Tuesday, December 29, 2009

Mwaka 2009 umeanza na kuisha kwa ufisadi na malumbano bila uwajibikaji

Mwisho wa mwaka ni wakati wa kutafakari tulipotoka, tulipo na tunapotaka kwenda katika mwaka mpya. Kwa taifa ni fursa ya kufanya tafakari hiyo katika muktadha wa hali na mwelekeo wa taifa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Yapo masuala na matukio mengi ambayo tunaweza kushawishika kuyatafakari mathalani: hali ya mwaka huu wa 2009 kugubikwa na migomo mbalimbali vyuoni, makazini nk; kutetereshwa kwa misingi ya utawala wa sheria na haki kwa kurejea hukumu ya kesi ya Zombe na wenzake, kesi ya Dereva wa Mohamed Trans, kesi ya Ajali ya Chenge inayoendelea, kesi za Mramba, Yona, Liumba nk; yaliyojiri ndani ya CHADEMA wakati wa mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama; mabomu ya Mbagala; ripoti ya UN na tuhuma kwa Tanzania na watanzania kuhusu silaha nk; ajali na maafa mbalimbali; kuzinduliwa kwa mkakati wa kilimo kwanza; chaguzi za marudio Busanda na Biharamulo; hali ya kisiasa Zanzibar; orodha ni ndefu sana.

Lakini kwa Tanzania toka CHADEMA na viongozi wake kwa kushirikiana na vyama vingine tutoe orodha ya mafisadi (list of shame) mnamo Septemba 15, 2007; ni vigumu kutathmini na kupanga mikakati ya kidemokrasia na kupanga dira ya maendeleo bila kutafakari kuhusu hoja ya ufisadi na haja ya uwajibikaji katika taifa letu.

Hivyo katika kuyatafakari masuala na matukio yaliyojitokeza mwaka 2009 ni muhimu kujadili jinsi mwaka husika ulivyoanza na kuisha kwa ufisadi na malumbano bila uwajibikaji kamili wenye kukabiliana na changamoto za ujinga, umasikini na maradhi katika nchi yetu ambayo Mwenyezi Mungu ameijadilia utajiri wa rasilimali.

Mwaka ulianza mwezi Januari 2009 kwa malumbano yaliyotokana na malalamiko ya Salum Londa (Mjumbe wa NEC CCM na Meya wa Manispaa ya Kinondoni) na Yusuph Makamba (Katibu Mkuu wa CCM) yaliyotokana na kauli ya Halima Mdee bungeni mwishoni 2008, akimtuhumu Makamba “kumlinda” Meya Londa, ambaye alisema anatuhumiwa kwa ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na uuzaji wa viwanja maeneo ya Kawe, Kinondoni. Kwa hiyo, mwaka ulianza kwa tuhuma za ufisadi zilizohusu Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni; manispaa ambayo sehemu kubwa ya viongozi wakuu wa serikali na vyama vya siasa wanaishi.

Mwaka unaisha mwezi Disemba 2009 jinamizi la ufisadi limeendelea kuinyemelea Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, baada ya kukubali kuuziwa matrekta 27 ya kuzoa takataka yasiyokuwa na viwango kutoka kwa mfanyabiashara, Yusuf Manji. Dalili za kuwepo vitendo vya ufisadi zimeonekana wazi baada ya Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo ambalo ndilo lililopitisha zabuni hiyo kugawanyika katika makundi mawili na kuendeleza malumbano bila uwajibikaji. Lakini tuhuma dhidi ya halmashauri hii haziishii kwenye zabuni pekee bali uuzaji na umilikishaji wa ardhi kinyume cha taratibu mathalani Eneo la Ufukwe wa Coco (coco beach) na umegaji wa kiwanja cha shule ya Msingi Kawe nk. Naandika haya mkononi mwangu nikiwa na taarifa ya siri yenye mihutasari na saini za viongozi wa CCM na Halmashauri ya Kinondoni ambazo zinathibitisha wazi kabisa tuhuma hizo zikitaja kwa majina na viwango vya rushwa ambazo zilitolewa ikiwemo kwa madiwani katika kashfa hizo. Taarifa hizo nitaendelea kuziweka hadharani mwaka 2010 kwa lengo la kuchochea uwajibikaji na mabadiliko ya kweli.

Ikumbukwe kwamba kauli za kupinga ufisadi ziliendelea mwezi Februari, mathalani Dk Wilbroad Slaa akihutubia wananchi sokoni Kariakoo Dar es salaam, katika mkutano wa Operesheni Sangara alirudia mwito wa kutaka Rais Mstaafu Mkapa ashtakiwe kufanya biashara akiwa Ikulu; kuchukua Kiwira kwa bei chee na kushinikiza kulazimisha wabunge waivunje NBC yeye kuchota Milioni 500 kutoka ABSA kama cha juu. Katika mkutano huo uliorejewa na vyombo vya habari Dr Slaa alitetea msimamo wake kuhusu posho za wabunge akieleza dhambi kwa yeye kupokea 180,000 kwa siku wakati walimu wanapokea kiasi hicho kwa mwezi. Mishahara na posho za wabunge ni moja ya masuala yaliyozusha malumbano na mgawanyiko hususani miongoni mwa wabunge katika mwaka huu unaomalizika na kuendeleza mjadala kuhusu kukosekana kwa usawa katika mgawanyo wa keki ya taifa katika nchi yetu.

Mwezi Machi; Wakati sakata la ujenzi wa maghorofa pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) likinguruma mahakamani kwa kushitakiwa maofisa wake wawili waandamizi, tuhuma nyingine za ziada zikajitokeza tena kuhusu ujenzi wa majengo hayo. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, akathibitisha tuhuma hizo kwa kutamka hadharani kuwa Taasisi ya Kuchunguza na Kudhibiti Rushwa (Takukuru) kuchunguza mashaka yaliyomo kwenye mkataba wa bima wa ujenzi wa maghorofa hayo na kuchukua hatua stahili. Ilibainika kuwa mkataba wa bima wa ujenzi wa makao makuu ya BoT unaacha maswali mengi kutokana na kuwa na mapungufu kadhaa mathalani kukosekana kwa dhamana ya bima, gharama za bima zilizolipwa kuonekana zimezidi kiwango, kuingia mikataba miwili inayofanana na kuwepo kwa taarifa zinazokinzana kwenye mkataba wa bima wa awamu ya pili; ujumla tuhuma hizo zilihusu matumizi ya zaidi ya bilioni 10 za kitanzania. Mwezi huu wa Disemba mwaka unaishia kwa tuhuma zingine hivi sasa zikuhusu matumizi ya anasa ya zaidi ya Bilioni moja(yaani milioni zaidi ya 1000) kutumika kwa ujenzi wa nyumba ya gavana wa BOT ndani ya mkoa wa Dar es salaam ambapo wananchi wakufa kwa magonjwa yanayotibika kwa kukosekana kwa dawa katika hospitali za serikali; huku malumbano yakiendelea bila uwajibikaji.

Mwezi Aprili 2009 zikatolewa taarifa za ziada ufisadi uliojikita zaidi katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Ukaanikwa mtandao wa rushwa, ukiukaji sheria na kanuni za matumizi ya fedha za umma, unafanywa na maofisa wa wizara hiyo; kwa kiwango kikubwa ukiibuliwa kutokana serikali ya Norway inayofadhili mradi wa matumizi bora ya maliasili kushindwa kuivumilia hali hiyo iliyokuwa ikiendelea chini kwa chini kwa muda mrefu. Katika taarifa ya tathmini ya matumizi ya fedha za wafadhili wa Norway ambayo ilitolewa kipindi hicho, maofisa wa wizara hiyo si tu walithibitika kuwa mafisadi, walionekana pia kufanya vitendo kadhaa vya jinai, ikiwa ni pamoja na kughushi nyaraka kwa lengo la kufanya ubadhirifu. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi wa matumizi ya fedha kwa miradi mitano, iliyokuwa chini ya Programu ya Udhibiti wa Maliasili (MNRP) ulifanywa na Athur Andreasen na Kailas Bhattbhatt ambayo ilianika kwa maelezo na vielelezo ufisadi na ubadhirifu huo uliohusu mabilioni ya fedha.

Mwishoni mwa Mwezi Aprili 2009, msamiati ambao ulipotolewa kupitia orodha ya mafisadi 15 Septemba 2007 ulikuwa mgeni kwa wananchi walio wengi ambao walizoea kutumia neno rushwa; ukapata mwenza wake.

Hali hii ilitokana na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kuwataja watu watano wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi mkubwa nchini ambao aliwaita ‘mafisadi papa’ na kuitaka serikali iwashughulikie haraka iwezekanavyo ili kuinusuru nchi kuyumbishwa nao. Hatua hiyo ilizua malumbano makali zaidi ambayo wengine walifikia hatua ya kuona kwamba yangeligawa taifa na kusababisha uvunjaji wa amani.

Mwanzoni mwa mwezi Mei mmoja wa ‘mafisadi papa’ Rostam Aziz(Mbunge wa Igunga CCM) akajitokeza na badala ya kujibu tuhuma yeye akaishia kuja na msamiati mwingine ‘fisadi nyangumi’; hali hiyo ilisababisha miezi miwili iliyofuatia kugubikwa na malumbano bila uwajibikaji. Hiyo ilikuwa ni awamu ya kwanza ya mwaka wa 2009.

Hali hiyo imejirudia tena katika awamu ya pili ya kufungia mwaka 2009; mafisadi wameendelea kuachwa wakitamba na kuliteteresha taifa. Mtiririko wa matukio unaonyesha kwamba CCM imetekwa na mafisadi, mivutano ndani ya NEC yao na mpasuko wa dhahiri katika kikao cha Wabunge wao na wazee wa chama chao cha hivi karibuni Dodoma na kauli zilizofuatia baada ya hapo za kulumbana hadharani bila uwajibikaji; ni ishara za hali hiyo. Katikati ya malumbano hayo alikuwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Utawala Bora), Sophia Simba ambaye kwa nafasi yake kama waziri ambaye anasimamia taasisi nyeti kama usalama wa taifa na ile ya kuzuia na kudhibiti rushwa(TAKUKURU) na kudhihirisha rangi halisi za watawala walioko madarakani na haya ya kubadili mfumo mzima wa utawala.

Mwezi Julai 2009 ilitoka kauli ya matumaini kwamba bado wapo watanzania wanaotaka uwajibikaji. Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Mhashamu Dk. Valentino Mokiwa, alitaka serikali kuziendesha kesi za ufisadi kwa kasi, vinginevyo zitaonekana kama ni usanii kwa wananchi; akitoa mwito kwamba kesi hizo zimalizike kabla ya mwaka 2010 ili taifa liweze kusonga mbele.

Kauli hiyo ilitolewa wakati ambapo taifa likiwa katika malumbano kuhusu waraka wa wakatoliki. Kwa ujumla, mjadala kuhusu waraka huo ulionekana kuligawa taifa katika makundi mawili makubwa; ndani ya bunge na nje ya bunge. Hata vyama vya siasa navyo viligawanyika katika makundi mawili; vingine vikiutetea waraka huo na vingine vikiupinga. Mwezi mmoja baadaye, mnamo Agosti ukatolewa waraka mwingine- waraka wa waislamu. Hata hivyo, katika hali ilizua malumbano mengine tofauti yenye ishara ya mgawanyiko kuhusu waraka huo; wakati kiongozi wa Kamati Kuu ya Saisa ya Shura ya Maimamu Tanzania, Amiry Mussa Kundecha anatangaza kuzindua waraka huo; Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) likatoa kauli kuwa halikuwa taarifa kuhusu kuzinduliwa kwa waraka huo na wala halihusiki.

Kuna mambo kadhaa ya kutafakari kutokana na masuala na matukio hayo: Mosi, ni ishara ya kupanuka kwa mapambano dhidi ya ufisadi, ambayo mwanzoni yalibezwa kuwa ni chuki ya CHADEMA na wapinzani wengine dhidi ya serikali. Kutolewa kwa nyaraka hizo ni ishara ya viongozi wa dini kuingia katika vita hii wakijikita zaidi katika kuhamasisha haki na kupinga aina zote za dhambi na dhulma kama sehemu ya kusimamia maadili. Pili, ni kuibuka kwa mjadala wa nafasi ya dini katika siasa hususani katika uchaguzi. Ni wazi kwamba mgawanyiko wa kimtazamo na kimaamuzi kuhusu matukio hayo na masuala yaliyojitokeza utakuwa ni moja ya hoja na changamoto za msingi tunapoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kutokana na matukio na masuala hayo; mikutano ya Bunge la Bajeti lililoanza mwezi Julai na hata Mkutano wa mwezi Novemba 2009 yalijitokeza mambo ambayo yaacha maswali kuhusu dhamira yetu ya pamoja ya kupambana na ufisadi na kutetea rasimali za taifa.

Pamoja na Spika wa Bunge kuapa kwamba suala la utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Richmond kumalizika kikao cha Novemba; kikao kimemalizika bila suala hilo kumalizika. Ufisadi wa EPA nawe umefanyiwa usanii wa hali ya juu wa kisiasa, kwa bahati mbaya ukiongozwa na mkuu wa nchi. Hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa bungeni ya kutamka msamaha kwa waliorejesha fedha za wizi; ni sehemu ya hali hiyo. Mhimili wa Bunge, umeshindwa kumwajibisha Rais katika hili kwani hata hotuba hiyo ya Rais pamoja na ahadi za Spika kuwa ingejadiliwa bungeni mpaka leo haijawahi kutolewa. Nachukua fursa hii kutoa mwito kwa ikulu kuiweka wazi Hotuba hiyo ya Rais Kikwete ijadiliwe na umma; kwani muda mrefu sana umepita toka tuelezwe kwamba hotuba hiyo imerudishwa ikulu ‘kukarabatiwa’. Kushindwa huku kuwa na kumbukumbu za Bunge zilizohadharani (Hansard) za suala nyeti kama hili la Hotuba ya Rais Bungeni kuhusu hali ya taifa (state of the nation address) na aibu kwa Spika aliyetangaza kuendesha bunge kwa viwango na kasi.

Funga mwaka ikawa ni masuala yaliyojiri kwenye kongamano la Mwalimu Nyerere mwanzoni mwa Mwezi Disemba na matokeo ya mjadala uliofuatia baada ya tukio hilo wa takribani mwezi mzima ambalo limeanika hadharani uongozi ulioko madarakani hususani namna ambayo wako tayari kutetea ufisadi. Kinara wa siasa hizo za ‘mipasho’ akiwa ni Katibu Mkuu wa chama kinachotawala(CCM), Yusuph Makamba. Ama kwa hakika mwaka huu ulikuwa na kauli ambazo ni aibu kwa taifa na zinafaa kuhifadhiwa kwa ajili ya kumbukumbu za vizazi vijavyo. Lakini watanzania wakumbuke kwamba kutekwa huku na mafisadi, chanzo chake ni viongozi wengi walioko madarakani kuingizwa kwa nguvu ya fedha za ufisadi.

Hali hii inatufanya tukumbuke; mabadiliko ya kweli katika taifa letu hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale. Kwa falsafa ya chukua chako mapema; Tanzania yenye neema haiwezekani. Tuunganishe nguvu kubadili mfumo wa utawala; mabadiliko yanawezekana. Tunahitaji uongozi wenye dira na uadilifu wa kulikomboa taifa; mwaka 2010 tuache malumbano tusimamie uwajibikaji.

2 comments:

Fadhy Mtanga said...

John, makala imesimama na kuandikwa baada ya uchambuzi wa kina.
Tutafika tu!

John Mnyika said...

Asante sana Fadhy, Pamoja Tunaweza; heri ya mwaka mpya

JJ