzo: Nipashe-20/12/2010

No comments: