Wednesday, December 29, 2010

Mnyika: Katiba ina mapungufu 90

HATIMAYE Mbunge wa jimbo la Ubungo jijini Dar e Salaam, John Mnyika (CHADEMA), amewasilisha taarifa ya hoja binafsi ya Katiba kwa Katibu wa Bunge na kueleza mapungufu 90 yaliyo katika Katiba ya sasa. Akiwasilisha hoja hiyo jana na kupokewa na Kaimu Katibu na Mkurugenzi wa Idara ya Taarifa za Bunge, Eliakim Mrema, kwa barua yenye kumbukumbu namba BJMT/01/2010 ambapo Mrema aliahidi kuifanyia kazi barua hiyo kwa mujibu wa kanuni za Bunge ya Mwaka 2007.

Akizungumza mara baada ya kuwasilisha taarifa hiyo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi ya kambi ya upinzani, Mnyika alisema Katiba ya sasa haikidhi mahitaji ya Watanzania kwa kuwa ilitungwa katika mfumo wa chama kimoja.
“Nichukue fursa hii kueleza kwamba Katiba ya sasa inampa mamlaka makubwa mno Rais, pamoja na vyombo vya kiutendaji; hakuna Mtanzania mwenye uwezo wa kuhoji hasa katika mfuno huu wa vyama vingi na Katiba hii imekuwa na matundu mengi ambayo yanakibeba chama kimoja waziwazi. Hakika mchakato huu ni wa Watanzania wote!” alisema Mnyika.

Alisema taarifa ya hoja binafsi aliyoiwasilisha ni kwa ya ajili ya Bunge kwenda kutimiza wajibu wa Kikatiba ambapo wabunge wana wajibu wa kuilinda kwa kutambua uwakilishi wao kwa wananchi waliowapa dhamana ya uwakilishi katika chombo hicho cha maamuzi.

Alisema hivi sasa taasisi za utendaji kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Tume ya Maadili ya viongozi wa umma uteuzi wa watendaji wake uko chini ya Rais hivyo kushindwa kutoa mwanya wa kuhoji.

Alisema Katiba ni muhimu na ya haraka wakati huu ambapo tayari makundi mbalimbali ya kijamii yamejitokeza na kuweka misimamo yao wazi ya kutaka Katiba mpya na mengine kutangaza kuanza kuandika miswada ama rasimu ya Katiba husika


Chanzo: Tanzania Daima-28/12/2010

1 comment:

Anonymous said...

Hongera Mh. Mnyika kuwasirisha mapendekezo hayo.

Sisi wakereketwa wa CHADEMA tunapenda kujua kwa kina uliyandikwa kwenye hayo mapendekezo walau tujue nini cha kuwaeleza wenzetu, wanautuuliza sana huku mtaani hasa majirani zetu wa kijani kijani.

Pia tunapenda utupatie hayo mapungufu 90 yaliyo kwenye katiba, ili tujue vizuri kwa nini tunahitaji katiba mpya.

Ahsante,
Mdau.