Wednesday, December 29, 2010

Mnyika awaasa maafisa ustawi wa jamii

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, amewataka maofisa ustawi wa jamii nchini kuepuka tabia ya kukaa ofisini huku wakiwaacha watoto wa mitaani wakihangaika bila ya kuwa na msaada wowote.

Amewataka maofisa hao kuvitembelea vituo vya watoto yatima ili kubaini maendeleo na mwenendo wa wake baada ya malalamiko mengi kutolewa juu ya vituo hivyo, kuwa vingi vinaendeshwa kwa ajili ya maslahi ya wanaosimamia au kumiliki vituo hivyo.

Mnyika alitoa kauli hiyo jana wakati wa chakula cha mchana alichokiandaa na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha ‘Boona Baana’ kilichopo Sinza Mori, Dar es Salaam.

Alisema hivi karibuni, Taifa limekuwa na idadi kubwa ya watoto yatima na wale wa mitaani, jambo linalohitaji ustawi mkubwa wa kuhakikisha wanapata elimu, malazi na huduma zingine, na kusisitiza kwamba hilo halitaweza kufanikiwa endapo maofisa hao wataendelea kujifungia ofisini.

“Idara ya Ustawi wa Jamii ndiyo yenye jukumu kubwa la kuwashughulikia watoto hawa wanaoishi katika mazingira magumu, kamwe tatizo hilo halitaweza kuisha endapo maafisa hawa wataendelea kulifumbia macho hilo kwa kukaa maofisini,” alisisitiza Mnyika.

Aidha, alisema hivi sasa kuna idadi kubwa ya vituo vya kulelea watoto yatima katika maeneo mbalimbali, hivyo maofisa hao wa ustawi wa jamii wanatakiwa wavichunguze vituo hivyo ili kubaini namna vinavyoendeshwa kwani yapo madai kuwa baadhi yao vinaendeshwa kwa maslahi ya waliovianzisha.

Katika chakula hicho, Mnyika alitoa msaada wa vifaa vya shule pamoja na vyakula vyote vikiwa na thamani ya Sh 500,000 kwa ajili ya watoto hao wanaoishi katika kituo hicho wapatao 10.

Mratibu wa kituo hicho, Marco Bara, aliwaomba wananchi kuacha tabia ya kuwachukulia watoto wa mitaani kama wakaidi na badala yake wasaidiane kuwaondoa katika maisha magumu yanayowakabili.

Chanzo: Habari Leo 27/12/2010

No comments: