Thursday, December 23, 2010

Serikali ilaani vurugu Ivory Coast

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeitaka serikali kulaani hadharani matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya demokrasia ya kimataifa unaofanywa na Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo na wafuasi wake nchini humo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya chama hicho iliyotolewa na Mkurugenzi John Mnyika (Mb) ilisema, Rais Jakaya Kikwete anatakiwa kutamka hadharani kumtambua Alassane Ouattara kuwa ndiye mshindi wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo na kulaani vitendo vinavyofanywa na Gbagbo na wafuasi wake.

“Inashangaza kwamba wakati Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na serikali za nchi mbalimbali ndani na nje ya Afrika zimetoa matamko ya wazi serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya diplomasia ya kimya.

“Hii ni tofauti kabisa na wakati Mwalimu Nyerere ambapo Tanzania ilikuwa mstari wa mbele na kutoa misimamo ya wazi ya kukemea vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza CHADEMA inatambua kwamba Rais Kikwete alizungumzia kidogo matatizo ya Ivory Coast wakati akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Amani katika eneo la Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika hivi karibuni nchini Zambia.

Katika mkutano huo Rais Kikwete alieleza kwamba suala la Ivory Coast linashughulikiwa na mikono salama na akaonyesha matumaini yake kwamba pande mbili zenye mgogoro zitafikia makubaliano.

“Kauli hii ya Rais Kikwete inalea vitendo vya ukiukwaji wa misingi ya demokrasia vinavyofanywa na Laurent Gbagbo na wafuasi wake kwa kuwa inatoa fursa kwa mgombea ambaye taasisi zote huru zimetamka kuwa ameshindwa katika uchaguzi kuanza majadiliano na aliyeshinda badala ya kumpisha katika uongozi wa nchi,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilisema serikali ya Tanzania inatakiwa kueleza msimamo wake kwa uwazi, ili kuondoa mashaka kwamba ukimya wake unatokana na Rais Kikwete kukosa uhalali wa kimaadili wa kukemea vitendo vya ukiukwaji wa demokrasia na mchakato wa uchaguzi uliomuingiza madarakani kuhojiwa kutokana na tuhuma za matokeo ‘kuchakachuliwa’ katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.


Chanzo: Tanzania Daima (Disemba 2010)

No comments: